Nini zakah?
Kilugha, zakah ni, kuongezeka, kusafika, wingi, maadili mema na kusifu; kama ilivyo istilahi ya kidini, inamaanisha kutoa sehemu ya mali kwa watu maalumu ili kumridhisha Allah.
Zakah, ambayo ni moja ya ibada za kifedha, ni moja ya nguzo tano za Uisilamu; iliwajibishwa katika mji wa Madina katika mwaka wa pili wa Hijria. Yafuatayo yameelezwa katika Quran:
“Na shikeni Sala, na toeni Zaka…” (al-Baqara, 2/43, 110; al-Hajj, 22/78; an-Nur, 24/56; al-Mujadala, 58/13; al-Muzzammil, 73/20);
“Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.” (at-Tawbah, 9/103).
Umuhimu wa zakah (zaka) kwa mtu anayeipokea
* Zakah humuhifadhi mtu anayeipokea dhidi ya kuwa mtumwa wa mahitaji yake makuu. Hakuna kinachodhalilisha zaidi kama mtu kudharaulika na kutaabika na kuwahitaji wengine kwa sababu ya kutoweza kupata mahitaji yake ya lazima. Kwa hivyo, Mjumbe wa Allah (s.a.w.) ameeleza yafuatayo katika moja ya dua zake: Ewe Allah! Nakuomba taqwa, stara na neema kutoka kwako.”
* Zakah inamfanya masikini afanye kazi. Yafuatayo yanaelezwa katika hadithi: “Mkono unaotoa ni bora kuliko mkono unaopokea.” “Muumini mwenye nguvu ni bora kuliko muumini dhaifu.” Masikini atajaribu kuwa ni mkono unaotoa na sio mkono unaopokea; atajaribu kuwa mkakamavu na sio kuwa dhaifu. Isitoshe, hadithi ifuatayo inawahamasisha waumini kufanya kazi: “Hakuna aliyekula mlo bora zaidi kuliko yule aliyechuma kwa kazi yake.”
* Zakah inafifisha hisia za choyo kwa masikini. Inatokomeza chuki inayowaangukia matajiri. Hivyo, hakutakuwa na ubaguzi kati ya masikini na matajiri katika jumuia.
* Zakah inanyanyua hadhi ya masikini katika jumuia. Kwa kuwa, zakah ni haki ya masikini. Sio msaada wa matajiri. Matajiri hawataachwa bila ya jukumu hili isipokuwa wawatafute masikini na kuwapa zakah. Kwa kuwa masikini wanawaondolea matajiri jukumu la zakah, hadhi ya masikini ni ya juu katika jumuia.
Umuhimu wa zakah (zaka) kwa mtoaji
* Zakah humwokoa mtu dhidi ya kuhusudu kitu. Inavunja msururu wa uchu kwa binaadamu. Inauepusha moyo dhidi ya usugu na nafsi dhidi ya ushenzi.
* Zakah ni ufunguo wa kuwahurumia watu.
* Zakah huidumisha mali ya mtu. Mali iliyotumiwa kwa ajili ya jema la umma katika njia ya Allah haipotei bali hudumu milele.
* Zakah huunda na kutunza uwiano kati ya roho na kiwiwili.
* Zakah ni kielelezo cha shukurani za dhati kwa Allah. Shukurani zinazotamkwa kwa ulimi tu hazitotimiza wajibu wa shukurani za mali. Kushukuru kwa mali hutimizwa kupitia zakah na sadaqah.
* Zakah huitakasa mali. Zakah humsafisha mtu kutokana na ubakhili na sifa ya chuki, choyo, wizi na macho ya hasadi. Hivyo, inaboresha usalama wa mali na maisha ya binadamu.
* Zakah humkinga mwenye mali dhidi ya kuwa mtumwa wa mali na kumkomboa. Yafuatayo yanaelezwa katika hadith:
“Wale wanaohusudu dhahabu, fedha (pesa) na mahameli (anasa) wataangamizwa.”
* Zakah huuimarisha mwonekano wa matajiri na kuwaongoza katika heri. Inawaongezea hadhi yao katika jumuia.
* Zakah inaongeza mali. Inasababisha mali ikue na kuwa nyingi. Ipo ahadi iliyotolewa na Allah kuhusiana na suala hili.
Kutoa zakah hakusababishi mali kupungua.
* Zakah inamhimiza mtu mmoja mmoja kuwekeza.
* Zakah ni tiba ya kupenda dunia moyoni.
* Zakah inawakinga Waislamu dhidi ya fitina (majaribu) ya mali. Yanaelezwa yafuatayo katika aya:
“Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.” (at-Taghabun, 15).
Yafuatayo yanaelezwa katika hadith:
“Katika kila ummah kuna fitina (majaribu). Na fitina ya ummah wangu ni mali.”
* Zakah inamfanya Mwislamu kuwa na nidhamu kwa upande wa kipesa.
* Zakah inamkumbusha mtu mmoja mmoja juu ya umuhimu wa uwezo wa kipesa.
* Zakah (zaka) ni uwiano wa nguvu katika umiliki. Sio kuitokomeza mali ya mmiliki wake wala kuiacha yote kwa mwenyewe, kuwanyima masikini mali hiyo. Inaigawa mali kati ya masikini na tajiri kwa mujibu wa viwango maalumu.
* Zakah ni namna ya hifadhi ya kijamii na bima. Miongoni mwa malengo ya zakah ni kuwasaidia wahitaji, kuwasaidia watu wanyonge kama masikini, mafukara, wenye madeni na wasafiri wasioweza kufika ukomo wa safari yao. Chochote kinachoipa nguvu hadhi ya mtu ambacho kitamwimarisha kiuchumi na kumwendeleza kimwili na kiroho pia kinaiimarisha jumuia.
* Zakah ni bima inayoyaenea matabaka yote yenye kuhitaji kwa mahitaji yao yote kuanzia ya kimwili, kiroho na kimaadili. Misingi ya mwanzo ya hifadhi ya jamii ya kisasa imewekwa mwaka 1941. Wawakilishi kutoka UK na USA waliitisha mkataba wa Atlantiki wa mwaka 1941 na kuamua kuratibu taasisi ya hifadhi ya kijamii kwa mtu mmoja mmoja. Hata hivyo, Uislamu umeitambulisha taasisi ya zakah tokea karne 14 zilizopita.
* Zakah inaondoa mwanya na tofauti zilizopo kati ya matajiri na masikini katika jamii. Inapunguza masafa kati ya matabaka na kuwezesha kuundwa tabaka la kati.
Kuongezeka kwa idadi ya raia wa tabaka la kati kutaathiri soko kwa namna chanya. Mali husika haitokuwa ni kitu kinachomilikiwa na tabaka moja tu; uwezo wa kununua wa masikini utaongezeka, pia. Sio matajiri peke yao bali sehemu kubwa ya jumuia itaweza kukidhi mahitaji yake na kuishi kwa raha katika jumuia.
Aya ya 7 ya sura al-Hashr inakataza baadhi ya mali kuzungushwa miongoni mwa matajiri peke yao. Hili linaweza kufikiwa kwa njia ya zakah tu.
* Zakah inaziepusha mali kulimbikizwa; inazipelekea mali kuwekezwa. Kwa kuwa, hutolewa kutoka katika mtaji na sio faida; hivyo itapungua ikiwa haikufanyiwa biashara. Mmiliki atawekeza mali ili zisipungue; na atajaribu kuiongeza.
* Zakah huwezesha uwiano wa kijamii. Allah Mtukuka amewaumba watumishi Wake kwa namna tofauti kwa upande wa maumbile na viwango vya maisha. Baadhi yao ni; matajiri na wengine ni masikini na baadhi yao wapo kati na kati.
Yafuatayo yanaelezwa katika aya:
“Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki.” (an-Nahl, 71)
Ni muhali kwa kila mmoja kuwa na kiwango sawa cha mapato kwa sababu katika jamii kuna majukumu na kazi mbalimbali zinazotofautiana kwa upande wa majukumu na mazingira ya kazi. Baadhi ya wajibu na kazi zikitelekezwa, athari zake zitasababisha madhara yasiyorekebishika katika jamii. Kama aina zote za wajibu zina mshahara sawa, hakuna atakayetaka kufanya kazi ngumu zaidi; kila mmoja angependelea zile nyepesi. Hivyo, kazi ngumu zaidi na zenye majukumu mengi zingeweza kutelekezwa na mfumo wa maisha ungevunjika.
Kwa hivyo, ni muhimu kwa watu kuwa tofauti kwa upande wa kipato na viwango vya maisha. Hata hivyo, daraja ni muhimu ili kuzuia tofauti hii isitengeneze mporomoko. Daraja hili ni zakah.
* Zakah inawashikamanisha watu wa jumuia.
Zakah inawashikamanisha watu pamoja kwa kuwa ni aina ya mshikamano wa kijamii. Matajiri wataendeleza hisia za upendo, na huruma kwa masikini. Masikini wataendeleza hisia za utii, heshima, kufanya kazi kwa umakini kwa matajiri. Hisia za choyo, chuki na kijicho zitatulizwa na hata kutokomezwa. Matajiri hawatowadhulumu masikini na kuwaweka chini ya masharti; masikini hawaendeleza hisia za udhalilishaji, utumwa, kinyongo na husuda kwa matajiri. Yafuatayo yanaelezwa katika hadith: “Moyo humfanya mtu ampende anayemtendea ihsani na kumfanya mtu amchukie anayemtendea uovu.”
* Zakah huwaepusha watu kutokana na kufuga kinyongo na chuki na kutokana na kushirikiana na maadui wa jamii na wachochezi. Kama matajiri hawakidhi mahitaji ya masikini, ulazima na ugumu wa kifedha utawasababishia kujiunga na maadui wa Waislamu au utawasababishia kutenda shari kama kuiba, kupora au kuua.
* Zakah ni mlango wa uwekezaji na ni hatua kubwa ya maendeleo. Zakah ina mitazamo yote miwili ya kijamii na kiuchumi. Kwa hivyo, ni ari ya kuanzisha maendeleo.
* Tofauti kati ya matajiri na masikini mara zote imekuwa ikisababisha mapambano ya matabaka ambayo yamekuwa yakiendelea kufanyika waziwazi au kimya kimya tangu mwanzoni mwa maisha ya kijamii – mapinduzi na ghasia za umwagaji damu zilizoonekana katika historia ni ushahidi wa mapambano hayo ambayo ni mapambano ya “unacho; mimi sina”. Uislamu umezitambulisha taasisi za zakah, sadaqah ili kutuliza mapambano hayo yaliyopo tokea kuanza kwa maisha ya kijumuia; pia inawafundisha wafuasi wake wawe na subira, kutosheka na kuridhika na qadar. Ufahari wa mali wala husuda zinazosababishwa na umasikini hauonekani kuwepo baina ya waumini waliokuwa wakifundishwa kama hivyo.