Kamari maana yake ni kutoa au kuchukua fedha au bidhaa kutegemeana na kitu fulani aambacho hakijulikani mwisho wake. Haijalishi ni jina gani, mchezo wowote au kuwekeana dau (bet) wenye sifa hii na ambao huchezwa kwa mrejesho wa fedha au bidhaa huitwa Kamari. Neno “maysir” lililotajwa katika Kur’an limetokana na neno “yusr”, lenye maana huru/uhuru, ambalo linaonesha kwamba fedha au bidhaa hupatikana au kupotezwa kirahisi kwenye Kamari.
Kamari ni njia ya kupata pesa isiyokuwa stahiki yako ambayo humfanya mtu amsahau Muumba wake, humzuia mtu kutekeleza ibada ya swala, humpelekea uvivu, kuondosha nguvu za kufanya kazi na kusababisha chuki na uadui baina ya watu. Aina zote za Kamari, ambazo zinasababisha vidonda visivyotibika kwa maisha ya mtu mmoja mmoja au jamii, ni haramu katika Uislamu.
Yafuatayo yameelezwa katika Kur’an kulingana na jambo hili:
“Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa ubatili,..” (al-Baqara, 2/188; an-Nisa, 4/29).
“Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, kamari, kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni chukizo na ni kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali, (al-Maida, 5/90, 91; Ibn Abidin Raddu'l Mukhtar, İstanbul 1307, V, p. 355; Hamdi Yazır, Hak Dini Kur'an Dini, İstanbul 1960, II, p. 766).
Kamari na uharamu wake:
Hakuna tofauti kati ya pombe na Kamari katika kukatazwa na kuhesabiwa kuwa dhambi. Allah anaziharamisha katika aya moja:
“Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, kamari, kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni chukizo na ni kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa.” (al-Maida, 5/90).
Aina zote za michezo ya bahati nasibu yenye faida na hasara huzingatiwa kuwa Kamari. Kucheza Kamari maana yake ni kujipatia fedha za mtu au bidhaa kwa dhulma na ni kuiba fedha au bidhaa za mtu kwa makusudi. Kamari ni janga la kijamii. Daima unaonekana kuwa uovu huu haribifu uliokatazwa na Uislamu bado unaharibu familia nyingi. Kwa wale ambao hucheza Kamari kwenye meza hadi asbuhi ni kwa tamaa zinazosababishwa na ulafi na matamanio, hawa hupoteza afya zao, utajiri, maadili na fedha; wanapoteza pia hisia za kibinadamu. Wanaoshinda leo hupoteza siku nyengine.
Wake, watoto na maskini wana haki kwenye fedha zinazopotezwa kwenye Kamari. Pesa inayopatikana kwa Kamari nayo si halali.
Kwa kadri Kamari inavyoshamiri, uharibifu kwenye kijamii utaongezeka. Kazi imeondolewa na uvivu. Uzalishaji katika biashara hupungua. Kamari huleta matendo maovu kama vile ulevi, kusema uongo, ulafi, kisasi na mauaji.
Kamari husababisha pia vurugu, migogoro na kulekeza familia. Kuna watu wengi ambao huuza dini yao, heshima na nchi yao kutokana na Kamari na ambao huondosha aina zote za maadili matukufu.
Kamari huathiri ndani ya muda mfupi kama ulevi unavyoathiri. Inakuwa ngumu sana kujitoa. Hivyo basi, Kamari na ulevi ni tabia za hatari sana.
Aina zote za michezo ya bahati nasibu ambayo huwa unashinda au unapoteza fedha kama vile kete, karata, bahati nasibu, mapuli ya mpira wa miguu, mchezo wa loto, kuwekeana dau, na michezo ya farasi ijulikanayo kama sweepstakes yote huzingatiwa kama Kamari.
Michezo yote ya bahati nasibu huchezwa kwa kujifurahisha na kupoteza muda katika hatua za awali. Kwa kadri mtu anavyoshinda, hujikuta anacheza kwa lengo la kujifurahisha na matamanio ya kushinda. Kwa kadri anavyopoteza, huendelea kucheza kwa lengo la kurudisha alichopoteza. Kisha, huwa mcheza Kamari. Inapaswa isisahauliwe kwamba wale wanaopoteza kila kitu kwenye Kamari, ambao huuza chochote walichonacho na kuishi maisha ya kikafir/hanasa na umaskini, ambao huharibu wake na watoto wao, kwa kuwafanya waanze kucheza Kamari kwa kujifurahisha na kujiburudisha.
Ni jukumu la msingi kujitenga mbali na Kamari na vile vile kuwakinga watu wanaotuzunguka hasa wanafamilia wasijiingize kwenye Kamari. Jukumu la kuwakinga wanafamilia kutokana na uharibifu na mambo maovu na kuwaelimisha kuhusu aina ya maisha ambao Allah na Mtume wake wanayataka, limepewa viongozi wa familia kama ilivyo kwenye Kur’an:
“Enyi mlio amini! Jiokoeni nafsi zenu na familia zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa.” (at,Tahrim, 66/6).
Ikiwa michezo kama mchezo wa bao (backgammon), sataranji (chess), checkers, karata, tenisi, na mabilidi (billiards) huchezwa kwa lengo la kamari kwa kuhatarisha fedha, nayo pia huzingatiwa kama Kamari.
Kuna hadithi mbali mbali za Mtukufu Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) ambazo zinakataza kucheza bao la kamari (backgammon): “Mtu anaecheza bao la kamari (backgammon) huzingatiwa kama amemuasi Allah na Mtume Wake.” (Abu Dawud, Adab, 56; Ibn Majah, Adab, 43; Malik, Muwatta', 6; Ahmad b. Hanbal, Musnad, IV, 394, 397, 400). “Hali ya mtu anaecheza bao (backgammon) kisha akaswali ni kama hali ya mtu anaetia udhu akiwa na usaha na damu ya nguruwe kisha akaswali.” (Ahmad b. Hanbal, V, 370).
Kwa mujibu wa makatazo ya jumla ya kucheza bao la Kamari (backgammon) katika hadithi hizi, wanazuoni wengi wa Kiislamu wanasema kwamba kucheza mchezo wa bao wa watu wawili ujulikanao kama backgammon hairuhusiwi. Ibn al-Musayyab na wanazuoni wengine wa Kiislamu wamebeba mtazamo kwamba si haramu kucheza backgammon iwapo lengo si Kamari. Karata na dominoz (dominoes) huzingatiwa ni sawa na backgammon.
Mchezo wa sataranji (chess), ambao hujulikana kama “shatranj” kwa kiarabu, ulijitokeza kipindi cha maswahaba baada ya kufa kwa Mtume Muhammad (rehma na Amani ziwe juu yake); kwa hivyo, hakuna hadithi yoyote ya Mtume inayozungumzia mchezo wa sataranji. Maswahaba na waliokuja baada yao (Tabiun ) wametoa fikra tatu kuhusu sataranji (chess):
Kwa mujibu wa Maswahaba na wanazuoni waliokuja baada ya Maswahaba (Tabiun) kama vile Abdullah b. Abbas, Abu Hurayra, Ibn Shirin, Hisham b. Urwa, Said b. al-Musayyab, Said b. al-Jubayr, wanasema inaruhusiwa kucheza sataranji (chess).
Kwa mujibu wa Imam Shafii, sataranji (chess) ni makuruhu tanzihi; kwa mujibu wa Abu Hanifa, Malik na Ahmad b. Hanbal, ni haramu.
Kwa kuzingatia kwamba mchezo wa sataranji (chess) ni kama mchezo wa kutumia akili na mchezo wa kuchemsha ubongo (chemsha bongo) kuliko mchezo wa bahati nasibu na hakuna makatazo ya moja kwa moja kuhusu mchezo huu. Hata hivyo, inafahamika kuwa Maswahaba waliufananisha mchezo huu na mchezo wa backgammon. Ukweli ni kwamba, yafuatayo ni maelezo yanayosimuliwa na Abdullah b. Umar:
“Mchezo wa sataranji (chess) ni mbaya zaidi kuliko backgammon.” Inaelezwa kuwa Hz Ali huuzingatia mchezo huu kama Kamari. (Ibn Kathir, Tafsiru'l-Qur'ani'l-Azim, İstanbul 1985, III, 170). Kwa upande mwengine, inasimuliwa kwamba Yahya b. Sad alisikia yafuatayo kutoka kwa Imam Malik: “Hakuna uzuri wowote kwenye mchezo wa sataranji (chess); ni makuruhu kucheza sataranji na michezo mingine ya bahati nasibu.” Imam Malik alikuwa akisoma aya ifuatayo wakati akitamka sentensi hiyo: “…Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu wa haki. Na kipo kitu gani baada ya haki, isipokuwa upotovu tu?” "(Yunus, 10/32; see Malik, Muwatta, Ru'ya, 7).
Chikaz (checkers) ni mchezo kama sataranji (chess). Kwenye mchezo wa tenisi na mabilidi (billiards), ni mchezo maarufu. Inahitaji kuruhusiwa ispokuwa chembe chembe za haramu zikiingizwa.
Kwa kuhitimisha, kuna masharti manne ya muhimu kwa michezo inayochezwa kwa ajili ya kujipumzisha, burudani na kujifurahisha bila ya kuwa na azma ya kucheza Kamari ili kidini iruhusiwe:
a. Lazima isiwafanye watu kukosa au kuchelewa kwenye swala za faradhi.
b. Watu wasitarajie faida yoyote ya kitu chochote.
c. Wachezaji wajizuie kutamka maneno mabaya na maneno ambayo si muhimu wakati wa mchezo.
d. Watu wasipoteze muda wao kwa kucheza kupita kiasi ambapo hawawezi kuizingatia tena kama sehemu ya kupumzika na kujiburudisha.