Kwanini Quran iliteremshwa?

The Answer

Dear Brother / Sister,

Quran iliteremshwa ili kuwafanya watu na majini, waliowajibishwa kwasababu wana akili na utashi, wafahamu ibada kama ilivyoelezwa katika aya ifuatayo: [Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.” (adh-Dhariyat, 56)] na kupata furaha kamili duniani na ahera. Quran si neno lisilo na malengo: [Wala si mzaha.”(at-Tariq, 14)] ni vigezo na kaida timilifu zinazobainisha ukweli mbali na uongo, jema dhidi ya ovu na zuri dhidi ya baya.

Ni sifa ya bainishi ya Quran, ambayo lengo lake la kipekee ni uongofu na furaha kwa wanadamu, kutumia mtindo unaolingana na lengo hilo, wakati mwingine kuiambia akili, wakati mwingine hisia, wakati mwingine dhamiri na wakati mwingine nyoyo za wasomaji wake, ili kuvutia nadhari zao kwenye mataifa yaliyotangulia, mbingu na ardhi, himaya ya mimea na wanyama, ukweli mwingi wa kisaikolojia, kifalsafa na kimaadili na kuwaomba wasomaji wake wayatafakari masuala hayo.

Kama Muhammad Asad anavyoliweka hilo, “Kamwe kitabu chochote - ikiwemo Biblia – kilichosambazwa kwa watu wengi, na kwa muda mrefu sana, hakijatoa jibu lenye kufahamika la swali hilo:

“Nifanyaje ili nipate maisha mema duniani na furaha katika ahera?

Quran inaendelea kuwa juu ya sifa zote za kibinaadamu kama vile jiografia na mbari; haitaji majina kamili ya watu na mahali inapopataja; inawapa watu mafundisho ya elimu ya ujumla kwa kuyataja hayo.

Quran ni kielekezi cha uokovu wa wanadamu wote katika zama zotena mahali kwa ujumla. Ni kielekezi chenye kuonesha njia za ufumbuzi kwa waumini na hususani walio katika mgogoro na matatizo. Dhana ya kuongoza (hidayah kwa Kiarabu) inayoashiria njia ya kutokea kwa wale wasiojua upande wa kwenda jangwani inatangamana na nafasi nya Quran kwa ajili ya wanadamu wote.

Quran, inayosema kuwa mwanadamo yupo katika hasara kwa kuapa kwa neno zama {al-Asr, 1-2}, ni “mbinu ya uokovu” na “chelezo” kwa ajili ya mwanamume, aliyevurugikiwa kwasababu ya migogoro ya kiroho, mmomonyoko wa kimaadili na matatizo ya kijamii katika nyakati zilizopita na leo.

Hiki ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatoe watu kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa!” Ibrahim, 1

Njia pekee ya ufumbuzi kwa jamii iliyopoteza maadili yake na sifa zake nzuri na ambayo hali yake ya sasa na ya ijayo imepata giza la kukosa ustawi na furaha imeoneshwa katika Kitabu cha Allah kama ifuatavyo:

Bila shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinacho bainisha. Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye njia iliyo nyooka.(al-Maida, 15, 16)

Itikadi za kibinadamu, zinazokuja pamoja na tamko kuwa zitatatua matatizo ya wanadamu, hupunguza matatizo kwa majibu yake ya muda mfupi na yasiyokamilika; kwa upande mwingine, Quran inatoa njia za kudumu na kamilifu za uokovu zinazofaa katika kila zama na mahali. Quran inamfananisha mtu anayejaribu kutatua matatizo kwa kutumia majibu yaliyotolewa na wanadamu kama mtu asiyejiweza anayetembea hatua chache pindi radi yenye mwanga mkali wa kufifisha macho inapopiga katikati ya giza na kisha anasimama {2/20}. Quran inaelekeza kwenye lililo sahihi zaidi. {17/9}. Kwa kuwa, ni ukweli kamili. {13/1; 17/105}.

Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini. Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.(Yunus, 57-58)

Quran ni ponyo na faraja, na kwa hivyo ni rehema, kwa ajili ya maradhi na matatizo yote. Nyoyo zilizofifia kwasababu ya uchafu wa kiroho na madhambi na zilizogeuka sugu na kupata maradhi {2/10; 6/43; 8/49} zinaweza kutakasika, kulainika na kuponywa kwa Quran:

Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. (az-Zumar, 23)

Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua! (ar-Rad, 28)

Kwa hivyo, Quran inakuwani ponyo na rehema kwa ajili ya watu ambao nyoyo na akili zao zimevurugika kwasababu ya ghiliba za kishetani. Nyoyo za watu wenye kuondokana na matatizo na maradhi hayo zinaongoka na uoni wao unakuwa hai.

“Hii (Qur'ani) ni hoja zinazo toka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu na rehema kwa watu wanao amini. {7/203; 45/20}

Quran ni kitabu kitukufu ambacho {6/155}, kama Hadhrat  Umar (ra) anavyoliweka hilo, “Allah hufungua macho yaliyofumba, masikio yasiyosikia na nyoyo zilizofungwa kwa kutumia Qur’an.”

Jina mojawapo la Quran ni “dhikr”, yaani, mawaidha; na jina jingine ni “tadhkira” yaani mwonyaji na mkumbushaji. Quran ni mkusanyiko wa mawaidha na maonyo yanayomfundisha na kumkumbusha mwanadamu juu ya majukumu yake na yanayomwongoza kwenye heri na ukweli:

“Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.” (Ibrahim, 14/52)

Quran inamfahamisha mwanadamu kuhusu majukumu yake kwa upande wake yeye mwenyewe, Mola wake Mlezi, watu wengine na maumbile. Inawafundisha wale wasiotambua majukumu yao na inawakumbusha wale wanaoyasahau majukumu yao. Inawaonya vikali wale wasiotimiza majukumu yao kwa makusudi. 

Rejea kuu kwa kila Muislamu anayeuchagua Uislamu kuwa ni dini yake na anajisalimisha kwa Allah ni Quran. Atajifundisha kanuni za maisha zitakazomletea furaha duniani na ahera kutokana na Quran. Atajifundisha kinachohitajika kuamini na cha kukataa, kipi ni chema na halali na kipi ni kiovu na haramu, anachotakiwa kufanya na anachotakiwa kukiepuka kutokana na Quran. Atautakasa moyo wake, kuuimarisha na kujisalimisha kwa Allah na kuhuisha imani yake na msisimko wake kwa Qur’an. {9/124; 16/102}

“Na inapo teremshwa Sura wapo miongoni mwao wasemao: Ni nani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia Imani? Ama wale walio amini inawazidishia Imani, nao wanafurahi.(at-Tawba, 9/124)

Sema: Ameiteremsha hii Roho takatifu kutokana na Mola wako Mlezi kwa haki, ili awathibitishe wale walio amini, na kuwa ni uwongofu, na ni bishara kwa Waislamu. (an-Nahl, 16/102)

Atajifundisha mazuri ya Peponi na kitisho cha mateso ya Jahanamu kutoka katika kitabu kitukufu cha Allah; Hivyo, atajitahidi kuendesha maisha bora na atatenda kwa umakini zaidi ili kuepuka madhambi na amali mbaya. Kwa kifupi, muumini atapata kila kitu katika Qur’an kuhusu jinsi ya kufanya ili apate radhi za Allah:

Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu. (an-Nahl, 16/89)

Hata hivyo, mtu asihitimishe kutokana na aya hii kuwa Quran ni ensaiklopidia au kitabu cha sayansi. Si kitabu kinachotaja nadharia za muda mfupi za kisayansi; ni mwogozo wa maisha. Ni kitabu cha mwongozo kilichotumwa na Allah, aliyetuumba sisi na anayeyajua zaidi maumbile yetu kuliko sisi; kinatuonesha jinsi ya kutumia viwiliwili vyetu vya kupita katika dunia hii ya mpito:

Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini. (Yusuf, 12/111)

Quran ni neno sahihi la mwisho la Allah. Wanadamu, waliohutubiwa kwa njia ya ufunuo tangu Hadhrat Adam (as), mtu wa kwanza, ambapo Quran, ambayo ni hazina bora inayothibitisha yaliyo kweli katika mafundisho yaliyotangulia ya upwekeshaji,  yaliyosahaulika, yaliyopotea au kubadilishwa na inasahihisha makosa yaliyomo ndani mwao. Wanadamu wanaweza kujua upi ni ukweli wa kiungu na lipi si sahihi na ushirikina, shukrani ziiendee Quran, ambayo ni “Furqan” (Kipambanuzi baina yake na shari).

Quran kwa hakika ni kipimo kwa ajili ya Waislamu. Akili ya Muislamu, mtizamo wa kidunia na mwenendo unapaswa ufundishwe na Quran. Anapaswa kuangalia kila kinachomjia kwa jina la elimu na utamaduni wa Kiislamu kwa utumia Quran, moja baada ya kingine; na anapaswa apambanue baina ya lililo sahihi na lisilo sahihi, la kweli na la kishirikina, lilo bora na lililozushwa.

Isisahaulike kwamba fursa adhimu ya Uislamu ni kwamba wafuasi wake wanayo Furqan, (mpambanuzi) kitabu ambacho hakijakumbwa na mabadiliko yoyote, kilichopo chini ya hifadhi ya Allah na kitakachobakia kuwa ni kigezo kisicho na doa kinachopambanua baina ya ukweli na uongo. Ni kitabu kisicho na kasoro hata chembe.

Waumini hufanya rejea kwenye Quran ili kujifundisha siri za dunia na ahera; pia hurejea kwenye Quran na sunnah bora ya Mjumbe wa Allah, ambaye ni Quran hai, kuhusu masuala wasiyoafikiana.

Kwa kifupi, Quran ni kitabu kitukufu cha rejea ambacho thamani yake kamwe haitapungua mpaka Siku ya Kiama kwa ajili ya waumini. Kitabu hiki cha hazina ndicho rejea pekee ambayo waumini watafanya rejea ili kutatua namna zote za matatizo ya kiroho yakiwemo masuala wasiyoafikiana.

Quran si kitabu kinachoshughulikia baadhi ya mambo ya kihistoria, kijamii, kifalsafa na kimaadili kwa njia ya kinadharia. Hata hivyo, kinalenga katika kuiweka jumuia iliyoundwa kwa maadili ya kidunia na kanuni za kiroho zinazoziweka. Inalenga kwenye kuondoa kila kinachohusiana na ukosefu wa fadhila na shari na kuwafanya wanadamu wote wajisalimishe kwa Allah, yaani, Uislamu, kama ilivyobadili mojawapo kati ya jamii za kijinga zaidi duniani na kuwa jamii bora zaidi {2/193}; ni kitabu cha kimapinduzi. Quran iliteremshwa ili itekelezwe kivitendo na watu waitii.

"Fuateni mliyo teremshiwa kutoka kwa Mola Mlezi wenu, wala msifuate rafiki au walinzi wengine badala yake. Ni machache mnayo yakumbuka." (al-Araf, 7/3)

Kila anayeiamini Quran, kimsingi, Mtume (s.a.w), anaitii na kushikamana na kanuni ilizoziweka:

Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa. (az-Zukhruf, 43/43, 44)

Quran “ni kitabu kitukufu cha Allah ambacho hamtapotea kamwe kama mtashikamana nacho.” {Ibn Majah} ni kamba imara ya Allah itakayokupelekeni kwenye mwangaza, ukomavu, na heshima kama mtaishikilia; Hakuna kulazimishana katika dini. Ukweli utajitokeza dhahiri mbali na uongo; mwenye kukataa Uovu na akamwamini Allah atakuwa amekamata kishikizo cha kutumainia, kisichovunjika.”

“Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.(al-Baqara, 2/256); {al-Baqara, 2/256, 257; Aal-i Imran, 3/103}

“Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.(Aal-i Imran, 3/103)

Jamii inayoshikamana na kamba ya Allah na kutii kanuni za ufunuo inakuwa na furaha duniani na ahera. Wale wanaoupa mgongo ukweli wa kiungu na kukiacha kitabu kitukufu cha Allah kwa kutokukitii watakosa furaha katika sehemu zote mbili za ulimwengu.

Kanuni za kimaadili, nasaha na mapendekezo yaliyo katika Quran yanakuwa muhimu yanapotekelezwa kivitendo. Mathalani, nasaha zifuatazo za kiungu hazitakuwa na manufaa yoyote kama hazitafanyika kivitendo:

“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya.

Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki...”

Wala msiyakaribie mali ya yatima...”

“na
timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa. (katika Siku ya Hesabu).”

Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa...”

Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa. (katika Siku ya Hesabu).”

Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.

Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako Mlezi.(al-Isra, 17/32-38)

Kitabu cha Wazi Wazi, Chenye Kufahamika, Kilichorahisishwa:

Kama inavyoonekana katika aya 32-38 za sura ya al-Isra tulizozinukuu kama mfano hapo juu, aya za Quran zina kanuni zenye kutendeka zinazoweza kufahamika hata kwa jumuia yenye ujinga mwingi. Quran haina utatanishi, wala kutokufahamika, wala kitabu cha kale kinachoweza kufahamika kwa wataalamu, wanasayansi na maulamaa tu au chenye alama za siri zinazoweza kutafsiriwa nao peke yao. Hukaririwa mara kwa mara kwa ujumla mwanzoni mwa sura za Quran ambapo Quran na aya zake viko wazi na vyenye kufahamika.

Katika Quran, kila kitu kimeelezwa “kupitia mifano mbalimbali” {18/54; 20/113} na kwa kina {6/55, 56, 126; 41/2-3}. Quran imerahisishwa ili ifahamike kupitia sitiari na mifano:

Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka? (al-Qamar, 54/17, 22, 32, 40)

“Kwakuwa wale wa mwanzo waliohutubiwa na Quran hawakujua kusoma na kuandika, Shari'ah tukufu za Uislamu zilikuwa rahisi. Shari'ah iliteremshwa katika mfumo ambao ungefahamika na kutekelezwa kwa urahisi na wale wanaohutubiwa bila ya kuhitajika elimu yoyote au ubobezi. Kudai kinyume chake ni kinyume na msingi wa Shari'ah. Watu wa mwazo kuhutubiwa hawakujua kusoma na kuandika; kwa hivyo, shari'ah iliyoteremshwa ilikuwa nyepesi. Vinginevyo, wangesema, “Iko juu ya kiwango chetu; haifanani na maneno yetu; hayo ni maneno tusiyoyajua au kuyafahamu, n.k...” {41/44}.

Licha ya hivyo, Allah anaeleza, Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo. {2/286}; Wala (Allah) hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini” {22/78}. Kwa sababu za kiutekelezaji, Shari'ah ilibidi iteremshwe katika lugha na mtindo ambao ungeweza kufahamika kwa kila mtu.” Shatibi

Quran imeelezewa kama ifuatavyo katika hadithi:

“Baadhi ya watu ni watu wa Allah. Mjumbe wa Allah alipoulizwa, 'Ni kina nani hao?', Alisema, 'Hao ni watu wa Quran; hao ni watu wa Allah na marafiki zao.” (Tirmidhi)

“Rehema na wingi humiminikia mahali na malaika na utulivu huzingira mahali ambapo muumini anasoma Quran kwa unyoofu na kwa kutaka radhi za Allah.” (Tirmidhi)

Harith al-Awar anasimulia: “Pindi tulipokuwa tunapita njia ya msikitini, niliwakuta watu wameacha kumtaja Allah na kuingia katika mazungumzo yasiyofaa. Kwa hivyo, nilimwendea Hadhrat Ali (ra) na kumwambia niliyoyaona.

Akaniuliza, 'Unasema kweli, ni hivyo?'

Nilipomhakikishia kuwa hivyo ndivyo ilivyokuwa, alisema: 'Nilimsikia Mjumbe wa Allah akisema,

“Tazama! Mfarakano utatokea! Hapo hapo nikamuuliza: ‘Ni ipi njia ya kujinusuru nao? Ewe Mjumbe wa Allah! Alijibu: Ni kutii kitabu kitukufu cha Allah.

Kina habari zote kuhusu yaliyowatokea jumuia za kabla yenu, habari za mifarakano na misukosuko itakayotokea baada yenu na ishara za Siku ya Kiama.

Pia ina hukumu kuhusu mambo yatakayotokea miongoni mwenu (kuhusu mambo kama vile imani-ukafiri, utii-uasi, kilichoruhusiwa-kilichokatazwa, n.k.). N
i kipambanuzi baina ya ukweli na uwongo.

Iko makini katika kila inachokitaja, Hakuna neno ndani mwake ambalo ni la kupita bure tu au la nje ya mada. Mwenye kuangukia katika upuuzi kwa kutokukizingatia na kutokutenda kulingana nacho, Allah atamwangamiza. Kama yeyote atatafuta uongofu mahali pengine Allah atamwacha apotee.

Ni kamba madhubuti ya Allah. Ni ukumbusho wa hekima, na ni njia iliyonyooka kabisa. Inahifadhi nafsi zinazoitii zisiharibiwe na upotovu na ndimi zenye kuisoma dhidi ya kutatizika. Wanazuoni wa Qur’an daima hutamani zaidi yaliyomo ndani mwake. Kukisoma mara kwa mara hakumchoshi msomaji wake; wala msomaji hapotezi ladha kwa kurudiarudia kukisoma. Mastaajabu yake makubwa yanayowashangaza wanadamu hayaishi kamwe.

Ni aina ya kitabu ambacho, pindi walipokisikia, majini iliwabidi wakiri kuwa, '
Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya ajabu. Kwa hakika Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini.' (Surah al-Majini, 72/1-2) Mwenye kukitamka, atakuwa anasema ukweli. Mwenye kutenda kulingana nacho atalipwa. Mwenye kuhukumu kulingana nacho, atakuwa mwadilifu. Mwenye kuwalingania watu kukiendea, atawaongoza kwenye njia iliyonyooka. Ewe Awar! Jifundishe vyema maneno haya mazuri.” (Tirmidhi)

Kwa muhtasari, Quran, “Ni kitabu cha muujiza”, kitakachokomesha siku za giza tunazoishi ndani mwake na matatizo na machungu tunayoumia na kitakachowaongoza wanadamu wote kwenye “furaha ya wote”, kiko katika utumiaji wetu kama hazina isiyo na kifani. Tunachohitajika kufanya ni kusoma hii “mbinu ya wokovu” kwa macho maangalifu ili tupate majibu ya maswali ya leo na kuwa na nguvu na msisimko uliokuwepo katika siku za mwanzoni mwa Uislamu.

Nyenzo:

(Kur'an Nedir, Nasıl Okunmalıdır, A. Yıldız-Ş. Özdemir, Pınar Yayınları)

Maswali juuyau islamu

Author:
Maswali juuyau islamu
Subject Categories:
Read 13 times
In order to make a comment, please login or register
MASWALI YENYE KUFANANA