1
Wakati inapotajwa ibada, vinvyokuja akilini ni amri kama vile swala na kufunga. Jee ibada inahusisha swala na funga tu?
Hapana. Ibada haihusishi maamrisho ya dini kama vile kuswali kila siku na kufunga tu. Kila kitu, kila jambo, neno, kitendo, fikra au nia kwa kutafuta radhi za Allah, vyote huzingatiwa kama ibada. Kufanya yote mawili, kutekeleza amri za Allah na kuacha makatazo Yake kwa usawa huzingatiwa kuwa ni ibada. Hivyo basi, inawezekana kuigawa ibada kwenye mafungu mawili:
1. Matendo sahihi,
2. Ucha Mungu (Taqwa).
Matendo sahihi maana yake ni kutekeleza maamrisho ya Allah kama vile kuswali daima, kufunga, n.k.
Ucha Mungu maana yake ni kuepuka mambo yote aliyoyakataza Allah kama vile ulevi, Kamari na zinaa.
2
Nini maana ya utumwa (kunyenyekea) kwenye Uislamu? Ni nini maana ya kumuabudu Allah?
Utumwa ni kitendo cha kutengeneza uhusiano baina ya mwanadamu na Muumba, Allah. Hivyo basi, ukweli kwamba Allah ndie Muumbaji na mwanadamu ameumbwa unasisitizwa kwenye aya za mwanzo kabisa kama zilivyoshushwa:
“Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba. Amemuumba binaadamu kwa tone la damu” (al-Alaq, 96/1-2).
Qur’an inavuta hisia za umakini kuhusu uhusiano huu mwanzo mwa aya inayomtaka mwanadamu kuabudu:
“Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka.” (al-Baqara, 2/21).
Inafahamika kuwa kutoka kwenye aya ya hapo juu kwamba kuabudu ni jukumu la kiuumbaji la asili ya mwanadamu, ni kupeleka shukrani kwa Muumba, na ni tendo tukufu linalopelekea kutambua lengo la kiroho na kimwili.
Sasa tutawasilisha ukweli wa kunyenyekea, ambao tumejaribu kuonesha katika baadhi ya mambo:
Kunyenyekea hufanywa kwa njia mbili: Ya kwanza ni unyenyekevu unaofanywa bila kuzingatia kuonekana kwa Muumbaji na kutokuzungumza na Yeye.; na wa pili ni unyenyekevu wa kumuelekea Yeye.
1. Unyenyekevu unaofanywa bila kuzingatia kuonekana kwa Muumbaji unaweza kufupishwa kama ifuatavyo:
a. Utumwa (Servitude): Kuthibitisha ukubwa wa Allah kusifia ufundi wake kwa kuangalia utendaji usiokifani wa Muumba unaoonekana ulimwengu mzima kama vile kutengeneza, kudhibiti, kupanga na kusanifu.
b. Utumwa (Servitude): Kuangalia uzuri wa usanifu unaoakisi majina mazuri ya Mungu, kuyazungumzia, na kila mmoja kumuonesha mwenzake ili kupata mazingatio kupitia majina hayo.
c. Utumwa (Servitude): Kutathmini lengo la uzuri wa majina ya Allah, ambayo yana faida za kiroho, pamoja na kiakili na kuyasifu toka moyoni.
d. Utumwa (Servitude): Kupokea, kufikiri na kutafakari kurasa za ulimwengu kama kitabu kilichoandikwa na kalamu ya nguvu na hekima ya Allah.
e. Utumwa (Servitude): Kuangalia Sanaa ya hali ya juu, darizi nzuri na maumbo yaliyopambwa yanayoonekana pembe zote za dunia, kuangalia uzuri wa kiroho na ukamilifu wa Muumbaji na kumjua kwa ukaribu mno, ili kumpenda na kumuheshimu.
2. Unyenyekevu mbele ya Allah na kuzungumza nae unaweza kufupishwa kama ifuatavyo: The servitude in the presence of the Creator addressing Him can be summarized as follows:
a. Utumwa (Servitude): Kujua kwamba mwanadamu siku zote yupo mbele ya Allah na kutenda ipasavyo. Kumfikia mtendaji kupitia matendo na kumfikia msanii kupitia Sanaa.
b. Utumwa (Servitude): Kufahamu kwamba Muumbaji anataka ajulikane kwa kuonesha Usanii wa hali ya juu na wa kimaajabu; na kujibu jambo hili kupitia Imani.
c. Utumwa (Servitude): Kufahamu kwamba Allah, ni mwingi wa huruma, anataka kupendwa kwani huonesha matunda ya huruma yake kama akisi/picha ya huruma yake isiyo na ukomo kwa kukamilisha hitaji hili la Allah; mwanadamu kuuweka upendo wake kwa Allah na kujaribu kujipendekeza ili apandwe na Yeye kupitia kumuabudu Allah.
d. Utumwa (Servitude): Kufahamu kwamba Allah, ambae ni Mkarimu, huwapa watu neema zisizo na ukomo za kimwili na za kiroho pamoja na kuvielekeza viungo vya hisia vya kimwili na vya kiroho vya watu, anataka avipe raha viwiliwili na akili; na hivyo basi, kupeleka sifa na shukran zake kwa Allah kupitia vitendo, maneno na fikra kwa kadri awezavyo.
e. Utumwa (Servitude): Kusema “Subhanallah, Alhamdulillah, Allahuakbar” (Ametukuka Allah, Shukran zote zinamstahikia Allah, Allah ni mkubwa) kwa ajili ya kumtukuza Allah juu ya utukufu wake (majesty) na uzuri wake (beauty), ambapo mfano wake unaonekana kila mahala kuanzia chembe ndogo ndogo (atoms) hadi maumbo makubwa (galaxies); kusimama, kurukuu na kusujudu mbele ya uwepo wake.
Kwa kuongezea, utumwa umegawika katika makundi mawili makubwa ambayo ni kuabudu na kuhudumia: funga, kuswali, kutekeleza nguzo ya Hijja, zaka ambapo zote hizi ni mifumo ya ibada; kuzalisha utaalamu wa aina zote wa kiteknolojia ambao unarahisisha maisha nayo pia huzingatiwa kama ibada. Kwa mfano, kutengeneza gari, kuunda meli, kutengeneza barabara na madaraja, kuanzisha viwanda ambavyo vitatoa bidhaa kadhaa za kiteknolojia vile vile nayo huzingatiwa kama ibada. Ni umuhimu usio na shaka kuazimia kupata radhi za Allah na kuwa mkweli hasa ikiwa mtu anataka ibada zake zikubaliwe.
3
Ni nini maana ya Ibada? Kwanini tunaabudu?
Ibada maana yake ni kutekeleza maamrisho ya Allah, kujitenga na makatazo Yake, na kutenda kutokana na ridhaa Yake. Ama kuhusu kwanini tunaabudu:
* Awali ya yote, tunaabudu kwasababu ndio lengo la kuumbwa kwetu kwasababu Allah alituumba, sisi wanadamu, ili tumjue, tumuamini na kumuabudu Yeye.
Jambo hili linaelezwa kama ifuatavyo katika Qur’an:
“Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.” (adh-Dhariyat, 56)
Kama waumini, tunatenda kwa mujibu wa lengo la kuumbwa kwetu lililotajwa katika aya na kujaribu kukalimisha wajibu wetu wa kumuabudu Muumba wetu.
* Vile vile, tunamuambudu Allah kama sehemu ya kupeleka shukurani zetu Kwake kwa neema nyingi anazotupa.
Tunamshukuru mtu ambae hutupa zawadi ndogo kabisa mara kadhaa; ikiwa hatutomshukuru Allah ambae anatupa neema nyingi na zawadi nyingi, kupitia kumuabudu, tutakuwa ni watovu wa shukurani. Tunajaribu kukamilisha majukumu yetu ya kuabudu kwa usahihi kabisa kuepuka utovu wa shukurani.
Allah ametuumba kutokana na si kitu, akatupa hisia na viungo kwa maelfu, akaumba kila kitu ambacho hisia na viungo hivyo vinahitajia na ametupa ubinadamu, Imani na muongozo wa maisha.
Inaelezwa katika Qur’an kwamba neema za Allah hazina mwisho na haiwezekani katu kuzihesabu kama ifuatavyo:
“Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu, hamwezi kuzimaliza. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu.” (an-Nahl, 18)
Ambacho tunatakiwa kufanya kutokana na neema ambazo hazina ukomo ni kumjua na kumpenda Allah Mtukufu, ambae ndie mmiliki wa neema hizo, kuonesha kwamba tunampenda kupitia kuabudu na kumuonesha shukurani na heshima zetu Kwake kama mrejesho wa neema anazotupa.
Kwakweli, ibada na shukrani zetu hazitoshi kwa neema anazotupa Allah katika ulimwengu huu. Kwa kweli, Allah ametuandalia neema kubwa Peponi ikiwa tutamuamini na kumuamini na ametuahidi neema zisizokwisha Peponi. Kwa hali hiyo, neema ambazo Allah ametuahidi kutupa siku ya Qiama ni upendeleo wake maalumu, huruma na malipo. Si kwamba tunapewa kama malipo halisi kupitia ibada na shukurani zetu.
Mtume (rehma na Amani ziwe juu yake) amelielezea jambo hili kama ifuatavyo:
“Matendo yenu hayawezi kuwapeleka peponi. Vile vile matendo yangu hayawezi kunipeleka peponi.Hili linawezekana tu kupitia huruma za Allah.”
4
Ni vipi vigezo vya ibada kukubaliwa na Allah?
Kuna sharti moja tu la ibada kukubaliwa na Allah. Ambalo ni Ikhlasi.
Uaminifu ni kama roho ya ibada inayofanywa. Ibada bila uaminifu/udhati ni sawa na kwamba haina roho. Haina thamani mbele ya Allah.
Uaminifu/Udhati kwenye ibada maana yake ni kuabudu kwasababu tu ni agizo kutoka kwa Allah na ndio njia ya kupata radhi za Allah. Mwanachuoni Badiuzzaman Said Nursi amelielezea jambo hili kama ifuatavyo:
Ibada na kumtumikia Allah hulenga (utekelezaji) wa agizo la kiungu, na radhi ya kiungu. Lengo la ibada ni kutekeleza agizo la kiungu, na tija yake ni radhi ya kiungu. Matunda na faida zake hulenga maisha ya akhera.
Ikiwa uaminifu utatumika kwa matakwa na faida ya kidunia, uaminifu utatoweka na hivyo ibada haitokuwa sahihi; maana yake ni kwamba, haitokubaliwa na Allah.
Katika hadithi, Mtume (rehma na Amani ziwe juu yake) ameelezea nafasi ya uaminifu katika matendo na ibada kama ifuatavyo:
“Bila shaka yoyote, Allah huyakubali baadhi ya matendo na ibada ambazo hufanywa kwa uaminifu kwa ajili yake na kutafuta radhi zake.”
5
Ni nini faida za ibada kwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii?
1. Moja kati ya faida za ibada ni kwamba, ibada huweka hukumu zinazohusiana na itikadi na imani kutulia katika moyo na nafsi na kutengamaa.
Kama inavyojulikana, elimu huongezeka, hukua na kumakinika kutokana na matendo na uzoefu. Ni vigumu kuihifadhi elimu ambayo haifanyiwi kazi na kutumiwa; haitokuwa na maana yoyote kwa mwanadamu. Jambo hilo ni sahihi pia kwa elimu na hukumu za Imani na itikadi. Hutulia katika moyo wa mwanadamu tu kupitia ibada, kwa sababu ibada, ambayo maana yake ni kutekeleza maamrisho ya Allah na kuacha makatazo yake, ni kama kutenda na kuifanyia kazi Imani.
Kuacha ibada husababisha taathira chanya ya Imani katika tabia ya mwanadamu kudhoofika na kufutika kabisa kwa kadri muda unavyoenda. Kwa kadri ambavyo taathira chanya ya tabia ya mwanadamu hudhoofika tabia mbaya na matamanio yenye madhara hutawala katika ulimwengu wake wa hisia na kumsukuma mwanadamu kutenda madhambi mbalimbali na matendo maovu. Kwa mantiki hiyo, Imani na ibada vina uhusiano wa karibu sana. Kama tutaifananisha Imani na taa, basi ibada ni kama glasi ya taa hiyo ambayo huizuia kuharibiwa na upepo na hivyo kuongeza mwanga wake. Katika kuonesha kazi ya ibada kuilinda Imani, Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) amesema, “Imani ni mwili ulio uchi; nguo yake ni ucha Mungu.” Kama inavyojulikana, ucha Mungu ni kuacha makatazo ya Allah na kujitenga mbali sana na mambo yote ya haramu na dhambi; tuliyoyaorodhesha juu ndio maana ya ibada.
2. Ibada hufanya kazi muhimu ya kupangilia mfumo wa maisha wa mtu kwasababu ibada hugeuza fikra zote kwa Allah Mtukufu na kuuweka utukufu na ukubwa wa Allah katika akili za watu. Jambo hili humfanya mtu kufukiria kupata radhi za Allah katika kila jambo analofanya na kutii maagizo ya Kiungu na kuacha makatazo yote.
Hivyo, maisha ya mtu binafsi yanapangiliwa kwa kufuata maelekezo ya dini na huwekwa katika nidhamu maalumu kivitu na kiroho.
3. Ibada hufanya kazi muhimu sana ya kuunganisha watu na kuhakikisha Amani na upendo katika jamii vile vile. Kuabudu kwa kuelekea Qibla kimoja huanzisha uaminifu usiovunjika na uhusiano usio na ukomo baina ya Waislamu. Uaminifu na uhusiano huu huleta umoja imara, mapenzi ya dhati na urafiki wa kweli.
Hivyo, maisha kwenye jamii yanakuwa ya Amani na upendo; maendeleo ya vitu na kiroho hudumishwa.
4. Kwa ajili ya kuleta athari za ibada kwenye ulimwengu wa kitabia na kiroho wa mwanadamu:
Muumini anaetekeleza ibada zake hupata Amani na utulivu. Huwa madhubuti kiroho. Huishi kwenye amani na furaha kwenye maisha yake yote pamoja na utulivu wa kisaikolojia wa mtu anaetekeleza majukumu yake.
Hatohisi kuchanganyikiwa, kuchoshwa au kukata tamaa. Hatohisi huzuni na kukosa matumaini wakati anapokabiliwa na changamoto, mazito na yasiyowezekana; hatopoteza msimamo na kujiamini kwake. Ulimwengu wa ndani wa mtu anaetekeleza ibada huwa na utulivu uliotengamaa. Kimbunga cha kisaikolojia, mikanganyiko na migogoro haitochukua nafasi katika maisha yake.
5. Ibada ndio njia kubwa kufikia ukamilifu wa mtu na kufikia ukomavu.
Kama inavyojulikana, mwanadamu ni kiumbe kidogo na dhaifu kwa kiwiliwili chake. Ingawa, anamiliki nafsi madhubuti na vipawa vikubwa vya akili. Fikra zake na matakwa yake hayana ukomo; fikra zake hazikuwekewa mipaka wakati alipoumbwa.
Kitu kinachonyanyua na kukuza nafsi ya mwanadamu, ambae atakuwa na asili hiyo, ni ibada.
Kitu kinachokuza uwezo wake na akili zake ni ibada.
Kitu kinachonyanyua hisia na matamanio ni ibada.
Kitu kinachomtambulisha malengo yake na kuyafanya upya matumaini yake ni ibada.
Kitu kinachohakikisha mawazo sahihi na hoja za msingi kwa kuziwekea kanuni za nidhamu fikra zake ni ibada.
Kitu kinachodhibiti hisia na mihemko, ambacho kinamlinda mtu asivuke mipaka na kuvuka kiwango katika utendaji wa mambo ni ibada.
Kwa ujumla, ibada ni kitu kinachomfanya mwanadamu kupata ukamilifu, Ukomavu wa kitabia na kiroho.