FAQ katika kifungu cha Hijabu-Kilemba-Kujistiri

1 Inadaiwa kuwa hakuna aya inayohusu tasattur (stara) katika Quran. Je unajibu vipi madai hayo?

Katika Enzi za Jahiliyya, watu wengi hawakuwa na maadili mema na staha. Maadili, Usafi wa tabia na utukufu yalikuwa ni mambo yaliyozungumzwa lakini hayakufanywa. Wanawake walikuwa wakivaa bila ya staha kama ilivyo leo na walikuwa wakijifaharisha kwa kuonesha sehemu zao za siri. Dini ya Uislamu, ambayo imetumwa kama rehema ya kiungu, iliweka baadhi ya amri na kanuni ili kuwarekebisha watu waliokuwa katika ufisadi. Amri mojawapo kati ya hizo ni kuhusu wanawake kujisitiri kwa ma-jilbab:

“Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao.“ (al-Ahzab: 59)

Kuna mitazamo michache kuhusu jilbab ni nini:

1- Jilbab ni kanzu ndefu au joho lenye kupwaya linalositiri mwili wote.
2- Ni nguo ya kupwaya inayovaliwa juu ya joho.
3- Ni kitambaa cha kufunika kichwa, shingo na mabega.
4- Ni vazi linalositiri sehemu ya juu ya mwili na kushuka chini mpaka tumboni.

Khalil, ambaye ni mwalimu wa Sibawayhi anasema, “Maana mojawapo katika hizo inaruhusiwa.” (as-Siraj al-Munir Juz. 3. uk. 271) Mwanamke muislamu anatakiwa ajisitiri mwili wake wote isipokuwa mikono yake na uso. Ikiwa mtu anaamini hayo lakini hayatendi, anakuwa mwenye kufanya dhambi. Hata hivyo, ikiwa mtu atayakanusha hayo, anatazamwa kuwa ameritadi. Ni upotovu kukimbilia tafsiri ambazo Uislamu hauzipokei ili kuharibu imani ya watu.

2 Je kuna aina ya stara iliyoamrishwa na Uislamu? Ni lipi lengo la tasattur (kujistiri)? Nini maana ya “vazi la uchamungu (taqwa)”? “Kwa nini tusitiri viwiliwili vyetu katika zama hizi?”

Stara (tasattur) ni jambo la lazima ya uumbaji

Kusitiri ni sifa mojawapo inayoziba njia zinazoelekea kwenye uzinifu. Kusitiri ni jambo la kimaumbile; ni jambo la lazima ya uumbaji. Soma jinsi Badiuzzaman anavyoeleza hilo :

Kijitanda ni jambo la kimaumbile kwa wanawake na hulka yao inavyotaka. Kwakuwa wanawake ni dhaifu na laini, na kwa kuwa wanahitaji hifadhi na msaada wa mwanamume kwa ajili yao na watoto wao wanaowapenda zaidi kuliko maisha yao wenyewe, wana utashi wa kimaumbile wa kufanya wao wenyewe wapendwe na si kuchukiwa, na kutokukaripiwa.

Pia, wanawake saba kati ya kumi ama ni wazee au wabaya, na hawataki kuonesha umri na ubaya wao kwa kila mtu. Au wana wivu, na hawataki kuonekana wabaya katika uhusiano na wengine walio wazuri zaidi. Au wao huogopa kushambuliwa au kashfa, na kimaumbile hutaka kujisitiri ili wasishambuliwe, wala kutuhumiwa suala la kutokuwa waaminifu mbele ya waume wao.

Ni dhahiri kuwa watu huchukizwa na mwonekano wa wale wasiowapenda au wenye kuchusha; wao hufadhaishwa nao. Pia, kwa kuwa mwanamke ambaye maadili yake hayajaharibika ni mwenye hisia na huathirika kirahisi, kwa hakika atavunjika moyo kutokana na mwonekano mbaya ambao athari yake imeshakuwepo kimwili, kwa hakika, hayo yana sumu. Huwa tunasikia pia kuwa wanawake wengi wamechoka kuwa kitu cha nadhari, na huwalalamikia polisi, kwa kusema: “Mahayawani hawa hutukazia macho na kutusumbua.” Hayo yanamaanisha kuwa kutokujitanda kwa mwanamke katika ustaarabu wa zama hizi ni kinyume na maumbile yao. Na licha ya kuwa ni kulingana na maumbile yao, amri ya Qur’an kuwa wajisitiri, inawaokoa wanawake—migodi hiyo ya rehema itakuwa na thamani ya masahibu wengi sana daima milele—dhidi ya kudhalilishwa, kutwezwa, yaliyokatika utumwa, na unyonge.

Zaidi ya hayo, wanawake kimaumbile ni wenye kuwaogopa wanaume wageni, na kuwa na wasiwasi nao. Hofu kimaumbile hutaka wanawake wajisitiri. Kuwa dhaifu, kuumbwa kwao kunataka kwamba kwa kujisitiri wenyewe hawachochei hamu za wanaume nje ya viwango vilivyoshurutishwa vya undugu, wala kuachilia fursa yoyote ya shambulizi; umbo lao dhaifu linatoa onyo kali. Inaonekana kuwa makoti yao ni ngao na ngome.

Hali mbaya ya leo kwa wanawake, ya mmomonyoko wa kimaadili waliyo nayo vijana wetu, na matokeo ya mmomonyoko huo hupiga katika nyuso zisizo na aibu za wanaopinga stara ya wanawake na wanaochukulia kusitiri kuwa ni “utumwa”.

Mahusiano ya uhakika na ya nguvu, mapenzi na huba baina ya wanaume na wanawake hayaji tu kutokana na mahitaji ya maisha ya kidunia. Ndio, mwanamke si tu ni mwandani wa mumewe katika maisha ya kidunia, yeye ni mwandani wake katika maisha ya milele pia.

Kwa kuwa yeye ni mwandani wa mumewe katika maisha ya milele, kwa hakika hatakiwi kuvutia macho ya wengine isipokuwa mumewe, rafiki na mwanadani wake wa milele, na asimkosee na kumsababishia wivu.

Matokeo ya mwujiza wa imani, kuamini kwake mahusiano ya mumewe kwake hayajabanwa katika maisha haya ya kidunia na mapenzi ya mumewe sio ya kama mnyama na ya muda mfupi tu, katika wakati wa uzuri wake; mume hushikilia kweli, penzi la dhati na kumheshimu kuhusu kuwa mwandani wake katika maisha ya milele. Na anakuwa na mapenzi hayo na kumheshimu, si katika wakati wa ujana wake tu alipokuwa mrembo, lakini pia anapozeeka na kuwa mbaya. Kwa hakika mke katika kulipa hilo, anapaswa kumwonesha mumewe urembo wake na kumpenda yeye tu; hayo hutakiwa na utu. Vinginevyo anaweza kufaidika kidogo sana na kupata hasara kubwa.

Maisha yenye furaha ya familia hudumishwa kwa kutumainiana baina ya mume na mke, na heshima na mapenzi ya moyoni. Mavazi yasiyo ya heshima na mwenendo usio wa taadhima huvunja matumaini, na kuharibu jambo la kuheshimiana na kupendana.

Ni dhahiri kuwa kila mmoja anataka watoto wengi. Hakuna taifa au serikali isiyosaidia kuzidisha idadi ya watu. Kwa hakika, Mtukufu wa Daraja Mtume (Rehema na amani zimfikie) amesema: “Oeni na muongezeke, kwani katika Siku ya Kiama nitajifaharisha kwa wingi wenu.”(Ibn Majah, Wedding, 1). Hata hivyo, kuacha vazi la Kiislamu kwa wanawake hakuongezi ndoa, kunazipunguza mno. (Leo ni jambo la uhakika kuwa nchi za Ulaya zinajaribu kuhuisha taasisi ya ndoa kwa kusaidia michango ya ndoa).

Nchi yetu haiwezi kulinganishwa na Ulaya, kwa sababu watu wa Ulaya si wachangamfu na baridi, kama ilivyo hali ya hewa. Asia, yaani, nchi za Kiislamu, kwa kiasi ni nchi za joto. Inajulikana kuwa mazingira huathiri hali ya kimaadili ya watu. Huenda katika nchi hizo za baridi nguo zisizo za heshima hazichochei hamu za mnyama na tamaa za kimwili za wanaume walio baridi, na kuwa ni njia ya tabia mbaya. Lakini nguo isiyo ya heshima inayodumu katika kuchochea hawaa za kimwili za watu wenye kuathirika kirahisi na wenye hisia nyepesi wa nchi zenye joto kwa hakika ndio sababu ya tabia mbaya na kupotea na kudhoofika kwa kizazi cha vijana na kupotea nguvu. Badala ya kujibu mahitaji ya kimaumbile kwa mwezi mmoja au kila wiki tatu au kama hivyo, mtu huliona hilo kuwa ni muhimu kila siku chache. Na kisha, kwa kuwa amewajibishwa kumwepuka mkewe pengine kwa wiki mbili katika kila mwezi kwa sababu ya matukio yasiyotarajiwa kama vile hedhi yake, ikiwa amezidiwa na hamu yake, ataenda katika nyumba zisizofaa. (Miwako, 24th Mwako, 1st-4th mifano ya hekima) 

Je kuna aina ya stara iliyoamrishwa katika Uislamu?

Hatuwezi kusema kuwa kuna jinsi maalumu iliyowekwa ya mavazi. Si Mtume wala Maswahaba wa Mtume waliokuwa na aina mahususi ya mavazi. Mbali na hayo, kuitathmini dini ya ulimwengu kama Uislamu wenye kuwaenea watu wote ndani ya wajibu wa mavazi ni kinyume na hali yake ya kilimwengu. Tunapoangalia namna ya mavazi ya Mtume, Chanzo cha Fahari ya utu, hatuoni aina moja mahususi. Mjumbe wa Allah wakati mwingine alikuwa akivaa kikoi na wakati mwingine kanzu na joho zuri la kupwaya.

Abdullah b. Jabir anasema: “Ninaapa kwa Allah kuwa nilimwona Mtume katika mbalamwezi akiwa amevaa joho na kanzu. Hakuna aliyependeza sana kwa nguo alizovaa isipokuwa Mtume.” Na siku moja, swahaba mwingine aliona kanzu nzuri ya Mtume na akamwomba ampe. Mjumbe wa Allah akaivua na kumpa zawadi.

Haiwezekani kupata kiwango kimoja cha nguo na huo ndio ushauri katika maisha yake. Mtume alikuwa akivaa namna ya mavazi ya kawaida katika jamii au yaliyofanana nayo. Na wakati mwingine alikuwa akivaa nguo iliyobadilishwa au iliyoboreshwa. Si haki kumkisia Mtume kuhusu kuvaa kanzu nyeusi. Kwa kawaida alikuwa akivaa nguo nyeupe za kung’aa; na wakati mwingine alikuwa akivaa nguo nyeupe, nyekundu na kijani. 

Tusing’ang’anie umbo na rangi ya nguo. Tusisababishe migogoro na ukinzani kwa kufanya hayo kuwa ni mambo ya mjadala. Watu wa Uthmaniya, mababu zetu, walichukua mafundisho ya Uislamu na kuyaunganisha na tamaduni zetu. Hawakuchukua namna ya mavazi bali linalopaswa kulijua; waliendelea na mavazi ya kabila la Kai, lililokuwa likivaliwa katika ardhi yao na kuliboresha kadiri wakati ulivyokwenda. Kwa nguo zao za zama za utukufu wetu, kwa nguo zao na majoho yaliyotengenezwa kwa ngozi, walionesha mfano kwa watu wa Ulaya kwa kitambo kirefu kilichopita. 

Kujisitiri ni amri ya Allah

Wanawake waliokuwa wakisitiri vichwa vyao katika enzi za Jahiliyya walifunga shungi zao juu ya shingo zao au walizining’iniza migongoni. Katika kukataza tabia hiyo kabla ya Uislamu kwa hakika kwa aya ya 30 na ya 31 za surah an-Nur katika Qur’an, Allah amewaamrisha wanawake wasioneshe haiba yao – isipokuwa yaliyodhihiri yenyewe– na kushusha shungi zao vifuani ilikusitiri nywele zao, kichwa, masikio na shingo.

Aisha (Allah awe radhi naye) anasema: “Allah awabariki wanawake wa mwanzo kuhama. Allah alipoteremsha aya “Na (waumini wanawake)  waangushe shungi zao juu ya vifua vyao,” walipasua kipande cha nguo kutokana na sketi zao na kwa nguo hiyo, walisitiri vichwa vyao.” (Bukhari, Tafsir-u Surati’n-Nur, 31, Abu Dawud, Mavazi)

Wanawake waliohama na wanawake wa Medina walichana kipande cha nguo na kwa hiyo nguo, walisitiri vichwa vyao pindi aya hiyo iliposhuka, na Mtume wetu amesema “mwanamke aliyebaleghe haruhusiwi kuonesha mwili wake isipokuwa mikono yake na uso.”(Abu Dawud, Mavazi, 32) Asma, dada yake Aisha; wote wanaonesha kuwa wanawake wanawajibika kusitiri viungo vya viwiliwili vyao.

Kwa kuongezea, ukweli kuwa Mtume aliashiria kwenye inchi mbili juu ya kifundo cha mkono, na kusema Mwanamke anayemwamini Allah na ahera haruhusiwi kuacha wazi mwili wake isipokuwa uso na mikono mpaka hapa pindi anapobaleghe” (Abu Dawud, Mavazi, 33) hilo linathibitisha kuwa amri zinazohusiana na aya ni za kufuatwa.

Hapa katika nukta hii, tutaeleza ibara ya maneno ya Mtume “Kasiyatun ariyatun” (“wamevaa lakini wako uchi”) kwa sentensi moja au mbili. Lengo la mwanamke kusitiri mwili wake ni kuficha haiba yake na si kuwaachia watu washawishike. Kwa kutafakari kauli ya Mtume, tunafahamu kuwa mavazi sharti yasiwe angavu na sharti pia yasioneshe ramani ya mwili. 

Ni nini lengo la Stara?

Lengo la stara inayoamrishwa na dini yetu ni kwamba wanawake sharti wasioneshe haiba yao na viwiliwili vyao kwa wanaume wasio-mahram na sharti wasiache uwezekano kwa wanaume wasio-mahram kuona maungo ya viwiliwili vyao yanayotakiwa kusitiriwa. Kwa sababu hiyo, ni sharti stara iwe nzito kiasi cha kutoonesha nywele, rangi ya ngozi na haiba yao; na sharti iwe ya kupwaya kiasi cha kutoonesha umbo. Kuhusu jambo hili, kuna hadithi nyingi nyingine mbali na hadithi zilizotajwa hapo juu. (Muslim, Mavazi, 34; Jannah, 13; Musnad 2:356)

Katika aya ya 59 ya surah al-Ahzab katika Qur’an, yanaelezwa yafuatayo: “Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe..”

Katika aya hiyo, wanawake Waislamu wameamrishwa wajishushie sehemu ya nguo zao za juu zisizodhihirisha umbo la mwili na wasitoke majumbani mwao wakiwa wamevaa nguo zinazovaliwa ndani ya nyumba. Katika aya ya 60 ya surah an-Nur, imeelezwa kuwa wanawake wazee wanaweza kutoka majumbani mwao bila ya kuchukua nguo zao za juu (koti n.k.) kwa sharti la kusitiri viungo vyao ambavyo ni muhimu kusitiriwa kama ilivyoamrishwa katika aya ya 31 ya surah hiyo hiyo:

“Na wanawake wazee wasio taraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao, bila ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijiheshimu ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.” (Qur’an, an-Nur, 24:60)

Katika kuhitimisha, ni amri kamili ya dini yetu kwa muwafaka wa maulama wa Kiislamu wa Kitabu na sunnah kuwa wanawake sharti wasitiri viwiliwili vyao isipokuwa uso na mikono karibu na wanaume wasio -mahram, kwa nguo isiyoonesha rangi ya ngozi na umbo la mwili na washushe shungi zao vifuani mwao ili nywele zao, vichwa na shingo zisionekane. Kutii amri hizo ni wajibu wa Waislamu kidini.

”Vazi bora ni vazi la uchamungu”

Allah anaamrisha katika aya ya Qur’an: “Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za uchamungu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu mpate kukumbuka.” (Qur’an, al-A’raf, 7:26)

Ni akili ya uchamungu na staha ambayo ndio muhimu kuliko nguo. Kusitiri maungo muhimu ni sharti la kwanza la kuhifadhi heshima. Hekima ya Allah imetoa stara endelevu, nzuri na ya kimaumbile kwa viumbe wengi isipokuwa kwa binadamu kwa kuwaacha pasi na akili ya kuwa na haya na kujisitiri.

Amemuumba tu mwanadamu, ambaye alimpa hisia za haya, katika hali ya uchi. Kwa hivyo, mtu anaweza kunufaika kutokana na mtihani wa stara na pia kuthibitisha kazi yake ya kuwa halifa wa Allah duniani. Mtu ana uwezo wa kutengeneza mavazi kutokana na wanyama na mimea na vitu vingine vilivyoenea juu ya ardhi na kwa kufanya hivyo, anaonesha uwezo wake wa kunufaika kutokana na kuvitawala viumbe vyote, ambavyo ni udhihirisho wa kuwa halifa wa Allah. 

Stara ni tabia za mwanadamu tu miongoni mwa viumbe hai wote. Kukaa uchi mara zote kunachukulika kuwa ni ukosefu wa mafundisho na ufidhuli wa dhamiri na akili katika kila zama za mwanadamu.

 Amri ya stara katika dini yetu inalenga katika kuhifadhi afya ya mtu ya kisaikolojia, heshima yake kwa sababu ya kuumbwa kwake na maadili ya umma na kudumisha urari miongoni mwa wanadamu na baina ya jinsia; na pia, kuanzisha njia ya kiheshima ya maisha ya kijinsia na familia. Ukweli kuwa mipaka ya stara inategemea amri mbalimbali kwa mwanamume na mwanamke ni utofautishaji uliofanyika kwa sababu ya tofauti zilizopo baina ya jinsia hizo mbili.

Je mwanamke asiyevaa ushungi si mnyoofu? Bila ya shaka haiwezekani kumchukulia mwanamke asiyevaa ushungi kuwa si mnyoofu. Juu ya hayo, kumwona kila mwanamke anayevaa ushungi kuwa ni mnyoofu kunaweza kuwa si sahihi. Kwa kuwa kuna wanawake wanyoofu na wenye heshima miongoni mwa wanawake wenye kusitiri vichwa vyao na wasiositiri, kunaweza kuwepo baadhi wasio na heshima na unyoofu.

Hata hivyo tukikiliangalia jambo hilo juu ya maadili na amri za Kiislamu, amri hii inabadilika kidogo. Uislamu unawajulisha watu kuwa baadhi ya viungo vya mwili wa mwanaume na mwanamke ni vya siri na visidhihirishwe kwa wasio -mahram na unaashiria kuwa watu wanaweza pia kuzini kwa mikono yao na macho yao. (Bukhari, Istizan, 12; Muslim, Majaliwa, 20) 

Kwa kuwa mara kwa mara watakuwepo watu katika jamii wanaoweza kuangalia sehemu za siri za wanaume na wanawake, Muislamu, anayetoka nje huku anayajua hayo na kudhihirisha sehemu hizo hiyo ni tabia inayoharibu dhana ya heshima na unyoofu wa Kiislamu. Mbali na hayo, kwa kuwa ushungi ni nguo inayositiri kichwa na kifua ambavyo husitiriwa na mwanamke, jambo hilo linatakiwa lifahamike hivyo. (Hayrettin Karaman)

Kwanini tusitiri miili yetu katika zama hizi?”

Natarajia kuwa mmelisikia swali hilo katika sehemu mbalimbali. Nilikuwa katika basi la umma. Wazee wawili walikuwa wameketi mbele yangu. Walikuwa wakizungumza. Wakati huo huo wasichana wawili waliokuwa wamesitiri vichwa vyao waliingia kwenye basi. Walikuwa wamesimama mbele ya basi kwa kuwa hakukuwa na viti vilivyosalia. Ajuza aliyekuwa ameketi mbele yangu, huku akimdukua mwanamke aliyekuwa karibu yake kwa mkono, aliuliza: “Unawaona?”. Mwanamke huyo akamjibu: “Ndiyo, ninawaona na ninawasikitikia. Ninawaonea huruma vijana hawa. Sisi pia tulikuwa tukisirtiri vichwa vyetu hapo zamani lakini sasa, tuko katika zama za kisasa. Unadhani vazi la namna hiyo linaweza kuendelea kuwepo? Hatuwezi hata kupiga hatua moja mbele kwa tabia hizo zilizopitwa na wakati.”

Kwa bahati mbaya, bado kuna watu wenye fikra kama hizo. Kwanza hebu tueleze kuwa stara si jambo linaloweza kushughulikiwa kwa mujibu wa zama. Watu wanaweza kuvaa nguo mbalimbali na za kigeni na bado akili zao zikaendelea kufanya kazi. Mathalani, huko Ujerumani, kila mmoja, wanaume na wanawake, walikuwa wakivaa kalpak (aina ya kofia ndefu) katika nyakati zilizopta. Wajerumani waliokuwa wakivaa kalpak hawakupungukiwa na akili; walipata maendeleo katika viwanda na teknolojia. Watu wa Ulaya walikuwa wakisitiri vichwa vyao mpaka hivi karibuni. Kusitiri vichwa vyao hakukuzuia maendeleo yao. Jambo hilo halihusiani na zama tunazoishi.

Haiwezekani kulihusisha jambo hili na ustaarabu. Maneno “Watu wastaarabu huzurura bila ya kujisitiri” hayana maana kabisa. Kama maana ya ustaarabu ni kuwa mbali na zama zilizopita na mitindo yao ya kimaisha, zama za ushenzi ziliachwa baada ya kuja Uislamu. Uislamu uliletwa na uliwaamrisha watu wasitiri miili yao. Kusitiri kulifanywa kuvutie, kuwe kamilifu na kukomaa na kuliushinda mtindo wa mavazi walioupenda wanawake.

Kutokana na sababu hizo, ikiwa maana ya ustaarabu ni kuishi kinyume na zamani, kukaa uchi kuliopo leo kulikuwepo kabla ya Uislamu, katika zama za Jahiliyya. Ikiwa kukaa uchi na kutokujisitiri ni ustaarabu, watu wanaokula watu na wenye ukabila msituni wanaishi bila hata kusitiri vifua vyao.

Watu wanaopinga vikali namna mwanamke anavyovaa wanatetea nini? Kwa nini wanaendelea kutilia mkazo jambo hilo? Haiwezekani kulielewa. Tunadhania kuwa wenye dhana hizo wanagugumia katika ulokole wanaoutetea juu ya mengine. Maana ya ulokole ni kuunga mkono dhana zisizo na ushahidi na msingi. Ushahidi wa muumini juu ya anayofuata ni wenye nguvu sana.

(Angalia. Gençliğin Cinsellik İmtihanı, M. Ali Seyhan, NESİL YAYINLARI)

3 Ni zipi sababu (hekima) za tasattur (kujitanda ushungi, kujisitiri)? Kwanini tasattur ni lazima?

Kanuni kuwa jina hubadilisha kitu kulingana na maana yake hudhihirika katika ukweli kuwa tasattur humbadilisha mwanamke inayembadilisha na kuwa kito cha thamani. Thamani ya kito hicho huzidi kadiri mwanamke anavyojihifadhi na kujificha.

Muunganiko uliowekwa na vitu hufanya vitu viwe na thamani au kukosa thamani kutegemeana na mahali vinakotumika. Jina tunalovipa vitu kuhusu sifa za vitu hivyo. Kila sifa ambayo kitu kinaipata huamua nafasi yake.

As-Sattar, ambalo ni mojawapo kati ya majina mazuri ya Allah Mtukufu, kilugha linamaanisha mwenye kuficha, anayesitiri na kuficha makosa na madhambi. Neno tasattur maana yake kujisitiri

Tasattur, ambalo limezingatiwa kama ni ishara ya kuheshimika mpaka sasa, halimaanishi hivyo kwa watu walioondokana na hali yao ya kimaumbile.

Kwa mujibu wa tunayoweza kuyaona pindi tunapochunguza historia ya jumuia mbalimbali ni ukweli kuwa kilicho cha kawaida, kilichoenea na muhimu ni tasattur. Katika mataifa mengine, tasattur huzingatiwa kuwa ni kiashirio kinachoamua kiwango cha heshima. Kwa upande mwingine, kukaa uchi kulizingatiwa kama alama ya fedheha na dharau na imeshutumiwa na takribani kila taifa katika historia yote.

Quran inatuambia “Hivyo (tasattur ) ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe." (al-Ahzab, 59)

Mola wetu Mlezi, aliyetuumba wanadamu na kufafanua neno mwanadamu, aliyetufahamisha maumbile yetu, aliyetuumba Waislamu na akafafanua neno Muislamu, aliyetufundisha maana ya Uislamu, aliyetuumba tukiwa utupu, aliyetutilia unyoofu na heshima, aliyetusitiri makosa yetu, anawataka wanawake waumini wajulikane na akafafanua kuwa wamesitirika.

Ili mtu ajulikane kuwa yuko katika tasattur haimaanishi kujulikana mbele za watu tu bali pia mbele ya viumbe wote; kutokuudhiwa hakumaanishi kuonewa na watu tu bali kutendewa vyema na viumbe wote.

Kuwa katika  tasattur kunalingana na mtu kujizingatia kuwa yupo katika ummah wa Muhammad (s.a.w).

Sababu nyingine ya tasattur ni kuwa mwanamke hujitazama kuwa amehifadhika na anawawezesha wengine kumbainisha kuwa ni mtu aliyehifadhika.

Nia hiyo hubainisha tabia  na sifa ya tabia hiyo. Kinachohitajika kuhifadhiwa hakiwezi kuwa ni ngao wakati huo huo. Mwanamke anahitajika kukubali kuhifadhiwa kama kito cha thamani kwa kuwa ni mwenye unyoofu na heshima; kwa hivyo, anahitajika azingatie unyoofu wake na heshima yake kama kito chake cha thamani.

Hali hiyo, ya kuafikiana na maumbile yake, ikifanikishwa, watu watakaomhifadhi mwanamke na watakaokuwa ngao yake watakuwepo kwa ajili yake. Atakuwa amehifadhiwa kama mwanamke wa kabila la Bani Qaynuqa ambaye alitukana na akahifadhiwa.

Mwanamke husifika vyema kama atakuwa amesitirika. Sifa hiyo inawahakikishia watu wajue maana ya kuwa mwanamke, na hifadhi ya hisia ya haya na unyoofu katika maumbile ya mwanamke hubainishwa na sifa hiyo: mwanamke ni yule aliyesitirika.

4 Ni ipi amri juu ya ushungi katika Uislamu? Kuna hatari gani kwa wanawake ya kutoka bila ya kuvaa ushungi?

Kwenye nukta hii, kuna aya mbili katika the Quran Tukufu. Katika aya hizi, Allah Mtukufu anatangaza waziwazi:

Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao (wanapotoka nje ya nyumba zao na wanapokuwa mbele ya wanaume wasiokatazwa kuwaoa kwa sababu ya nasaba).” (1)

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao …” (2)

Katika aya hizo, haioneshwi waziwazi jinsi gani wanawake waumini wajitande mitandio, na mahali gani wanaweza kuonekana. Hata hivyo, hadithi hii inatafsiri aya hizo kama ifuatavyo: Mtume Muhammad (S.A.W) alimwambia shemeji yake, Asma: “Ewe Asma! Mwanamke haruhusiwi kuonesha sehemu za mwili wake kwa wageni isipokuwa mikono yake na uso baada ya kufikia umri wa baleghe.” (3)

Kuwa Mwanamke Muislamu katika umri wa baleghe anapaswa asitiri nywele zake kwa amri ya Allah (SWT) na Mtume’s (SAW). Yaani, ni wajibu kusitiri kichwa kwa namna ambayo uso utakuwa wazi na kusitiri shingo na kifua. Ama kuhusu mtu kutokujisitiri kwa mtandio, kunamaanisha kuacha wajibu na hilo limekatazwa. Anapata madhambi na kwamba anabebeshwa jukumu kwa kuwa hazingatii amri ya Allah (SWT) na Mtume (S.A.W). Mtu mwenye madhambi lazima atubu na kuomba msamaha kutoka kwa Allah (SWT) ili afutiwe dhambi yake.

Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? - na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua. Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao!” (4)

Kwa hivyo, ili toba ipokelewe au dhambi isamehewe, mtu anatakiwa asiendelee na dhambi hiyo pasi na udhuru wowote.

Hapa kuna hadithi juu ya nukta hiyo:

“Muumini anapotenda dhambi, hutokea doa jeusi moyoni mwake. Ikiwa ataiacha dhambi hiyo na akamwomba msamaha Allah (STW), moyo wake utasafika doa hilo jeusi. Ikiwa ataendelea na dhambi hiyo, doa jeusi litakuwa kubwa. Ni kwa hali hii ndipo “dhambi huufunika moyo, ambayo ipo katika Qur’an.” (5)

Kauli “Katika kila dhambi kuna nia inayopeleka kwenye ukafiri.” inaeleza ukweli ulio muhimu. Mtu anayedumu katika kutenda dhambi anaizoea dhambi hiyo kadiri wakati unavyosonga mbele na hawezi kuiacha. Tabia hiyo inamvutia kwenye hatari kubwa za kiroho. Anaanza kuamini kuwa dhambi hiyo haina adhabu huko Ahera na Jahanamu haitakuwepo hata kidogo. (6)

Ili mtu huyo asikutane na hatari kama hizo na asidanganywe na Shetani, anahitajika ajiondoe na kuiacha dhambi hiyo, hilo litaleta toba yake.

(1) (al-Ahzab, 33:59)
(2) (an-Nur, 24:31)
(3) (Abu Dawud, Libas, 33)
(4) (Aal-i Imran, 3:135-136)
(5) (Ibn Majah, Zuhd, 29)
(6) Miwako, Badiuzzaman Said Nursi)