Yaliyosomwa zaidi katika kifungu cha Allah (JJ)

1-) Je, inawezekana kuona ishara zinazohusu kuwepo kwa Allah kwa kuangalia katika ulimwengu?

Ni jambo lenye kupendeza kuwa Allah anaaziita sentensi zake mbili (aya) ndani ya Qurani na kazi zake katika kitabu cha ulimwengu (aya) (ishara). Ndani ya Qurani, moja kati ya ishara zilizotajwa mara nyingi za ulimwengu ni mbingu. Allah mara nyingi huelekeza mazingatio katika mbingu ambayo kila mtu huiona wakati wote na mara nyingi hupendezewa nayo.

 “Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyozijenga, na tukazipamba…” (Qaf, 50/6) 

Yafuatayo yameelezwa katika aya nyingine:

“Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakikakatika hayo zipo Ishara kwa wajuzi.” (ar-Rum, 30/22)

Aya ya kwanza inatuamrisha kuangalia katika ulimwengu na kutafakari. Aya ya pili inasema kwamba wale wenye kupata elimu ya uumbaji wa mbingu na ardhi na wale wanaotafakari kwa kutumia elimu hiyo wataona shuhuda kuhusu kuwepo kwa Allah. Aya hizi ziliteremshwa zaidi ya karne ya kumi na nne zilizopita. Kumekuwa na maendeleo makubwa kuhusu elimu ya mwanadamu juu ya anga tokea hapo. Tawi jipya linaloitwa elimu ya falaki limeundwa. Hatuwezi kutoa maelezo yote hapa. Tutajaribu kufahamu namna ya kusoma ishara za Allah kwa kutumia maelezo mapya ambayo tumeyapata kuhusu anga kupitia mfano mmoja.

Shuhuda kutoka katika anga juu ya kuwepo kwa Allah.

Tunapoangalia mbingu, inaonekana kama kuba nzuri ni kama iliyopambwa kwa dhahabu katika kasri ya Dunia hii. Katika mtazamo mwengine inaonekana kama bahari ya anga ambayo ndani yake mamilioni ya safina husafiri kwa kasi sana. Na bado katika mtazamo mwengine inaonekana kama mkusanyiko wa ndege ambazo ni kubwa mara mabilioni kuliko ndege zilizotengenezwa na mwanadamu na ambazo ni zenye kutembea kwa kasi zaidi.

Umewahi kufikiri kuna nyota ngapi mbinguni? Kumekuwa na majaribio mengi ya kujibu swali hilo lakini hakuna aliyeweza kupata jibu sahihi. Mnamo mwaka 2003, kundi la watafiti kutoka chuo kikuu cha taifa cha Australia walifanya makadirio kwa kutumuia vifaa vya kisasa vya teknolojia. Namba waliyoipata ilikuwa ni 70.000.000.000.000.000.000.000 (seventy sixtrilion). (1)

Kwa mujibu wa wanasayansi hao hao, idadi ya nyota angani ni nyingi mara kumi zaidi kuliko idadi ya chembe za mchanga ardhini. Tunapoifikiria kwa kipimo cha anga, mapigano ya umiliki wa dunia ni kama mapigano ya watoto kwa chembe moja ya mchanga. Mwisho, hata tukiumiliku ulimwengu wote tutakacho kimiliki hakitakuwa hata sehemu moja ya kumi ya chembe ya mchanga katika kipimo cha anga.

Kitu gani nyota na sayari ambazo idadi zake hatuzifahamu zinatueleza? Allah anatutaka tufikiri kuhusu namna gani zimekuja katika uwepo na namna gani zinatembea kwa mfumo wa kupendeza na kuelekeza mazingatio yetu kwazo. Tunaweza kuziweka idadi za nyota zisizo hesabika chini ya mwanga wa vipawa, elimu, na uzoefu tulionao. Tunaweza kufahamu namna viumbe hivi vya mbinguni vilivyokuja katika uwepo kwa kuvilinganisha na kitu kilicho tengenezwa na wanadamu.

Mwanadamu hajaweza kutengeneza nyota bado; hata hivyo, nchi zote zinajaribu kutengeneza sayari ndogo iitwayo Kituo cha anga cha kimataifa kwa kuunganisha nguvu zao. Kisha, tunaweza kufahamu, kwa kiasi fulani, namna nyota na sayari zilivyokuja katika uwepo kwa kuangalia sayari ndogo iliyotengenezwa na mwanadamu. Ninapotumia neno ndogo, usifikiri kwamba ninadharau moja kati ya kazi nzuri ya mwanadamu. Kwa kweli, najisikia fahari katika jina la ubinadamu kwa kazi hii nzuri, ambayo sitoweza kuifahamu hata nikitumia maisha yangu yote. Nataka kusema kwamba ni ndogo inapolinganishwa na ulimwengu pamoja na sayari nyengine. Ikiwa watu hapa wanajaribu kutengeneza kituo kingine cha anga, hawatoweza kufanya hivyo kwa sababu hatuna mamia, maelfu ya wanasayansi na wahandisi wa kufanya hivyo. Hatuna viwanda vya kuzalisha vifaa vya lazima. Yaani, ni lazima kuwa na elimu na elimu iliyoendelea katika matawi mengi ya sayansi kama fizikia, uhandisi, baiolojia, na hesabati ili kutengeneza sayari ndogo. Nguvu kazi na mashine pia ni lazima ili kuifanyia kazi elimu hiyo. Kwa ufupi sayari ndogo ni kazi ya daraja ya juu ya elimu na nguvu kubwa. Basi, trilioni za nyota na sayari ambazo ni kubwa zaidi na nzuri zaidi kuliko kituo cha anga cha kimataifa, ni kazi ya dhati ambayo ina elimu na nguvu isiyokuwa na mwisho. (2)

Mtu anayeangalia anga kwa umakini anaona kuwa inamuashiria Allah kwa uwazi zaidi kuliko maneno ya kiarabu “laa ilaaha illa llah” (Hakuna mola ila Allah). Kwa kuwa, kama ulimwengu utafananishwa na kasri, mwezi ni taa yetu ya usiku, jua ni jiko na taa yenye mwanga mkali, na nyota nyengine ni zenye kupambwa kwa dhahabu na taa ndogo zilizopambwa. Basi, nani aliyeziumba nyota hizi, jua na mwezi? Quran inajibu swali hili kama ifuatavyo;

“Ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Ametukuka na wanayo shirikisha.” (an-Nahl, 16/3).

“Na amefanya ukutumikieni usiku na mchana, na jua na mwezi, na nyota zikutumikieni kwa amri yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wenye akili.” (an-Nahl, 16/12).

Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao. (Yasin, 36/40).

Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua. (Yasin, 36/38).

Aya mbili zilizopita zinaashiria mzunguko wa jua. Sayansi ya falaki imegundua kwamba jua lilikuwa likizunguka katika karne ya ishirini tu, lakini ukweli kwamba Hz. Muhammad (s.a.w), ambaye hakuweza kusoma au kuandika ametueleza kuhusiana na hilo karne kumi na nne zilizopita ni ushahidi kamili kwa utume wake.

Kwa mujibu wa elimu ya falaki ya sasa, jua linatembea 225 km kwa sekunde, kilomita 13.500 kwa dakika na kilomita 810.000 kwa saa moja. Tukifikiria kasi ya ndege iyendayo kwa kasi zaidi namna inavyotembea, tunaweza kufahamu kwamba jua linatembea mara 100 kwa kasi zaidi kuliko ndege iendayo kwa kasi zaidi.

Katika ndege ya kigiriki mnamo mwaka 2005, marubani wawili walifariki kutokana na baridi kwa sababu mfumo wa kupooza hewa ulileta hitilafu na ndege ikagonga mlima katika dakika kadhaa. Basi, vipi trilioni za ndege (nyota na sayari) ambazo ni kubwa mara mabilioni na zenye kasi mara maelfu kuliko ndege zetu zinatembea bila ya kugongana na kuanguka ilhali hazina marubani? Tunapolinganisha nyota na sayari na ndege zilizotengenezwa na mwanadamu, tutaona kuwa dhati yenye elimu isiyo na mwisho, nguvu na hekima imeumba nyota hizo na kwamba yeye kwa kuendelea anazihifadhi na kuzidhibiti. Na hiyo ni ni sababu haya yameelezwa katika Quran;

“Hakika Allah ndiye anaye zuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wakuzizuia isipo kuwa Yeye.” (Fatir, 35/41)

Japo kuwa tumetengeneza mfumo wa kujihami dhidi ya makombora yaliyotengenezwa na mwanadamu, hatuwezi kufanya kitu bali kuangalia “makombora ya angani” ambayo yanaweza kutuangukia toka angani.

Shuhuda za kuwepo kwa Allah kutoka katika ulimwengu wa mimea.

Sio nyota tu pekee bali kila kitu tukionacha ambacho kimetezunguka kinatueleza kuhusu Mola wetu kupitia ndimi tofauti. Isha nzuri zaidi zenye kutueleza kuhusu Allah katika sayari ya bluu tunayoishi ni mimea na wanyama na wanadamu. “Maisha”, ambayo ni muhuri wa kiungu wanaoshiirikiana wote, unatuonesha Allah katika kila nyanja. Ni Allah ambaye ni Al-hayy (Aliye hai) na Al-Qayyum (Msimamizi), anayetoa uhai na kuuhifadhi. Qurani inaeleza ukweli huu kama ifuatavyo:

“Kwa hayo (maji) Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na mizaituni, na mitende, na mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanao fikiri.” (an-Nahl, 16/11).

Aya hii kwa uwazi inaeleza kuwa mimea imeumbwa kutokana na maji na Allah na kwamba kuna mafunzo makubwa ndani yake kwa wale wenye kutafakari. Sayansi inakubali kwamba asili ya uhai kwa sasa ni maji lakini haijaweza kufahamu kwa ukamilifu uhai ni kitu gani. Hata hivyo, kuna wanyama hai na mimea katika kila inchi ya sayari yetu.

Katika mwaka 2014 wanasayansi wa elimu ya mimea wameamua kuwa kuna spishi 350,000 za mimea. Yote hii ni yenye kufanana na yenye kutofautiana. Kwa vile yote imeundwa kutokana na atomu, elementi, molikuli na seli ambazo ni zenye kufanana; Kwa vile zina miundo tofauti na zina DNA tofauti, zinatofautiana.

Usiidharua mimea. Hakuna mwanadamu awezaye kufanya kinachofanywa na mmea mmoja. Kama tutataja kwa mujibu wa kila tendo linalofanywa na jani la kijani, itakuwa inaendana kuliita kila jani “kiwanda cha oksijeni na chakula”. Mwanadamu ameelewa kidogo kile kilichokuwa kinafanywa na jani la kijani kwa muda wa miaka milioni kati kati ya karne iliyopita. Dr. kelvin amepata tuzo ya Nobel kwa sababu alielezea moja ya stadi za jani la kijani. (3) Katika maneno mengine, baada ya kufanya juhudi kwa karne nyingi baadhi tu ya wanadamu wenye akili ndio wamekuja kufahamu kidogo kile kinachofanywa na mimea ya kijani. Hata hivyo, hakuna mwanasayansi anayeweza kufanya kinachofanywa na mimea. Kwa hivyo, tunapomuambia mtu wewe ni mfano wa nyasi huwa tuna msifu na kukashifu nyasi. Pengine anastahiki kuitwa nyasi mtu mwenye akili sana hata kupata zawadi ya nobel.

Mimea ambayo tunaidharua kwa kuita nyasi ni watumishi wetu, ambayo inajitoa muhanga kwa ajili yetu. Inatoa oksijini, ambayo ni hitajio letu kubwa, kwa kufanya kazi kwa kuendelea na hutoa vitamini vya lazima na protini kwa ajili ya miili yetu; inajitoa muhanga maisha yao kwa ajili ya kuendelea kwa maisha yetu. Wanadamu hutumia spishi zaidi ya elfu nne za mimea na wanyama kama chakula. Miti inafanya kazi kama viwanda vikubwa na kutuandalia chakula. Hatushukuru kikamilifu huduma ambayo mimea inatupa kwa sababu hatufikirii kuhusu ilo. Kutokana na pazia la sababu tunarejesha matunda kwa miti na mboga mboga bustanini. Hatuvipi thamani yake halisi. Kama tutajaribu kutengeneza tunda katika kiwanda, tusingeweza kununua tunda moja hata kwa bilioni 1 ya dola. Wingi wa chakula hauoneshi kwamba havina thamani bali huonesha wingi wa rehma. Kwa hakika, oksijini, ambayo ni kirutubisho chenye thamani zaidi kwetu ni bure lakini sio kama haina thamani. (4)

Kila mmea, kila tunda na kila mboga mboga ni neema ya kiungu ya kimaajabu na zawadi nzuri kutoka kwa mola. Jaalia kwamba kampuni imetoa biskuti zenye mbegu na ulipozipanda mbegu za biskuti, ukapata miti ya buskuti; utashangazwa. Itagonga vichwa vya habari na televisheni zitautaja mti huo. Kwa kweli, ni lazima kustaajabishwa na mtu anayestaajabishwa na biskuti kuwa na mbegu lakini kuzingatia maelfu ya matunda na mboga mboga zenye mbegu ni kawaida.

Sayansi ya sekula na falsafa isiyo na dini inaficha kazi ya kiungu ambayo ni miujiza kutoka katika nyanja zote nyuma ya pazia ya asili na sababu, kuzifanya zionekane za kawaida. Wanazifanya kazi za mwanadamu ambaye hubadilisha vitu viliopo katika miundo tofauti zionekane za kimaajabu. Katika kitabu chake cha mwisho alichotuteremshia Allah anatuuliza mara thelathini na moja:

 “Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayoikanusha” (ar-Rahman, 55/13,)

Kama tutatumia akili zetu na kuthamini na kushukuru thamani ya kila neema, hatuwezi kukana yeyote kati ya neema hizo. Hata hivyo, kama tutarejesha neema hizi kwa asili na kwa bahati, tutazikana zote. Mamia ya maelfu ya spishi ambazo zina vitamini na protini ambazo wanyama na wanadamu wanahitajia, na kwamba zinaendana na ladha yao, mdomo, meno, na tumbo ni katika shuhuda za wazi za rehema ya Allah. Mtu mwenye akili anaweza kumtambua mola wake hata kupitia tufaha moja. Muundo wa kimajabu wa tufaha, ambao umeundwa bila ya teknolojia (5) katika daraja la atomu, mulikuli, na seli unaonesha elimu isiyo na mwisho, nguvu na hekima ya mmiliki wake; uhusiano wake na makubaliano na jicho la mwanadamu, jino, ladha na tumbo huoenesha huruma isiyo na mwisho, rehema na msaada.

Mtu anayetumia akili yake vizuri anaweza kumtambua mola wake kwa kutazama tufaha moja. Ndio, mtu anayeweza kufahamu tufaha moja tu anaweza pia kufahamu kuwepo kwa mola wake. Kama nilivyotaja hapo mwanzo, usilidharau tufaha. Ni lazima kuandaa kiwanda kikubwa kama ulimwengu na kupanda mti ambao una seli hai ili kutenegeneza tufaha moja. Mtu asiyeweza kutengeneza seli moja hawezi kutengeneza mti wenye bilioni za seli kwa namna yoyote, jaalia ameweza asingeweza kuwa na taathira kwa jua na asingeweza kuratibu joto lake kuivisha tufaha, tunaweza kuoredhesha maelfu ya hali kama hii ya lazima kwa kutengeneza tufaha.

Badiuzzaman Said Nursi anaelezea kwa ufupi tulichokimaanisha hapo juu kama ifuatavyo:

“Anayeumba tufaha bila shaka lazima awe na uwezo wa kuumba matufaha yote ulimwenguni na kuleta majira ya kuchipua katika uwepo. Kinyume chake, asiyeweza kuumba majira ya kuchipua hawezi kuumba tufaha moja vile vile, kwa kuwa tufaha huundwa kutoka sehemu hiyo hiyo moja. Lakini anayetengeneza tufaha anaweza kutengeneza majira ya kuchipua. Kila tufaha ni mfano wa mti mdogo, hata wa bustani au wa ulimwengu mzima. Mbegu ya tufaha inayobeba ndani yake maisha ya mti mkubwa, kutoka katika mtazamo wa kisanaa, muujiza kama huo, anaye uumba mti na kama hivyo basi anaweza kufanya kila kitu.” (6)

Kwa hivyo, Qurani inatutaka tule kwa kufikiri namna chakula tunachokila huundwa, badala ya kula kwa lengo la kujaza matumbo yetu tu:

“Hebu mtu na atazame chakula chake. Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu, Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu, Kisha tukaotesha humo nafaka, Na zabibu, na mimea ya majani, Na mizaituni, na mitende, Na bustani zenye miti iliyo songana baraabara, Na matunda, na malisho ya wanyama; Kwa manufaa yenu na mifugo yenu.” (Abasa, 80/24-32).

Shuhuda za kuwepo kwa Allah kutoka kwenye ulimwengu wa wanayama.

Tunapowaangalia wanyama kwa kutumia akili zetu na elimu, tunaweza kusema kwamba kila mmoja ni mashine au “kiwanda chenye kutembea”. Mwanadamu amepiga hatua kubwa katika kutengeneza vifaa vya kiteknolojia tokea mapinduzi ya kiviwanda. Vifaa ambavyo havikuwahi kufikiriwa karne moja kabla kama televisheni, simu za mkononi na kompyuta vimekuwa ni sehemu katika maisha ya kila siku. Tunaishai katika zama za maajaabu ya kitejnolijia na kila siku tunaona mapya. Hata sayansi isiyo ya dini huzingatia uwezo wa mwanadamu wa kutengeneza vifaa changamani ili kufikia mahitaji yao na matakwa kama ni elementi ya msingi inayo mtofautisha yeye na wanyama. Ndege, magari, treni za umeme, na majumba marefu, ni matunda ya uwezo huu. Kila mtu anafahamu kupitia uzoefu wake kwamba hata kifaa kidogo zaidi kilicho tengenezwa na mwanadamu ni kazi ya sayansi na nguvu. Vifaa kila vinapokuwa changamani, elimu na sayansi zaidi huwa ni lazima. Kwa mfano, mtoto mweye elimu ndogo na nguvu ndogo anaweza kutengeneza gari ya mbao. Hata hivyo, hata maelfu ya watoto wakikusanyika pamoja, hawawezi kutengeneza hata gari ndogo. Kisha, linganisha wanyama na “maajabu ya kiteknolojia” ambazo ni kazi zetu.

Inaweza ikawa rahisi kwetu kumtambua mola wetu kwa kutafakari katika uumbaji na stadi za wanyama ambazo daima tunaziona katika maisha yetu, bustani za wanyama na maisha halisi ya wanyama katika televisheni. Qurani ina tueleza kupitia aya ifuatayo kuna mifano ya ishara katika wanyama.

“Hakika katika mbingu na ardhi ziko Ishara kwa Waumini. Na katika umbo lenu na katika wanyama aliowatawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini.” (al-Jathiya, 45/3-4).

Kwa kweli, si vigumu kuona ishara za kimifano kwa wanyama zinazotuambia kuhusu Allah kwa kuwaangalia kwa makini. Qur'an inawaelezea wale wasioamini kama vipofu na kusema kwamba hawataweza kuona ishara hizi isipokuwa waamini na kufungua macho yao kuona ukweli. Hebu tujaribu kusoma baadhi ya ishara kwa wanyama kwa kutumia akili zetu.

Wanasayansi waliyotafuta wanyama wameamua kuwa kuna takriban milioni 2 za spishi za wanyama tofauti hadi sasa. Kulingana na makadirio, takwimu hii ni asilimia 20 tu ya wanyama wote. Inakadiriwa kuwa kuna spishi milioni 10 tofauti za wanyama. (7)

Kwa mujibu wa wanasayansi wanaotafuta wanyama wanatuambia, hata mnyama mdogo sana ni ajabu zaidi kuliko bidhaa zetu za teknolojia kubwa katika suala la uendeshaji wake. Kwa maneno mengine, tunapolinganisha "vifaa vya kiteknolojia vya kibinadamu" na "vifaa vya kiteknolojia vya kiungu", tunaona tofauti kubwa kati yao. Katika kitabu alichoteremsha, Allah anatoa changamoto kwa mtu, ambaye anajivunia "vifaa vya teknolojia ya juu", kama ifuatavyo:

“Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa.” (al-Hajj, 22/73)

Achilia mbali kuzalisha nzi, haijawezekana kuzalisha hata seli ndogo ya nzi hadi sasa. Basi, hebu tuulize kwa maneno ya Quran:

“Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?” (at-Tur, 52/35).

Mfumo wa mwili wa ajabu wa wanyama unaonyesha kuwepo kwa Allah mara nyingi kama idadi ya aina zao na labda idadi ya wanyama wote; faida na madhara ya wanyama vinashuhudia hekima na rehema ya Allah. Qur’an inaeleza ukweli huu kama ifuatavyo:

“Na hakika katika wanyama mna mazingatio kwa ajili yenu.Tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na damu, maziwa safi mazuri kwa wanywao.” (an-Nahl, 16/66).

Yaani, hatupaswi kuwadharau wanyama. Hatupaswi kuwaita watu tunaowakasirikia "wanyama" na kudharau wanyama. Ni sahihi zaidi kuwapa wanyama majina kulingana na yale wanayofanya kama ifuatavyo: "kiwanda cha maziwa na nyama" kwa ng'ombe, kondoo na mbuzi, "kiwanda cha yai na nyama nyeupe" kwa kuku, "kiwanda cha hariri" kwa mdudu wa hariri na "kiwanda cha nyuki" kwa nyuki. Kwa kweli, tunapofikiria faida nyingine za wanyama hawa, hata majina kama hayo hayatoshi.

Katika aya ya juu, Allah anasema kuwa kuna masomo katika wanyama wa ndani ikiwa ni pamoja na ng'ombe. Tawi tofauti la sayansi linaloitwa dawa ya mifugo ilianzishwa ili kuelewa hekima hizo. Maelfu ya wanasayansi wamejaribu kuwaelewa lakini hawajaweza kumaliza bado.

Kwa mfano, Dk. Virtanen, ambaye alikuwa akijaribu kuelewa jinsi ng'ombe hutoa maziwa, hakuweza kuzalisha maziwa lakini aligundua jinsi ya kupata maziwa zaidi kutoka kwa ng'ombe. Alipewa Tuzo ya Nobel kwa sababu yake. (8) Sasa, ninawauliza swali hili: Kama tuzo ya Nobel inapewa kwa mtu aliyeelewa kwa kiasi fulani kile ng'ombe alichofanya lakini ambaye hawezi kuzalisha maziwa, ni aina gani ya tuzo tunapaswa kumpa ng'ombe?

Nadhani kila mtu anayeelewa kwa kiasi fulani ni nini ng'ombe wanavyofanya anahitaji kuwaheshimu. Kwa kweli, ninaweza kuelewa kwa nini Wahindus wanaabudu ng'ombe ingawa wanachofanya ni ukafiri. Nadhani kuwona ng'ombe kama viumbe vya kawaida ni ajabu sana kama kuabudu ng'ombe.

Maneno yafuatayo kwa muhtasari ya Badiuzzaman Said Nursi yanafupisha kile tulichosema hadi sasa:

“Kuweka ndani ya chuchu za ng'ombe, ngamia, mbuzi na kondoo, pamoja na mama za kibinadamu, kati ya damu na uchafu lakini bila kuchafuliwa, kitu ambacho ni kinyume kabisa, maziwa meupe, safi, mazuri, ya lishe, na kuchochea huruma katika nyoyo zao kwa watoto wao ambayo ni ya kupendeza zaidi, tamu na yenye thamani zaidi kuliko maziwa - hii inahitaji kiwango cha rehema, hekima, ujuzi, nguvu, utashi na utunzaji ambapo haiwezi kuwa kazi ya bahati changamani, ya mchanganyiko wa vitu, au ya nguvu pofu. " (9)

Ushahidi wa kuwepo kwa Allah kutoka kwa "Mwanadamu"

Ushahidi mwingine, labda muhimu zaidi, kwa kuwa kuwepo kwa Allah kunafanyika katika ulimwengu wetu wa ndani. Kila mtu anaweza kumtambua Mola wake kwa kutafakari juu ya uumbaji wake mwenyewe na neema anayopewa kila siku. Ushahidi ambao mtu anaona katika kila kitu katika ulimwengu huitwa "objective", yaani, "ushahidi wa nje" na ushahidi anao uona na anahisi ndani yake unaitwa "subjective", yaani, "ushahidi wa ndani". Ni rahisi kuelewa ushahidi wa ndani kwa sababu unategemea uzoefu wa kibinafsi. Kwa bahati mbaya, watu wengi wana shida ya kuona ushahidi huo kwa sababu hawafikiri juu ya miili yao wenyewe. Hata hivyo, Quran inaelekeza umakini wetu katika masomo juu ya uumbaji wa mwanadamu:

“Na katika umbo lenu na katika wanyama aliowatawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini.” (al-Jathiya, 45/4).

Katika kipindi ambacho hapakuwa na teknolojia kabisa, uumbaji wa mwanadamu umeelezwa katika Qur'ani kama ilitazamwa kupitia "ultrasound ya Mungu":

“Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Allah mbora wa waumbaji.” (al-Muminun, 23/14).

Mwanasayansi ambaye aliona uumbaji wa mwanadamu kutoka kwenye tone la maji katika uzazi wa binadamu kwa mara ya kwanza, alieleza kile alichoona kama "muujiza". Kushangaza kwa kutosha, hata waraka zilizoandaliwa kwa uelewa wa kidunia zilihitajika kuuita "muujiza wa maisha".(10)

Watu wengi wamesahau muujiza huu, ambao wanapata katika safari yao ya maisha, na wanaishi bila ya mazingatio na bila ya kushukuru kama kwamba wametumwa kutoka angani. Aya ifuatayo ya Qur'ani inawahimiza watu wenye akili kuamka kutoka katika kutozingatia na kuona muujiza wao wa uumbaji:

“Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri?” (Yasin, 36/77).

Kuumbwa kwa mwanadamu kutoka kwenye tone la maji kunaweza tu kuwa kazi ya dhati yenye ujuzi usio na mwisho, nguvu na hekima. Ikiwa mtu anadai kinyume, anaweza kuthibitisha madai yake kwa kumtengeneza mwanadamu au seli moja ya mwanadamu kutoka kwenye tone la maji. Qur'an imetoa wito wa kushindana kwa wasioamini kuhusu suala hilo kwa karne kumi na nne. (11) Hakuna mtu aliyeweza kujibu changamoto hii hadi sasa; hakuna mtu anayesema kuwa wanaweza hata licha ya teknolojia ya hivi karibuni. Hii inathibitisha kuwa Quran ni kitabu cha Allah na Allah ni Muumbaji wa viumbe hai vyote.

Uumbaji wa mwanadamu ni muujiza; Vivyo hivyo, neema ya maziwa ya mama kutoka kwa mama yake ni "muujiza wa rehema" tofauti. Wengi wetu tunaona kama tukio la kawaida. Tuseme kwamba juisi ya machungwa badala ya maziwa imetoka kwenye matiti ya mama zetu; tutafanya nini? Tutastaajabishwa na tutasema kuhusu hilo kwa kila mtu. Ni dhahiri kuwa itakuwa habari ya kwanza kwenye televisheni. Hata hivyo, "juisi ya machungwa" inayotokana na matiti ya mama zetu badala ya "maziwa" ni kitu ambacho ni mara elfu zaidi ya kushangaza na kwamba inahitaji kujiuliza zaidi. Wanasayansi wanashauri wanawake kunyonyesha watoto wao kwakuwa hawajaweza kupata kitu cha kuchukua nafasi ya maziwa kikamilifu. Kama inavyoonekana katika mfano wa maziwa, kila kitu ni ajabu na muujiza lakini huonekana kuwa vya kawaida kwetu kwa sababu sisi daima tunaviona. Wale wanaofungua "jicho la akili" kwa uangalifu wanaweza kuona matendo ya miujiza na mtendaji wao nyuma ya "pazia la kawaida".

Ninataka kutoa mfano mwingine kuhusiana na ushahidi wa ndani. Wakati mtu anafikiria mwili wake mwenyewe, anaweza kuona ishara zinazoonyesha Mola wake. Kila kiungo cha mwili wetu, mpangilio wao bora na utendaji, utaratibu wao na hekima na faida zisizo na hesabu zinatuonyesha sisi dhati yenye ujuzi usio na mwisho, hekima, huruma na nguvu. Ninataka kukuambia juu ya kitu ambacho nimejifunza hivi karibuni na kukiweka wazi kile ninachotaka kumaanisha. Nina meno yaliyofanywa na binadamu na meno ya asili katika kinywa changu. Sikupata mtu wa kawaida kufanya meno yangu. Nilikwenda kwa daktari wa meno mwenye ujuzi ambaye alikuwa amehitimu kutoka katika kitivo cha meno. Kwa nini nilikwenda kwa daktari wa meno na si mtu wa kawaida? Jibu ni rahisi: Kwa sababu sio rahisi sana kupata nyenzo nzuri kwa meno, kuyafanya kwa usawa na meno yangu mengine na kuyaweka katika kinywa changu. Si kila mtu anayeweza kufanya hivyo. Mtu ambaye hana ujuzi wa kutosha wa meno na ambaye hana zana muhimu hawezi kufanya hivyo.

Sasa, hebu tulinganishe "meno yaliyofanywa na binadamu" na "meno mengine". Yepi ni bora zaidi? Ambayo ni salama zaidi? Ambayo ni kamilifu? Bila shaka, ni yale mengine. Mfano wa wazi zaidi ni kwamba hakuna daktari wa meno anasema niruhusu kutoa meno yako na kukuekea meno ya kisasa ya teknolojia badala yake kama meno yako ni mazima.

Sasa, hebu fikiria kwa uangalifu: "meno yaliyofanywa na binadamu" yanaweza kutolewa kupitia teknolojia ya juu na nguvu; basi, inawezekana kwa yale "meno" mengine, ambayo ni bora zaidi kuliko meno yaliyofanywa na wanadamu katika kila kipengele yaweze kujiunda wenyewe au kwa bahati mbaya? Je, yanaweza kuwa kazi ya nguvu ya asili ambayo yamenyimwa ujuzi na ufahamu na ambayo ni jinga na yasio na akili? Basi, kila jino letu ambalo sio lililotengenezwa na mwanadamu linatujulisha kuhusu Allah. Kwa kuwa meno, ambayo ni miongoni mwa sehemu rahisi zaidi za mwili wetu, yanatujulisha kuhusu Mola wetu kama hivyo, narejesha kwa akili yako kufikiri juu ya jinsi mamia mengine ya viungo kama jicho, pua na ubongo vinavyotuambia kuhusu Allah.

Tunaweza kufupisha kile tulichoandika hadi sasa kama ifuatavyo:

Mola wetu amefanya ulimwengu kuwa kitabu kizuri na kutujulisha juu yake mwenyewe kupitia maneno (ishara) ya viumbe hai na viumbe visivyo na uhai ambayo aliandika ndani yake. Alitafsiri kitabu hiki kupitia Qur’an na kutufundisha jinsi ya kusoma kitabu hiki kupitia Hz.Muhammad (s.a.w), ambaye ni mwalimu mkuu. Tunapoondoa glasi nyeusi za bahati na asili na kusoma kitabu cha ulimwengu kupitia glasi za uwazi ambazo Quran inatupa, tunaweza kumwona Mola wetu, kuchunguza shughuli zake na kutafakari juu ya hekima yake katika kila kitu tunachosoma. Tunaweza kumjua kwa njia ya kazi zake zisizo na hesabu na kumpenda kwa njia ya neema zake zisizo na mwisho.

"11 Eylül’e Rağmen Amerika’da Yükselen İslam (Islam Rising in America despite September 11)" Nesil Yayınları 

Maelezo ya chini:

(1) Unaweza kufikia makala iliyotajwa katika maandishi kwa njia ya kiungo kinachofuata:

http://www.cnn.com/2003/TECH/space/07/22/stars.survey/

(2) Yafuatayo yamesemwa katika aya ya Quran: “Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu.” (Luqman, 25)

Neno "wao" linatumiwa kwa wasioamini katika aya hii. Aya hii huangazia mambo mawili muhimu: Kwanza, inafaa zaidi kuanzia uumbaji wa mbingu na ardhi, ambazo ni ishara kubwa zaidi, unapowaambia wasioamini kuhusu Allah. Pili, hata wasioamini hawawezi kueleza uumbaji mkubwa na utukufu wa mbingu na ardhi; wakati wanafikiria vizuri, watasema "Allah".

(3) http://nobelprize.org/nobel_prizes/chemistry/laureates/1961/calvin-bio.html

(4) Katika mfumo wa soko huria, bei zimewekwa kulingana na usambazaji na mahitaji, sio thamani ya bidhaa na huduma. Sababu ya kwa nini oksijeni, ambayo ni muhimu kwa mwanadamu, ni bure haionyeshi kwamba haina thamani, lakini ni nyingi; ili, kusiwe na mtu anayelipia fedha kwa ajili yake. Ni kosa kwamba watu hutathmini bidhaa na huduma kulingana na bei ya soko. Kwa kweli, vitu vingi ambavyo haviuzwi na kununuliwa kwenye soko ni vyenye thamani sana.

(5) Kuchunguza suala hilo katika mwelekeo wa atomiki au molekuli na kufunua sifa zake mpya.

(6) "Umekutana na mahitaji yako ya chakula, vinywaji na nguo katika duka la dunia. Ikiwa utalipa pesa kwa ajili ya bidhaa hizi za bure kutoka hazina ya kimungu, ungeweza kununua komamanga moja kwa pesa nyingi na kwa kutumia muda mwingi. Kwa maana, makomamanga hayo yanahusiana na vitu vyote. Inaeleweka kutoka kwa vitu vyema kama kudarizi, nidhamu, sanaa, harufu, ladha na harufu nzuri kwamba komamanga ni kazi ya Muumba anayeumba kwa urahisi, na hahitaji mawasiliano ya kimaada nayo."(Badiuzzaman Said Nursi, Hubab Risalesi, Mesnevi-i Nuriye).

(7) Kuna baadhi ya wanasayansi ambao wanakadiria kuwa idadi ya wanyama ni milioni 100: http://news.bbc.co.uk/2/hi/science/nature/4013719.stm

(8) Dk. Virtanen alipata Tuzo ya Nobel katika Kemia mwaka 1945 kwa kazi zake zinazohusiana na kuongeza uzalishaji wa maziwa wa ng'ombe.

(9) Badiuzzaman Said Nursi, Mwale was aba, Ishara kuu.

(10) Hati iliyoitwa "Muujiza wa Maisha" iliyotengenezwa na NOVA, mmoja wa wazalishaji wa hati nzuri, ni mfano tofauti wa hilo.

(11) Unaweza kusoma jinsi Thomas, mtu asiyeamini Mungu, amenyamazishwa na changamoto ya Quran katika kitabu kinachoitwa Rabbini Arayan Thomas (Thomas akimtafuta Mola wake) na mwandishi aliyechapishwa na Nesil Yayınları (Publications).


2-) Tawhid (Umoja wa Mwenyezi Mungu) ina maana gani?

Umoja wa Mwenyezi Mungu maana yake ni: kuamini kutokuwepo kwa mungu yoyote isipokuwa Allah , kwa “kusema maneno laailah illah - Hakuna Mola ila Allah.”

Papo hapo umoja unatukumbusha kuhusu tamko laaillah ilaallah . Hili huitwa neno la upwekesho na maana yake ni kwamba hakuna mola wa kweli wa kuabudiwa isipokuwa Allah.

Malinganisho kadhaa yamefanywa kuhusu uwepo wa ulimwengu huu. Moja kati ya hayo ni kasri la ulimwengu. Kwa hivyo, umoja ni kumjua mfalme wa kasri hili kwamba ni mmoja na kutomshirikisha na yoyote.

Juu na chini ya kasri ya ulimwengu hakuwezi kumilikiwa na dhati tofauti. Taa, na vitu vingine vya ndani ya kasri haviwezi vikawa vimeletwa kutoka dunia nyengine na kuwachwa hapa. Kila kitu katika kasri na muhimu kuliko vyote, kila mgeni, anazaliwa katika kasri hii. Hebu tuangalie ua: kutokea katika dunia hadi katika jua, kila kitu kina mchango ndani yake. Na hebu tuuangalie mwili wa mwanadamu sehemu zake ambazo ni mawe ya msingi katika kasri hili, yapo ndani yake pia.

Milima huanzishwa juu ya tambarare kama viti vya kuegemeza mikono, kwa kutoletwa kutoka sehemu nyengine, bali huchomoza kutokea sehemu tambarare. Matunda yameambatana na matawi, kwa kutotokea kutoka katika nchi nyengine, bali yamekuja kutoka katika mti.

Mtoto huwa juu ya mapaja ya mama yake, hakuletwa kutoka katika nchi nyengine anakuwa katika fuko lake la uzazi. Jua ni taa ya kasri hili; halikununuliwa kutoka sehemu nyengine bali limeumbwa pamoja na mbingu.

Katika dunia hii, viumbe visivyo hisabika huungana na baina yao mchanganyiko hutokea na dunia hii ya viumbe hupewa muundo wa kasri. Watu wanaoakisi njia hii husoma neno la umoja na kufahamu kwamba kasri hili ni mali na kiumbe cha Allah pekee.

Wakati neno la umoja likiwa na maana ya kwamba hakuna mola wa kweli wa kuabudiwa isipokuwa Allah, jina la Allah linakusanya majina yote ya kiungu kwa hivyo, hubeba maana kama hakuna anayetoa maisha isipokuwa Allah hakuna muumbaji isipokuwa Allah hakuna isipokuwa Allah. Na kama hivi ndani ya umoja kuna wingi wa umoja kwa idadi ya majina ya kiungu.

Baadhi ya wanachuoni huugawa umoja katika sehemu mbili umoja unaogemea katika elimu na umoja unaegemea katika matendo. Kwa mujibu wa mgawanyo huu, kujua kwamba Allah ni mmoja na kwamba vitu vyote vilivyokua katika hali ya umoja ulimwenguni vinaonesha umoja wake ni umoja unaoegemea katika elimu. Umoja unaoegemea katika matendo ni umiliki wa imani hii ya umoja kwa ukamilifu ndani ya ulimwengu wa matendo wa mwanadamu.

Aya, “Iyyaka na’budu wa iyyaka nastain” Wewe tu ndie tunakuabudu, na Wewe tu ndie tunayekuomba msaada. Ya sura al-fatiha inatufundisha umoja unaoegemea katika matendo. Tunaelekea upande ambao wewe unataka tunasimama kwa heshima ya uwepo wako tu; tunainama na kukusujudia Wewe tu. Tunafikiria kuhusu mambo unayoyaridhia na tunawapenda wale tu unaowaridhia.

Mtu anayemuabudu Allah pekee anakua amewekwa huru kutokana na udhalili wa kuabudia miungu wa uongo; mtu anayetafuta msaada wa Allah pekee huwa huru na kuabudia sababu na huwa huru pia na kua mtumwa wa matukio. Huomba msaada kutoka kwa mola hali ya kuwa akiwa na utegemezi kamili hii ni yote mawili furaha na nguvu ya ushindi.

Kwa kuongezea, njia ya kuwa muumini kamili ni kwa kupitia ukamilifu katika umoja unaoegemea elimu na umoja unaoegemea matendo.

Umoja hauishii katika mambo hayo tu. Umoja wa sifa, majina na matendo pia upo. Aina hizo zinaweza kufupishwa kama ifuatavyo:

Umoja wa matendo: “Kujua kwamba sababu hazina taathira katika uumbaji wa vitu na katika kuviongoza”, “kuamini kwamba wa pekee ni Allah pekee.”

Umoja wa matendo: “Kufahamu kwamba sifa kama elimu, nguvu, utashi ambazo zinaambatana na viumbe nazo pia ni viumbe wa Allah na sio kuzipa dhati ya kujitegemea.

Umoja wa dhati: “Kufahamu kwamba viumbe vyote havina uwepo unapovilinganisha na dhati yake na uwepo wake.”

Kuhuisha na kufisha, kuponya, kuongoza katika njia sahihi, kutoa chakula kila moja ni kitendo tofauti. Matendo haya yasiyo na ukomo hutegemea sifa hizo hizo. Sifa hizo ni uhai, elimu, nguvu, kusikia, kuona utashi, kuongea na kuumba. Hivyo umoja wa matendo ni kufahamu kwamba matendo yote ya tangu ambayo yanafanya kazi katika ulimwengu wa uumbaji huja kutokana na sifa hizi za kiungu na kuzirejesha sifa hizi kwa dhati moja peke yake ni umoja wa dhati.


3-) Ni zipi tofauti kati ya Imani juu ya “Mungu “ katika dini tofauti na imani juu ya “Allah” kama ilivyoelezwa na Quran; na ni zipi sifa za Muumba kama zilivyobainishwa na Uislamu?”

Quran inajibu swali hili kwa ufupi katika sura ndogo yenye maana ya kina. Kwa sura hii Allah anataka kusahihisha kosa lililoenea baina ya wanadamu; Pia anawaokoa Waislamu kutokana na kosa ambalo Wakristo wamelifanya. Allah anajibu swali la hapo juu katika sura al-Ikhlas kama ifuatavyo:

Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee; Mwenyezi Mungu Mkusudiwa; Hakuzaa wala hakuzaliwa; Wala hana anaye fanana naye hata mmoja. (al-Ikhlas, 112/1-4)

Aya ya mwanzo inakataa namna zote za shirki kwa kusema kuwa Allah ni mmoja na sio zaidi ya mmoja. Aya ya pili inasema kuwa yeye hahitajii chochote lakini kila kitu kinamuhitaji Yeye kila wakati. Aya ya tatu inasema kuwa imani ya utatu ni batili na kwamba kitu kilichozaliwa na kuwa mtoto hakiwezi kuwa Mungu. Aya ya nne inasema kuwa Yeye yupo tofauti na viumbe vyote kama Muumba na haifai kumlinganisha na chochote.

Quran inataja Muumba aliye hai ambaye anaumba wakati wote na anayehifadhi ulimwengu wa kuwepo kwa kuendelea pamoja na kudhihirisha jina lake la al-Qayyum (Mwenye kuwepo kwa kujitegemea). Quran inawajibu ambao wanadai kuwa Mungu ameumba ulimwengu kama kwamba ametengeneza saa na kuiacha peke yake kama ifuatavyo:

 “Vinamwomba Yeye vilivyomo katika mbingu na ardhi. Kila siku Yeye yumo katika mambo.” (ar-Rahman, 55/29)

Aya inasema kwamba viumbe wote humwomba Allah ili kufikia mahitaji yao wakati wowote na kwamba Allah anajibu maombi haya. Tunaposoma aya kinyume, tunaweza kupata maana kwamba kama kusingekuwa na uumbaji wa kuendelea dua za viumbe zingelikua hazina maana. Aya zifuatazo zinatujulisha kwamba ulimwengu unahifadhiwa na Muumba kwa kuendelea kwa jina lake la al-Qayyum:

 “Mwenyezi Mungu, hakuna mungu ila Yeye - Aliye Hai, Msimamizi wa yote milele.” (al-Baqara, 2/255 and Aal-i Imran, 3/2).

( (1) Kumfananisha Allah na mwanadamu ni kosa la msingi ambalo dini nyingi hulifanya. Ukristo na Uyahudi unaegemeza mtoto kwa Allah wakati ambapo inaaminika katika dini nyingi za kishirikina kuwa Mungu amezaliwa. Nilishangazwa na kauli ya mzungumzaji wa Kihindu katika shirika liitwalo siku ya sala duniani iliyofanywa na The Unity Church wiki ya pili ya mwezi wa Septemba aliposema: Leo ni siku muhimu kwetu kwa sababu “Leo ni siku ya mazazi ya Mungu mkubwa ambaye Wahindu wanamuamini.”

 “Maandiko hapo juu yamefupishwa kutoka katika kitabu cha Dr. Furkan Aydıner ambapo ndani yake amekusanya maandishi aliyoandika alipokuwa anaongea na makundi ya wasio na dini.”


4-) Nini maana ya kumwamini Allah?

Maana yake ni kuamini juu ya uwepo na umoja wa Allah na kumjua vizuri kupitia majina yake na sifa zake. Kuamini Allah ni msingi wa dini zote. Haja ya kumuamini Allah, kumtegemea na kumuabudu yeye ipo katika asili ya mwanaadamu. Hisia hizo alizaliwa nazo mwanaadamu na zimeendelea kila zama.

Ni moja ya dalili ya uwepo wa Allah. Kwa kuwa asili ya mwanaadamu haisemi uongo. Kwakuwa kuna haja ya kumuamini na kumtegemea Muumba mtukufu, kumuabudu, kumuomba, na kupokea anayoyahitaji mtu kutoka kwake, hivyo, ni muhali kwa Muumba mtukufu huyo kutokuwepo. Itamaanisha kukana asili ya mwanadamu. Hata kama hakuna dalili nyingine, dalili hii ya uumbaji na ufahamu ni nuru ya kutosha kufahamu kuwepo kwa Allah.

Kwa kweli, wale wanaothubutu kumkana Allah, wanalazimika kumuelekea Allah na kuomba msaada wake wanapokuwa katika shida. Hata hivyo, shida inapoondoka tu, hurudi katika hali yao ya mwanzo.

Bila ya shaka umeona na kusikia mifano mingi inayohusu jambo hilo. Jambo hilo limeashiriwa katika Qur’an kama ifuatavyo:

"Na mtu akiguswa na shida hutuomba naye kaegesha ubavu, au kakaa, au kasimama. Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea kama kwamba hakupata kutuomba tumwondoshee shida iliyo mpata. Ndio namna hiyo wamepambiwa warukao mipaka yale waliyo kuwa wakiyatenda." (Yunus, 12)

"Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha." (al-Ankabut, 65).


5-) Nini maana ya Allah kuwa huru na mbali kutokana na wakati na sehemu? Je, unaweza kuelezea kupitia mifano?

Dhati ya Allah na sifa zake ni za tangu… dhati na sifa zetu ziliumbwa baadaye… bila ya shaka, hatuwezi kujua dhati yake au sifa zake vya kutosha; hatuwezi kufahamu kuwa kwake wa tangu na kuwa kwake huru kutokana na wakati… Vipi tutaweza kufahamu hayo? Hatuwezi hata kufahamu wakati ni kitu gani!..

Wakati ni nini? Ni kitu cha aina gani? Kitu chenye kutembea katika mto mmoja katika wakati mmoja, lakini kwa nini unaathiri vitu kwa tofauti? Huwafanya watoto wawe viana, watu wa makamo kuwa vizee na vizee kuelekea katika umauti. Je, mto huu unatembea kuelekea chini au juu?

Shairi lina uliza kwa uadilifu:

Wakati ni nini, ni nini?

Ni maji au ndege?

Wakati ni nini, ni nini?

Chini ya mlima au juu ya mlima?

Tumewekewa mpaka na wakati. Tuna jana na kesho. Ni awamu za muda wote wa maisha. Hata hivyo, awamu zote hizo ni zenye mahusiano; zimepewa majina kwa uhusiano. Leo iliitwa jana masaa ishirini au thelathini yaliyopita. Asubuhi, tutaiita jana. Muda uliyopita na ujao hauna tofauti na jana na leo. Kila siku, kila saa, hata kila wakati ni dunia yenye kujitegemea… Yote yanayojiri katika ulimwengu katika wakati fulani huleta michoro tofauti ukilinganisha na wakati mmoja kabla yake na wakati mmoja baada yake. Hivyo, mchoro tofauti unadhihirishwa katika dunia hii kila wakati.

Wakati unasomwa kupitia michoro hiyo iliyopangiliwa katika mistari, au michoro hiyo imezamishwa ndani ya wakati. Maneno mengi yamesemwa kuhusu wakati. Bila ya kujali asili yake halisi ni kitu gani, wakati, ambapo ni dhana inayohusiana na vitendo, harakati, kutulia na kuondoka kwa viumbe, hauwezi kuwa tendaji kwa Mola na Muumba wa limwengu zote. Anajua kila kitu ambacho kiliumbwa na kitakachoumbwa kupitia elimu yake ya azali.

Aya ifuatayo inaeleza vizuri sana:

Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari? (al-Mulk, 14 )

Mtu anayetazama kitabu lazima afikiri kwamba kila neno, mstari, na herufi ndani ya kitabu hiki imeandikwa. Hivyo, yule aliyeandika hayo lazima atakuwa tofauti na maandiko na kuwa huru na kufanana na herufi na maneno!..

Ulimwengu, wanadamu wote, wanyama, mimea wanatiririka katika mto wa wakati kwa kuendelea… wanaelekea upande wa umauti na akhera. Anayefanya mto huo utiririke bila ya shaka yupo huru na wakati. Hiyo ni kusema, hajafungwa au kudhibitiwa na wakati. Na hakuna kati ya hao wanaotiririka katika mto huo awezaye kufahamu kuwa huru kutokana na wakati vya kutosha.

Allah yupo huru na mbali kutokana na sehemu, pia. Tunaweza kutoa mwanga wa jua kama mfano: Upo katika vitu vyote vyenye kung’ara ulimwenguni kupitia rangi zake saba; Lipo na linaonekana katika kila kitu kwenye mfumo wa mwanga, joto na rangi saba, ambazo ni kama sifa zake; hata hivyo, halipo lenyewe dhati yake katika kila kitu linachokimulika na kukiangazia. Hiyo ni, jua lipo katika vitu vyote vyenye kung’ara ulimwenguni kupitia sifa zake lakini halipo katika kitu chochote kiupande wa ukubwa na umbo lake.

Sifa na asili ya Allah ambaye analipa jua sifa hizi, ni kamilifu sana kufahamika na akili zetu. Allah amekizunguka kila kitu kupitia sifa zake, hiyo ni kusema, kupitia nguvu zake, elimu na utashi. Hata hivyo, hayupo katika kitu chochote kwa dhati yake. Hiyo ni kusema, Yeye yupo kila mahali kwa sifa zake. Na hayupo sehemu yoyote kwa dhati yake. Kwakuwa Yeye ndiye aliyeumba sehemu; hahitajii sehemu.


6-) Je inawezekana kwetu kumuona Allah na kufahamu asili yake halisi?

Haiwezekani kwa mwanadamu kumuona Allah katika dunia hii na kufahamu asili yake halisi.

Ni kwa sababu akili na hisia za mwanadamu zina ukomo. Havitoshi kufahamu asili halisi ya Allah. Hata hivyo, mwanadamu anaweza kufahamu uwepo wake na umoja wake kwa kuangalia viumbe na kufahamu nguvu yake isiyokuwa na ukomo, na sifa zake nyingine pamoja na majina yake.

Kwa hivyo, Allah ametukataza kufikiria kuhusu dhati yake na asili yake halisi; ametuamuru kufahamu kuwepo kwake na umoja wake na kufahamu sifa zake na majina yake.

Hayo yameelezwa katika hadithi:

“Angalia mbingu na ardhi na jiangalie wewe mwenyewe ili uweze kufahamu kuwepo na umoja wa Allah; na fikiri kuhusu uzuri katika maumbile ambao hushangaza akili na kwamba haviwezi vikawepo wenyewe. Kwa sababu, hizo ni dalili zenye kuonesha kuwepo na umoja wa Allah.

Hata hivyo, usifikiri kuhusu dhati na asili halisi ya Allah. Usianze kufikiri ‘Je, Allah ni kama hivi au kama vile?’ Vipi Allah huona na kusikia? Nguvu yako haitatosha katika hilo. Hata ukijaribu vipi, huwezi kujua na kufahamu vizuri. Utachanganyikiwa. Vipimo vyako vya elimu na uzoefu havitatosheleza.

Ikiwa tutafikiri japo kidogo, tunaweza kufahamu kupitia akili zetu kwamba ni muhali kufahamu asili halisi ya Allah. Kifaranga ndani ya yai hatarajiwi kufahamu dunia iliyo nje ya yai. Akili ya mwanadamu haitofautiani na kifaranga ndani ya yai kuhusu suala la kujua ulimwengu wa kushangaza na Nyanja za ulimwengu ambazo Allah ameziumba. Hivyo, haiwezekani kwa akili ambayo imewekewa uwezo wa kufahamu wenye ukomo kufahamu asili halisi ya aliyeumba ulimwengu pale mtu anapofikiri kuhusiana na hilo kupitia akili yake.

Mehmed Kırkıncı anafafanua kuhusiana na jambo hilo kama ifuatavyo:

 “Jaalia kwamba kuna mtu ameishi ndani ya pango na kwamba hakuwahi kuona mwanga wowote na kwamba alitolewa nje ya pango mapema asubuhi kabla ya jua kuchomoza. Pale mtu huyo ambaye amepata kizunguzungu kwa mwanga ambao umekuja kutoka kila sehemu alipo ambiwa kwamba mwanga umetoka katika jua, angelishangazwa na jua hilo na angelijaribu kujua kuhusiana na jua hilo.

Ni wazi kwamba, vyovyote alivyolifikiria jua katika mawazo yake, asingeweza kulifahamu jua na angelifikiria vitu tofauti kila mara atakayojaribu kulijengea picha jua hilo. Angelilifananisha jua hilo na vitu alivyoviona;  kila mfanano ungelikuwa si sahihi.

Ikiwa kuamini juu ya jua ingelikuwa msingi wa Imani kwa mtu huyo, vyovyote angelifikiria jua angefanya shirki. Kitu pekee angeliweza kufanya ingelikuwa ni kufahamu kwamba mwanga umetoka katika jua lakini asingeliweza kujua asili halisi ya jua hilo. Kwa hakika, Imani inayotarajiwa kutoka kwake ni hiyo tu.

Kama ilivyokuwa mtu huyo katika mfano hawezi kulifahamu jua, mwanadamu hawezi kufahamu asili halisi ya mfalme aitwaye roho ambaye anatawala katika nchi ya mwili wake. Japo kuwa tunajua kwamba miili yetu hufanya kazi pamoja na roho, na kwamba mwili utashindwa kufanya kazi pale roho itakapouacha mwili huo, kwamba mfalme anautazama ulimwengu huu kupitia dirisha la jicho, anafahamu ulimwengu wa sauti kupitia sikio, na anaonja kila kitu kupitia mizani ya ulimi, sisi hatufahamu asili  halisi ya roho. Vyovyote tusemavyo kuhusiana na asili yake halisi, itakuwa ni kinyume na ukweli; vyovyote tuifikiriavyo dhati ya roho, tutafanya makosa kuhusiana na hilo.

Mwanadamu, ambaye ni dhaifu kuelewa au kufahamu dhati ya jua ambayo hakuwahi kuiona kabla na ambaye ni mjinga mno kufahamu  asili halisi ya roho yake, hawezi kumfahamu, kwa namna yoyote, muumbaji mtukufu na mmiliki wa kweli wa limwengu zote. Ambaye yupo huru kutokana na wakati pamoja na mahali; itakuwa ni kosa kubwa na uendawazimu kujaribu kuifahamu dhati yake na ni fikra isiyo ya kawaida ambayo itamfanya mwanadamu adondoke katika shirki.” .” (Hikmet Pırıltıları: Glitters of Wisdom)


7-) Ni upi umuhimu wa Imani juu ya Allah?

Msingi wa kuamini juu ya Allah ni kama msingi wa jengo au mizizi ya mti. Jengo haliwezi kuwepo bila ya msingi na mti hauwezi kuwepo bila ya mizizi; vivyo hivyo, misingi mingine ya Imani haiwezi kuwepo bila ya Imani juu ya Allah. Kwa kuwa matawi yote ya Imani hupatikana na kukua kwa kutegemea msingi wa Imani juu ya Allah.

Kwa mfano, mtu asiyeamini juu ya Allah hawezi kuamini juu ya Qadar (Kadari), ambayo ni kielelezo cha elimu ya Allah. Ni muhali kuamini juu ya akhera moja kwa moja bila ya kuamini juu ya Allah, ambaye atakayeumba akhera. Inawezekana kutoa mifano zaidi. Matawi yote ya Imani yanaegemea katika msingi wa Imani juu ya Allah.

Imani na uongofu (hidayah) ni nuru iliyotumwa katika moyo na Allah baada ya mtu kukubali Imani na uongofu kupitia utashi wake. Shukrani kwa nuru hii ing’aayo, mwanaadamu anasoma mapambo yote ya majina ya Allah na sifa yanayodhihiri katika limwengu zote. Shukrani kwa nuru hii, anagundua siri za ulimwengu. Katika chumba cha chini ya ardhi giza hupotea na vitu huonekana kwa macho taa zinapowashwa. Vivyo hivyo, nuru ya Imani na uongofu hudhihiri baada ya mtu kutumia utashi wake anapokuwa katika giza la ukafiri na upotovu inaangaza  ulimwengu wote. Kinachoangaza ulimwengu, huangaza ulimwengu na kuonesha siri ya kila kitu ni Imani na uongofu; Mfanyaji halisi anayeifanya Imani na uongofu kufika katika moyo ni Allah.

Kilichomaanishwa katika kauli Imani ni nuru ing’aayo ni kuwa na uwezo wa kuona majina ya Allah na sifa zake nyuma ya kila tukio na kuwa na uwezo wa kusoma sifa ya kweli na ya kiungu ya kila tukio.

Kwa mfano, umauti ni tukio kubwa kwa mwanaadamu. Kama tutautazama umauti kama nuru ing’aayo ya Imani, umauti utakuwa ni mwanzo wa ulimwengu wa milele na nukta ya mpito, na si kutokuwepo. Kama tutautazama kupitia miwani nyeusi za ukafiri, umauti ni tukio baya na la kutisha lenye kumtenganisha mwanadamu kutokana na vipenzi vyake milele na kutupa katika uwanja wa kutokuwepo. Mtazamo huu wenye kung’ara wa Imani unaonesha uhalisia na sura nzuri ya matukio yote. Hili ndilo lililokusudiwa na kauli Imani ni nuru ing’aayo na kwamba ni yenye maana. Kuna matukio mengi kama umauti ambayo mwanaadamu hawezi kufahamu kupitia akili yake.


8-) Je haki ya Allah inawafaa Waislamu tu; au ni pia inawafaa wasio-Waislamu?

Haki ya Allah inamfaa kila mtu, kama Muislamu au hapana. Allah ameharamisha dhuluma na uonevu kwa watu bila ya kujalisha dini yao. Inawezekana kwa Allah, anayeharamisha dhuluma ukandamizaji, Awakandamize watu kwa kuacha haki?

Imesisitizwa na ibara wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja. Katika aya ifuatayo: Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja.(Fussilat, 41/46) kuwa hakuna atakayedhulumiwa na kwa hiyo watu wote watatendewa haki bila ya kujalisha dini yao.

Kuna aya nyingi kuhusu jambo hilo. Aya mbili zinazowaambia makafiri moja kwa moja ni kama ifuatavyo:

Anaye geuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuungua. (Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yako. Na hakika Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja. (Hajj, 9-10)

Aya ifuatayo inaeleza kuwa hakuna amali, ndogo au kubwa, itakayopotea na kuwa kila amali itakuwa na malipo au adhabu: “Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona! Na anaye tenda chembe ya uovu atauona! (az-Zilzal, 99/7-8)

"Dharra" iliyotajwa katika aya inamaanisha mdudu mdogo sana au chembe inayoweza kuonekana katika mwangaza wa jua tu. Kinachomaanishwa hapa ni kueleza jukumu la mwanadamu kwenye kitu kidogo kabisa ambacho akili ya kibinadamu inaweza kuvutiwa nacho. Lengo halisi ni kueleza kuwa amali ndogo kabisa njema au mbaya haitapotea katika macho ya Allah.