Fungu la mwanamke katika Mirathi na Usawa
A. Hali ya kabla ya Uislamu
Sababu mojawapo ya watu kudai kuwa Uislamu unawaona wanaume ni bora kuliko wanawake na kuwa unakiuka usawa wa wanaume na wanawake ni ukweli kuwa mwanamke hupewa fungu moja lakini mwanamume hupewa mafungu mawili katika mirathi. Kwa hakika, kuwapa fungu moja kwa wanawake na mawili kwa wanaume hakuhusiani na jambo la wanaume kuwa bora kuliko wanawake. Kinyume chake, kwa kuwapa wanawake fungu kutoka katika mirathi, Uislamu umelinda haki za watoto wadogo na wanawake waliokuwa wakidhulumiwa na kuonewa na watu wa Jahiliyyah. Kiukweli, yafuatayo yameelezwa katika aya:
“Wanaume wana sehemu katika wanayo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Na wanawake wanayo sehemu katika waliyo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Ikiwa kidogo au kingi.” (an-Nisa, 4/7)1
Katika jamii ya Waarabu wa Jahiliyyah, wanawake hawakuwa wakipewa fungu lolote katika mirathi. Zaidi ya hivyo, wanawake walirithiwa kama mali pindi waume wao walipofariki. Ni wale wanaume waliotumia silaha tu na kulinda nchi ndio waliokuwa na haki ya kurithi. Mali ya mwanamume aliyekufa iligawanywa miongoni mwa ndugu zake wa kiume walioweza kupigana. 2 Hata hivyo, mjini Madinah, watoto waliobaleghe waliweza kurithi mali za baba zao; watoto wadogo, mabinti na akina mama hawakurithi chochote kutoka kwa baba zao. 3
“Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili.” 4
Kwa hiyo, ilipoteremshwa aya hiyo, washirikina hawakuipenda amri hiyo na wakasema,
“Mwanamke anapewa moja ya nne au moja ya nane; binti anapewa nusu ya fungu; watoto wadogo nao wanapewa mafungu. Lakini, hawawezi kuendesha farasi wala kupigana. Watoto wadogo pia wanapewa mirathi lakini watoto wadogo hawasaidii chochote katika vita.” 5
Kinachofahamika kutokana na mtizamo huo ni kwamba thamani ya mtu ilipimwa kwa mchango wake katika uchumi.
Fikra hizo ni za Waarabu wa Jahiliyyah, ambazo bado zimo nyoyoni mwa baadhi ya watu, dhidi ya utaratibu wa ugawaji alioufaradhisha Allah kwa msingi wa haki na sababu nyingi zenye hekima. Fikra za Jahiliyyah zilizomo akilini mwa baadhi ya watu wanaoishi leo haitofautiani sana na fikra za Waarabu wa Jahiliyyah. Sababu za kushuka aya hiyo zinadhihirisha waziwazi hali ya wanawake na watoto katika enzi za Jahiliyyah. Mke wa Sa’d b. Rabi, aliyekufa shahidi katika Vita vya Uhud, alikwenda mbele ya Mjumbe wa Allah pamoja na mabinti zake wawili. Akasema,
“Ewe Mjumbe wa Allah! Hawa ni mabinti wa Sa’d. Baba yao alikufa shahidi katika Uhud. Ami zao wamerithi mali yake na hawakuwaachia chochote mabinti hawa. Hata hivyo, mabinti hawa hawawezi kuolewa bila ya mali yoyote.”
Mjumbe wa Allah (s.a.w) alisikiliza malalamiko ya mwanamke huyo na akasema, “Allah ataleta amri Yake kuhusu jambo hili.” 6 Papo hapo, aya ya mirathi iliteremshwa. 7
Uislamu umewanusuru wanawake na watoto wasinyimwe mirathi; umewapa utu wa kijamii na wa kisheria pamoja na wanaume. Kwa hiyo, wale wanaodai kutetea haki za wanawake wasiukosoe Uislamu kwa kusema, “Uislamu unawapa wanawake nusu ya fungu”; badala yake wapokee na kukiri usawa na ubora wa Uislamu, unaowapa wanawake haki ya mirathi kwa njia ya mapinduzi makubwa. Kwa amri hii, Quran haikuondoa tofauti na dhuluma tu miongoni mwa watoto wadogo na wakubwa bali pia imeweka haki za mirathi kwa mama, binti, dada, bibi, mjukuu wa kike, n.k. kwa kuwataja mmoja mmoja kwa majina. Mafungu hayo, yaliyopangwa na Quran kuwa ni haki zisizobadilika, haziwezi kuondolewa na mpango wowote wa kisheria au kidesturi kama vile wosia. Hayo yamejumuishwa katika kundi la (nasiban mafrudan) “fungu lililopangwa” (an-Nisa, 4/7). Ibara hiyo ni ishara ya wazi kabisa kuwa amri hiyo iko dhahiri na yenye kufahamika na kuwa haiwezi kubadilishwa.
B. Aya Zinazohusu Mirathi ya Wanawake
Ni dhahiri kuwa mwanamke ana haki ya kurithi kama alivyo mwanamume katika Uislamu. Vipingamizi juu ya amri hiyo vinahusiana na ukweli kuwa mwanamke hupewa nusu ya fungu la mwanamume.
Awali ya yote, hebu tueleze kwamba umajumui kuwa Uislamu umeamuru mwanamke apewe nusu ya fungu katika mirathi unatokana na kutokuitathimini aya zinazohusu jambo hilo kwa makusudi. Aya hizo zinapotathiminiwa bila ya chuki zozote na kwa uangalifu, madai ayo yataonekana kuwa si kweli:
1. Kumpa mwanamke nusu ya fungu katika mirathi hakudumu katika hali zote; hutokea pale tu anaporithi pamoja na kaka yake (zake) wa baba mmoja na mama mmoja:
“Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu.” (an-Nisa, 4/11) 8
Kwa hiyo, ni dhahiri kuwa kanuni ya kumpa mwanamke nusu ya anachopata mwanamume katika mirathi si kanuni inayojumuisha hali zote. Kwa hivyo, kudai kuwa mwanamke hupewa nusu ya anachopata mwanamume katika mirathi ni kanuni ya ujumla tu pasi na kujali hali ya mwanamke na yanakusudia kukwepa maana ya aya iliyotajwa hapo juu.
2. Kama inavyodhihirika katika aya hiyo, fungu la mwanamke katika mirathi si nusu ya lile la mwanamume kama madai hayo yalivyodai. Ikiwa aliyefariki ameacha mabinti (angalau wawili) tu, theluthi mbili watapewa wao. Ikiwa aliyekufa amemwacha binti mmoja tu, atapata nusu ya mali yote. (an-Nisa, 4/11)
3. Ikiwa mtoto atafariki na kuacha mirathi na ana watoto, basi mama na baba kila mmoja atapewa moja ya sita ya mali. Ikiwa aliyefariki hakuacha watoto na wazazi ndio warithi, basi mwanamke atapata theluthi ya mali yote. Ikiwa aliyefariki ameacha ma-kaka, mama atapata moja ya sita ya mali yote. (an-Nisa, 4/11) 9
4. Mume akifariki, mkewe atapewa robo ya mali. Mtu akifariki na kuacha watoto zaidi ya mmoja kwa mkewe mmoja au mke mwingine, au ikiwa mwanaye wa kiume ana watoto, mkewe atapata moja ya nane ya mirathi.
“…Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni...” (an-Nisa, 4/12) 10
Kama inavyoonekana, madai kuwa fungu la mwanamke kila mara ni nusu ya lile la mwanamume si kweli. Fungu hubadilika kutegemeana na warithi waliopo.
C. Kwanini Mafungu mawili kwa mwanamume na Fungu moja kwa mwanamke?
Kwa mujibu wa Quran, inaweza kuonekana dhuluma kwamba mwanamke anapata nusu ya fungu anaporithi pamoja na kaka yake pindi jambo hilo linapotazamwa kijuujuu lakini kwa hakika ni haki. Licha ya kuwa ni haki, itaonekana kuwa ni sahihi litakapotazamwa chini ya nuru ya uadilifu na haki.
1. Katika Uislamu, mirathi imegawanywa kwa kuzingatia mahitaji na wajibu wa watu. Matumizi ya mama, mke, binti na dada yanapaswa yatimizwe na baba, mume, mtoto wa kiume na kaka. Kwa ujumla, mwanamke hahitajiki kutoa matumizi kwa nduguze. 11 Mwanamume anatakiwa atoe matumizi kwa mkewe, binti, mama na dada katika hali zote. Mwanamume ni mlinzi rasmi wa familia yake na anawajibika kwa kila mwanafamilia. Kwa hiyo, kulingana na kanuni “Zawadi zinategemea majukumu”, mwanamume, ambaye ndiye anayewajibika kuwapa matumizi mkewe, mabinti, mama na inapolazimu kumpa dada yake, hupewa mara mbili ya fungu la dada yake, ambaye hana majukumu hayo.
2. Mwanamke ana mamlaka kamili ya kutumia mali yake apendavyo. Hata kama mwanamke ni tajiri, hahitajiki kutoa mali yoyote kwa ajili ya familia. 12 Kutokana na mtazamo huo, kama mwanamke na mwanamume wangepewa mafungu sawa, uwiano usingekuwa dhidi ya mwanamume kwa kuwa anahitajika kutoa matumizi kwa ajili ya familia; mwanamke hana wajibu huo. Badiuzzaman Said Nursi anaeleza yafuatayo kuhusu jambo hilo:
Aya “...Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili...” ni haki kabisa, pia ni huruma haswa. Ndiyo, ni haki, kutokana na wanaume wengi huelemewa kwa kumchukua mke na kumkimu. Ama kwa wanawake, wao hupata mume na kumtwisha mzigo wa maisha, na hilo hupunguza walichorithi.”13
3. Kama mwanamke hajaolewa, yeye ni mtu mmoja asiyewajibika kumtunza yeyote. Anapoolewa, mumewe anatakiwa amtolee matumizi yeye na wanawe kama ilivyoelezwa hapo juu. Mwanamke hana wajibu wa kuchuma mali. 14 Zaidi ya hayo, mwanamke anapata mahr kutoka kwa mumewe na atapata zawadi nyingi kama vile dhahabu, vyombo vya ndani, pesa n.k. kulingana na desturi. Mwanamke halazimiki kutumia mali aliyo nayo. 15 Akitaka, anaweza kuizidisha kwa kuwekeza. Kaka atatumia mirathi aliyopata kwa ajili ya gharama za ndoa, mahr na matumizi ya familia. Mbali na hayo, ikiwa dada ambaye hajaolewa hawezi kuishi kwa kutegemea mirathi aliyopokea, kaka anatakiwa amsaidie. 16 Kwa hiyo, jambo hili linapotazamwa kwa mtazamo huo, kumpa mwanamume fungu moja na mwanamke nusu ya fungu ni haki kabisa.
Ni muhimu kuzingatia kuwa Uislamu unapendekeza muundo ambao wanawake watajitegemea kijamii lakini huru kiuchumi. Hilo ni muhimu ikiwa tunataka kufahamu mkazo wa Uislamu juu ya kupendana wote wawili, kuheshimiana, kuvumiliana na kuelewana miongoni mwa wanafamilia. Hata hivyo, haijalishi uhuru wa uchumi ulivyo bora, haimaanishi kuwa wanawake wanatakiwa watoe matumizi yao wenyewe na kuwa wanaweza kuishi kwa kujitegemea nje ya familia. Wajibu wa kiuchumi wa familia kila mara unamtegemea mwanamume. Kwa hakika, haki hii, wanayopewa wanawake, inaonesha umuhimu ambao dini yetu inawapa wanawake.
4. Kaka anaweza kumpa dada yake fungu sawa au zaidi akitaka wakati wa kugawana mirathi. Hilo litatazamwa kuwa ni mchango au zawadi. Hakuna anayeweza kuzuia hilo.
5. Suala hilo pia lina sura ya kisaikolojia. Uislamu si wa wakati au enzi, nchi au taifa fulani tu. Unaenea vyote; unazingatia nyakati zote, jumuia zote na saikolojia zote za kibinadamu katika amri zake. Takribani katika jumuia zote, mabinti wamekuwa wakitazamwa kuwa ni “wasichana wenye kutoa mali ya nyumbani na kuwapelekea watu wengine”; hayo yapo hata leo. Kwa hakika, hata kama ataolewa, ana familia tofauti na ana watoto, bado atahitaji huruma na ulinzi wa wazazi wake na kaka zake. Huruma anayopata ina thamani kubwa kuliko mali anayopata kutoka katika familia yake. Katika hali hiyo, kumpa mtoto wa kiume na binti fungu lililofanana wakati wa kugawanya mirathi kunaweza kuiharibu huruma hiyo. Katika kulishughulikia hilo kwa mtazamo huo, Badiuzzaman Said Nursi anasema yafuatayo juu ya hayo:
“Pia ni rehema, kwani msichana mnyonge anahitaji sana ukarimu wa baba yake na kaka zake. Qur'an inaamuru kuwa apate ukarimu wa baba yake bila ya wasiwasi. Baba yake hamwangalii kwa wasiwasi kwa kumfikiria kuwa ni “mtoto mwenye madhara ambaye kwa sababu yake itaondoka mali yake na kwenda mikonomi mwa mgeni.” Wasiwasi na hasira havitangamani na ukarimu wake. Pia anapata ukarimu wa kaka yake na hifadhi bila ya ushindani na husuda. Hamfikirii “kama ni mshindani atakayeangamiza nusu ya familia na kuipa sehemu muhimu ya mali yetu kwa mtu mwingine.” Hawatakuwa na chuki na uhasama uliochanganyika na hisia zake za kumhurumia na kumhifadhi. Kwa hivyo, msichana, ambaye ni mlaini na mdhaifu kimaumbile, kijuu juu anaonekana amenyimwa sehemu ndogo, lakini badala yake anapata mali isiyokwisha kwa njia ya huruma ya wale walio karibu naye. Na kumpa zaidi ya anavyostahiki kwa dhana ya kumhurumia zaidi kuliko Rehema ya Kiungu, si ukarimu, bali ni makosa makubwa. Kwa hakika, ulafi wa kishenzi wa zama hizi, unaokumbusha udhalimu wa kuwazika watoto wachanga wa kike wakiwa hai katika zama za Ujinga kwa sababu ya husuda za kishenzi, huenda zikafungua njia za uovu wa kikatili. Ama kuhusu hilo, hukumu zote za Quran zinathibitisha hukumu hii, “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” (al-Anbiya, 21/107).” 17
Kwa tathmini hii, Badiuzzaman Said Nursi anashughulikia suala hilo kwa mtazamo wa kina.
Migogoro hutokea baina ya wengi kati ya ma-kaka na ma-dada kwa sababu wanaume na wanawake wanapokea mafungu sawa kutoka katika mirathi ya leo. Kaka hawezi kukubali pindi dada anapopata nusu ya mali ya baba yake na kuwapelekea watu wengine. Kwa sababu ya fikra hii ya Jahiliyyah, migogoro mingi ya mirathi hutokea baina ya makaka na madada katika nchi yetu. Leo, watu wengi huwashinikiza dada zao kuwataka wayaache mafungu yao kutoka katika mirathi au watosheke na kiasi kidogo. Madada kwa ujumla huachilia haki zao chini ya shinikizo. Wanawake hubembelezwa na kunyamazishwa katika mahakama haramu za kisheria za kifamilia. Kama tuonavyo katika vyombo vya habari, migogoro ya mirathi inaweza kubadilika na kuwa umwagaji damu usiokoma. Kutokutumia mpango wa ugawaji mirathi wa Allah na kutokutosheka na fungu lake mtu husababisha ukosefu mkubwa wa haki na dhuluma nyingi.
Kutokana na sababu tulizojaribu kuziorodhesha hapo juu, mwanamume hupewa fungu lake kutegemeana na kiwango cha majukumu yake ya kifedha; mwanamke, ambaye hana majukumu ya kifedha ama akiwa ni tajiri au masikini, daima huwepo chini ya dhamana ya kijamii hata akiwa hajaolewa, binti, mke, mama na mjane; yeye hupewa fungu kulingana na alivyo. 18 Ikiwa amri hii ya Allah, mwenye hekima zisizo na ukomo katika amri Zake, si ya haki, inamaaisha kuwa hakuna haki juu ya ardhi.
Kwa kuhitimisha, sheria ya mirathi, ambayo hushughulikiwa kama ni mwendelezo wa sheria ya familia katika Quran, ni jambo lililoelezwa kwa kina. Kuutazama usawa wa wanawake katika mirathi, ambao ni katika masuala ya kisasa zaidi hivi leo, kutokana na mtazamo wa usawa huunda tu msingi wa kosa lenyewe. Kwani, mafungu ya wanawake hutathminiwa tofauti katika hali tofauti tofauti. Hilo hushughulikiwa katika makundi tofauti kutegemeana na kama yeye ni mke, mama, dada pekee au mmojawapo kati ya dada wengi. Wenye kutetea usawa kamili katika kila jambo likiwemo hili husingizia kutoangalia kanuni za msingi zilizotajwa hapo juu. Kwa hiyo, mwanamke huyo hupewa nusu ya fungu la mwanamume katika baadhi ya hali katika mirathi halihusiani na dhana ya kuwa wanaume ni bora kuliko wanawake. Kama ingekuwa kama hivyo, tungepaswa tuseme kuwa watoto ni bora kuliko baba zao kwa kuwa wanapokea fungu kubwa kuliko baba zao. Yatakuwa ni madai ya kubezwa. Kinyume chake, utaratibu huu wa ugawaji unawiana moja kwa moja na majukumu ya mwanamke na mwanaume; unalenga kusambaza matumizi kwa urari na kuhakikisha yanakuwepo mapenzi na haki katika maisha ya kifamilia na ya kijamii.
Mbali na hayo, ukweli kuwa mambo ya lazima na wajibu wa mwanamke na mwanamume ni ya kimaamuzi hapa na kuwa watoto, wanaokaribia kuanza maisha na watakaokabiliana na shida za kifedha katika maisha kwa sababu ya kuhitaji mali zaidi kuliko wengine, wanapewa mafungu zaidi kuliko wazazi wao na kuwa wanaume hupewa kuzidishiwa kuliko wanawake kusudio ni kuhakikisha maisha ya kibinadamu katika familia, ambayo ni kitengo cha chini zaidi cha kijamii. Pia ni ishara ya hatua zilizochukuliwa ili kuunda tabaka la kati. 19
Marejeo
1. an-Nisa, 4/7.
2. angalia Tabari, Jamiu’l–Bayan 4/262, Misri, 1968; Razi, Tafsiru’l-Kabir 9/194, Beirut; Tahir b. Ashur, at–Tahrir wa’t-Tanwir 4/248, Tunus, nd; Ibn Kathir, Tafsirul-Qur’ani’l-Azim 2/161. Waarabu walikuwa wakisema, “Wale wasiopigana kwa mikuki, wasioweza kulinda nchi yao na wasioweza kupata ngawira hawawezi kurithi.” angalia rejea ya hapo juu; kuhusu desturi ya mirathi katika Enzi za Jahiliyyah, angalia Ali Osman Ateş, İslâm’a Göre Cahiliye ve Ehl-i Kitap Örf ve Adetleri uk. 379-388.
3. Hamidullah, Muhammad, İslâm Peygamberi 1/260, İrfan Yay. İst. 1980; Kwa ajili ya desturi ya mirathi katika Uyahudi, angalia Ali Osman Ateş, İslâm’a Göre Cahiliye ve Ehl-i Kitap Örf ve Adetleri uk. 372-380.
4. an-Nisa, 4/11.
5. Angalia Tabari, sawa na rejea ya hapo juu 4/275; Ibn Kathir, sawa na rejea ya hapo juu 2/197.
6. Abu Dawud, Faraid 4; Ibn Majah, Faraid 2.
7. Wahidi, Asbabu’n–Nuzul p.150; angalia Ibn Kathir, sawa na rejea ya hapo juu 2/196; Qurtubi, al-Jami’ li Ahkami’l-Qur’an 5/39; Razi, sawa na rejea ya hapo juu 9/203-204. Jambo lililompata Jabir b. Abdullah pia ni sababu miongoni mwa sababu za kushuka aya. Angalia Bukhari, Tafsiru’l-Qur’an 4; Tirmidhi, Faraidh 6; Tirmidhi, Tafsiru’l-Qur’an 5.
8. an-Nisa, 4/11.
9. an-Nisa, 4/11.
10. an-Nisa, 4/12. Jambo la kifani katika aya hiyo ni kuwa wanawake wanapewa haki ya madeni na wosia kama ilivyo kwa wanaume. “Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto.” Mwanamume au mwanamke anapofariki, madeni yake hulipwa, wosia wake hutimizwa halafu mirathi hugawanywa. Inamaanisha kuwa mwanamke ana namna zote za haki za kiraia na kijamii. Mwanamke anaweza kumiliki mali, anaacha mirathi, anapata mirathi, anatoa wosia, anatimiza wosia, anakopa na anakopesha. Yaani, Quran inampa mwanamke haki ya kumiliki mali na kutumia mali yake atakavyo; kwa hivyo, inampa mwanamke uhuru wa kuwa na mali binafsi. Angalia Süleyman Ateş, Çağdaş Kur’ân-ı Kerim Tefsiri, Yeni Ufuklar Neşriyat, 1988, 2/574; Kwa maelezo ya kina kuhusu hali ya mwanamke anayefiwa na mume inakuwaje mirathi yake, angalia Hamza Aktan, İslâm Miras Hukuku İşaret Yay., İstanbul, 1991.
11. Kwa maelezo zaidi kuhusu matumizi ya mwanamke na majukumu yake, angalia İslâm’da Kadın Hakları (Diwani) 2/178-283 Rehber Baş. Yay. 1. Baskı. Ankara, 1993.
12. Kwa maelezo zaidi, angalia Ruhi Özcan, İslâm Hukuku’nda Hısımlık Nafakası uk. 68-84, Çağlayan Yayınları İzmir, 1996.
13. Nursi, Badiuzzaman Said, Mektubat uk. 37, Envar Neşriyat, İstanbul, 1997; angalia pia Sözler uk. 381.
14. angalia Kasani, Alauddin Abu Bakr Ibn Masud, Badaiu’s–Sanai’ 4/28. Misri, 1328; Sarakhsi, Muhammad b. Ahmad, al-Mabsut 5/187. Misri, 1324; Ibn Rushd’il–Hafid, Muhammad Ibn Ahmad, Bidayatu’l–Mujtahid 2/55, Misri, 1379.
15. Mathalani, ikiwa mume ni masikini na mke ni tajiri, mume anawajibika. Mwanamke hawezi kuwajibishwa kwa ajili ya matumizi ya mumewe. Amri hiyo hiyo inafaa kwa mume asiyeweza kupata na kumpa matumizi mkewe kwa sababu kadhaa kama vile kuwa mlemavu. Katika hali hii, matumizi ya mwanamume hutolewa na ndugu wa mumewe, si mkewe. Mwanamke husaidiwa na nduguze. Matumizi ya ndoa ambayo mwanamke hupokea kutoka kwa mumewe ni deni lisiloondoka kutokana na maagizo. Hata kama mwanamke atatumia mali yake, anaweza kuchukua mali hiyo kutoka kwa mumewe. Angalia Özcan, Ruhi, Hısımlık Nafakası uk. 71.
16. Kwa matumizi ya wanandugu, angalia Ruhi Özcan, sawa na rejea ya hapo juu uk. 89-154.
17. Nursi, Badiüzzaman Said, Mektubat 37; Sözler uk. 381.
18. Kwa hifadhi ya kijamii ya mwanamke katika Uislamu, angalia Faruk Beşer, Kadının Çalışması Sosyal Güvenliği ve İslâm p.165-180, Nun Yay. İst. 1995; Bayraktar Bayraklı anasema, “Ikiwa baba katika familia ni mzee na ikiwa watoto wa kiume na binti wanafanya kazi kwa pamoja na kupata mali kwa pamoja, mafungu yao katika mirathi ni sawa.” Anatumia aya 32 ya sura an-Nisa kama ushahidi. Hata hivyo, aya hiyo haiwezi kuwa ushahidi kwa ajili ya suala hilo kwa sababu aya hiyo inaeleza kuwa mwanamke, aliyenyimwa mirathi katika enzi za Jahiliyyah, anahitajika apewe fungu lake kutoka katika mirathi. Fungu la mwanamke kutoka katika mirathi hutegemeana na hali mbalimbali zilizoelezwa zilizoamuliwa na aya na hadithi. Pia ni muhimu kusema kuwa kipato cha mtoto wa kike katika familia ya namna hiyo ni cha msichana tu. Hahitajiki kutumia mali yake katika matumizi ya familia. Ni mali yake binafsi. Angalia Bayraktar Bayraklı, Kadın, Sevgi ve Temel Hakları uk. 64, İşaret Yay. İstanbul, 2000.
19. Kuhusu kanuni za tabaka la kati na kanuni za Kiislamu, angalia İzzet Er, Sosyal Gelişme ve İslâm uk. 94-115, Rağbet Yayınları, İstanbul, 1999.