Kuzunguka Kaaba kunawakilisha dhana ya upwekeshaji. Maana yake kuhusu maisha ya kijamii si kuuacha umoja na kujaribu kudumisha umoja huu. Maana yake katika maisha ya mtu mmoja mmoja yana ukweli mwingi wa kina. Mbingu ina tabaka saba; mwanadamu ana nafsi saba. Kila kuizunguka Kaaba kunawakilisha awamu moja, ngazi; mwanadamu anashikilia hatua moja na imeinuliwa mpaka katika mbingu ya saba, juu ya ulimwengu wa kiyakinifu. Licha ya hayo, inamaanisha kupanda kutoka hatua ya chini kabisa ya nafsi, yenye hatua saba, mpaka juu kabisa. Yaani, kutoka nafs al-ammarah (nafsi inayoamrisha uovu) mpaka kwenye nafs al-mutmainnah (nafsi iliyotulia); kutoka maisha ya kinyama mpaka katika maisha ya kiroho.
Kuzunguka Kaaba ni namna ya ibada iliyochukuliwa kutoka katika mpangilio wa ulimwengu. Sayari hulizunguka jua, elektroni kuzunguka kiini, nondo kuzunguka mshumaa; kuzunguka kitovu hicho kunamaansha utii pamoja na mapenzi.
Mwenyezi Mungu anasema yafuatayo katika Quran:
“Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake...” (al-Isra, 44)
Maendeleo ya sayansi yamesaidia kuieleza aya hiyo. Kwa hakika, wakiwemo viumbe ambao walidhaniwa kuwa hawana uhai, kila kitu kilikutwa kuwa kina atom kadhaa. Elektroni daima huzunguka viini vya atom na kwa kufuata utaratibu maalumu; Quran imeeleza kuwa huko ni kumtukuza Allah. Kwa hivyo, kuzunguka Kaaba, ambayo ni alama ya Uislamu, kunamaanisha kuupenda Uislamu, kuizunguka kama nondo na mtu kujishikiza kwa Allah.
Kuabudu; ni mja kutimiza majukumu kama vile takbir, hamd, shukr kwa ajili ya Allah kwa namna Alivyoamuru. Kwa hivyo, hali ya kila kiumbe kutimiza majukumu inaweza kuitwa kuwa ni ibada yake kwa Allah na kumtukuza.
Kufahamu Tawaf: Kilugha, tawaf inamaanisha kugeuka, kutembea, n.k. katika hali ya kukizunguka kitu. Kila kitu ulimwenguni, kuanzia atom ndogo sana mpaka galaksi (kundi la nyota) kipo katika hali ya tawaf. Katika atom, elektroni hugeuka kuzunguka kiini, ambacho ni kama moyo, kwa kasi sana; katika galaksi, mabilioni ya nyota huzunguka kitovu cha galaksi kwa kasi kubwa. Hivyo huzunguka kana kwamba vinamwaabudu Muumba aliyeviumba. Kama ilivyoelezwa katika Quran, kila kimoja kinaogelea katika njia. (Yasin, 36/40)
Mwonekano wa makumi kwa maelfu ya Waislamu wanapotembea kuzunguka Kaaba ni kama mwonekano wa galaksi ikigeuka pamoja na mabilioni ya nyota. Kwa hivyo, ni muhimu mtu kuwa katika njia ili kupata furaha kamili ya kiroho katika tawaf. Muislamu mwenye kujiweka kwenye njia hii na kudhibitiwa na mtiririko huo wa kiroho anapata furaha ya kuwa tone moja katika bahari ya waumini. Kuzunguka Kaaba kunazingatiwa kuwa ni alama ya muhtasari wa ulimwengu na viumbe, na kujisalimisha katika takdiri za kiungu.
Watu kutembea kwa taabu katika shawt (duru) tatu za mwanzo za tawaf kunaitwa ‘ramal’ na kuliacha wazi bega la upande wa kulia huitwa ‘iztiba’.
Maana ya kihistoria ya vitendo vitatu vilivyofanywa vilikuwa ni kudhihirisha uwezo na kuwahofisha wapinzani. Waislamu wa Makkah walipohamia Madinah, hali ya hewa ya Madinah iliwaathiri na wakadhoofika kidogo. Waliporudi Makkah baada ya miaka saba ili kufanya umrah, walimweleza Mtume kuhusu hali hiyo. Papo hapo, aliwaambia Maswahaba zake waonekane wenye nguvu kwa washirikina na watembee katika hali ya kuogofya wakati wa kupita mbele yao; na Maswahaba wakafanya hivyo.
Bila ya shaka, hali yao ya kutembea kwao kwa kuogofya ilitosha kuonesha kuwa walikuwa imara katika siku hiyo. Vipi kuhusu siku hizi? Mahujaji wataoneshaje kuwa wako imara siku hizi? Uwezo wa kiyakinifu, nguvu za kiroho, nguvu za kimaadili … Tumepoteza nini, wapi na kivipi? Tunawezaje kuyarejesha hayo? Kwa hakika tunapaswa kuyatafakari hayo katika wakati wa hajj.
Ramal (kutembea katika hali ya kuogofya), kulikokuwa kunafanywa ili kuonesha nguvu ya Waislamu kwa Makuraishi kwa mujibu wa kauli ya Ibn Abbas, kulikuwa ni sunnah pindi Mtume alipotembea kama hivyo katika wakati wa shawt (duru) tatu za mwanzo za Hajj ya Kuaga. Hadhrat Umar alisema, baada ya kutoa maelezo juu ya Hajar al-Aswad,
“Kwanini tunaendelea kudumisha ramal? Huwa tunaifanya ili tuonekane imara machoni mwa washirikina, ambao walisema tulikuwa dhaifu. Kwa hakika, Allah amewaangamiza.” (Bukhari, Hajj, 57)
Ingawa Umar alidhani kuwa sababu ya ramal haikuendelea kuwepo, hakutaka kuacha jambo alilofanya Hadhrat Mtume na kwa hivyo aliendelea kulifanya jambo hilo. Huenda ramal iliendelea kwa sababu Waislamu mara zote walihitajika wawe imara na kwa sababu hawakutakiwa kuisahau.
Mtu huanza tawaf huku Kaaba ikiwa katika upande wake wa kushoto. Maana yake ni ya kisitiari. Moyo wa mwanadamu, ambao ndio anaoutazama Allah, unaielekea Nyumba ya Allah katika tawaf. Allah anautazama moyo wa mtu, si sura yake, umbo, pesa na mali. Katika hali hii, kuna uhusiano mzuri kati ya Kaaba na moyo wa mtu. Kwa hivyo, moyo wa mtu unaikabili Kaaba katika wakati wa tawaf. Pia unaashiria kuwa tawaf inapaswa ifanyike kwa unyenyekevu.
Mtu anafurahia kuwa muumini anayeizunguka Kaaba. Ni vigumu sana kuipata furaha hiyo kwingine, ambayo huja waziwazi kabisa na kwa shauku. Hisia za ukaribu anaouhisi mtu katika mahali hapo patakatifu huwafanya mahujaji wajihisi wako nyumbani. Mahujaji hujihisi kana kwamba wako nyumbani kwa sababu sehemu ya mbele ya Kaaba huonekana maarufu, manukato yake huwa yenye kujulikana sana na burudani yake huwa pana sana kiasi kwamba muumini hatapenda avutiwe zaidi na kingine chochote.
Hakuna tofauti baina ya watu wanaoswali swala ya jamaa; halikadhalika, hakuna tofauti baina ya watu wanaozunguka Kaaba. Waumini wote wako sawa hapo. Hakuna dalili ya mtu kutofautiana na wengine. Hapo kuna umoja, ambao ni alama ya upwekeshaji. Ni muhimu kupotea katika bahari ya waumini na kuyeyukia katika jamaa.
Kumgeukia mtu na kumzunguka kama nondo ni kitendo kinachoonesha utii wa dhati na kuwa anaweza kujitolea vyovyote tu kwa ajili ya mtu huyo. katika hali hii, kuzunguka Kaaba ni ishara ya kumgeukia Muumbaji Mtukufu, kwa kuinama mbele Yake na kutomwabudu yeyote mwingine isipokuwa Yeye tu.
Katika wakati wa kuzunguka, hajji anapaswa aheshimu stahiki ya Allah na kuwa na mapenzi yaliyo baina ya hofu na matumaini. Wakati anapozunguka, hajji anapaswa ajenge nyumba ya imani, yaani, moyo wake, kama Hadhrat Ibrahim na Hadhrat Ismail, mwanaye, walivyojenga Nyumba ya Allah kwa kuizunguka. Kaaba ni nyumba Yake na moyo ndio Anaoutazama. Hajji anadumu katika kuitazama Kaaba, anaiangalia kwa makini na anaona utukufu wake; halikadhalika, Allah anautazama moyo wa mja Wake na kuusikiliza. Ni kama alivyosema Mtume kwa kifupi,
“Allah hatazami sura zenu, umbo au mali bali nyoyo na amali zenu. (Muslim, 1, 33)
Ndivyo hivyo duniani na ahera. Kama katika maelezo ya aya ya 88 ya sura ash-Shuara, katika Siku ya Kiama, ambapo hakuna kitakachokuwa na manufaa yoyote, Allah hana haja ya dhahabu wala fedha bali moyo mzuri.
“Ewe hajji! Usidhani wanataka dhahabu au fedha yako. Wanataka moyo mzuri katika siku ambayo mali na watoto havitasaidia.”
Kwa hakika, katika utamaduni wetu, ma-sufi hutumia vivumishi vyote ambavyo hutumika katika kuieleza Kaaba kwa ajili ya moyo na kuuita moyo ni Nyumba ya Allah. Au, huwa wanaiita “Bayt al-haram” (nyumba tukufu) na wanatumia maneno hayo hayo kwa ajili ya moyo kwa sababu moyo ni nyumba ya Allah na ni haram (imeharamishwa) kwa yeyote isipokuwa mpendwa kuingia humo. Kwa hakika, hadithi ifuatayo aliyoisema Mjumbe wa Allah wakati wa kuzunguka Kaaba inathibitisha hayo.
“(Ewe Kaaba!) Wewe ni mzuri; harufu yako ni nzuri sana. Umashuhuri na hadhi yako ni vitukufu. Hata hivyo, ninaapa kwa Allah, ambaye mkononi mwake upo uhai wangu, kuwa utukufu wa kinga ya muumini pamoja na mali yake na uhai ni mkubwa kuliko utukufu wako.” (Ibn Majah, Fitan 2)
Rejea:
1- Kur'ân'in Getirdigi - Emin Isik.
2- Kurban Kesmenin Psikolojik Temelleri - Doç Dr. Ali Murat DARYAL.
3- Kur'ân-i Kerîm ve Açiklamali Meâli - Türkiye Diyanet Vakfi.
4- Diyanet Islâm ilmihali.
5- Hac Rehberi - Irfan YÜCEL - Türkiye Diyanet Vakfi.
6- Diyanet yayinlari (hacci anlamak)