Je, inawezekana kupata shuhuda za Utume wa Mtume Muhammad (S.A.W) katika Biblia, Taurati na Zaburi?

The Answer

Dear Brother / Sister,

Shuhuda za Utume wa Hadhrat Muhammad (S.A.W) katika Biblia iliyogeuzwageuzwa.

Ni muhimu sana kwamba tumeiita Biblia kuwa “imegeuzwageuzwa” katika kichwa cha habari. Neno imegeuzwageuzwa linamaanisha kuwa imepotoswa na kubadilishwa. Shuhuda zote tutakazozileta hapa zinamshuhudia Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo zimeondolewa kwa umakini kutoka katika Biblia na kwa hivyo zimegeuzwageuzwa. Licha ya kazi makini na ya uangalifu ya mchakato wa kugeuzageuza kwa kuondoa kila aya iliyoeleza habari ya Mtume Muhammad (S.A.W) kutoka katika Biblia, kumebakia shuhuda nyingi sana. Kama kuna ishara nyingi sana za Mtume (S.A.W) katika Biblia iliyogeuzwageuzwa, basi kuna ishhara ngapi zilizomo katika Biblia halisi aliyoshushiwa Yesu (AS)? Hebu tafakari hilo!

Ugeuzaji walioufanya Wakristo na Wayahudi katika vitabu vyao hususani uondoaji wa aya zilizoeleza habari za Mtume Muhammad (S.A.W) umetajwa katika Qur’an kama ifuatavyo:

Basi ole wao wanao andika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyo andika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayo yachuma. (al-Baqara, 2/79)

Enyi Watu wa Kitabu! Amekwisha kujieni Mtume wetu anaye kufichulieni mengi mliyo kuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anaye samehe mengi. Bila shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinacho bainisha. .―” (al-Maida, 5/15)

Qur’an inatueleza kuwa Wakristo wameficha habari nyingi sana alizofunuliwa Yesu (AS). Baadhi ya sehemu za habari hizo ni maneno katika Biblia kuhusu kuja Mtume Muhammad (S.A.W). Katika sehemu hii, tutachanganua maneno yanayosu kuja Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyomo katika Biblia.

1. Yesu alisema;Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Periklito (Msaidizi) mwingine, ili akae nanyi hata milele.” (Yohana 14:16,17)

2. Yesu alisema;Lakini huyo Periklito (Msaidizi), ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. (Yohana 14: 26)

3. Yesu alisema; Na sasa nimewaambia kabla halijatokea (Periklito), kusudi litakapotokea mpate kuamini. (Yohana 14: 29)

4. Yesu alisema;Lakini ajapo huyo Msaidizi (Periklito), nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia …” (Yohana 15: 26)

5. Yesu alisema;Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi (Periklito) hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. (Yohana 16: 7)

6. Yesu alisema; “…Lakini Msaidizi (Periklito) atakapokuja, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. (Yohana 16: 13)

7. Yesu alisema; “…Yeye (Periklito) atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.(Yohana 16: 14)

Neno la asili la misemo ya mshabaha ya Kibiblia iliyooneshwa hapo juu kama Periklito na Mtume Yesu (S.A.W) kupewa habari njema ni “Munhamenna” katika lugha ya Sham (Ki-Syria) na “Periklytos” kwa Kigiriki. Kisawe cha neno hilo kwa Kiarabu ni “Ahmad”.

Maneno ya Kigiriki ya Periklytos wa Biblia, yaani, “Ahmad” yameoneshwa kuwa ni “Briklitus” katika baadhi ya vyanzo. Kwani “Ahmad” (S.A.W) ni jina la Mtume Muhammad (S.A.W), imeelezwa na Qur’an kuwa jina Lake ni “Ahmad” katika Biblia. (Angalia. Saff, 61/6)

Na pia sifa zote zilizotajwa hapo juu anazo Mtume Muhammad (S.A.W) peke yake. Basi, ni Mtume Muhammad (S.A.W) ndiye aliyetajwa kuwa mtu aliyesubiriwa katika Biblia na ikatolewa habari njema kumhusu yeye.

Licha ya hivyo, neno “Periklito” limeelezwa katika ufafanuzi wa Kibiblia kuwa ni "mtu sahihi atakayepambanua ukweli na uwongo"; yaani, ni jina la mtu atakayewaongoza wanadamu kwenye ukweli baada ya Yesu (AS). Je, yupo yeyote asiyekuwa Hadhrat Muhammad (S.A.W) aliyefanya kazi hiyo zaidi yake aoneshwe duniani?

8. Yesu alisema;Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi (Periklito) hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.” (Yohana 16: 7)

Ni nani asiyekuwa Hadhrat Muhammad (S.A.W) aliyepo duniani na akawapa wanadamu faraja ya kweli? Ndiyo, ni Mtume (S.A.W) anayemwokoa mwanadamu kutokana na adhabu ya kifo na kuwapa faraja halisi.

9. Yesu alisema;Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. (Yohana 14: 30)

10. Yesu alisema; “…Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. (Yohana 16:8)

Baada ya Mtume Yesu (AS), ni nani aliyekuja asiyekuwa Mtume Muhammad (S.A.W) kama mkuu wa dunia na akapambanua haki na batili na kuwaonesha wanadamu njia ya kweli? Na, ni nani anayestahiki kupewa cheo cha “kiongozi wa dunia” asiyekuwa yeye? Na, ni mtume gani baada ya Hadhrat Dawud (AS) asiyekuwa Mtume Muhammad (S.A.W) aliyeeneza dini yake kutoka magharibi mpaka mashariki na akaweka mfumo wa kodi katika nchi na kupata ushindi nyoyoni mwa masultani na sehemu moja ya tano ya wanadamu wakimsifu kwa swala na kumtukuza kila siku? Ni nani asiyekuwa Hadhrat Muhammad (S.A.W) anayeweza kuoneshwa kama mtu mmoja tu aliyeyafanya hayo yote? Kwa hivyo, maneno yaliyotumika kwa ajili ya mtu baada ya Yesu (AS) katika Biblia kuwa ni “mtawala wa wa dunia” ni kwa Mtume Muhammad (S.A.W). Cheo chake mashuhuri ni “rehema ya ulimwengu”.

11 “Ushuhuda wa Yohana Mbatizaji ni kama ifuatavyo; Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nani basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La!” (Yohana 1:20-21)

Mtume Yohana (Yahya) aliulizwa maswali matatu na majibu yake kwa maswali yote matatu yalikuwa ya kukana:

a. Je, wewe ni Kristo, yaani, Yesu?

b. U Eliya wewe?

c. Wewe u nabii yule?

Hivyo, mitume watatu tofauti wametajwa katika Biblia ya Yohana. Hao ni Yesu (AS), Eliya na Mtume Muhammad (S.A.W)!

Kinachofahamika kutokana na maneno hayo ni kwamba; “Nabii yule” ni tofauti na Yesu (AS). Kwa hivyo, ni nani mtu huyo aliyefunuliwa kwa watu aliyoyasikia kutoka kwa Mungu na ambaye hakuwa hai wakati wa Mtume Yesu na aliyetajwa kuwa ni “Nabii yule” asiyekuwa Mtume Yesu? Kwa hakika ni; Mtume Muhammad (S.A.W). Kwani hakuna mwingine ghairi ya Mtume Muhammad anayeweza kuoneshwa kama aliyefuatia baada ya Yesu (AS) ambaye amefanya kazi ya Utume na kupata nafasi kubwa katika historia.

12. Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua. (Mathayo 7:15-20)

Hakuna sehemu yoyote ya Biblia inayosema kuwa Hakuna mtume baada ya Yesu (AS). Hata hivyo, sifa ifuatayo imewekwa ili kumtambua anayedai kuwa ni mtume:

 “Mtawatambua kwa matunda yao mumjue mwongo na mkweli…”

Kusingekuwa na mtume yeyote baada ya Yesu (AS), angetoa jibu fupi na la wazi wazi kama hivi: “Hakutakuwa na mtume yeyote baada yangu, Atakayedai utume baada yangu, kwa hakika ni mwongo.” Kwa hivyo, mbinu ya Yesu (AS) ya kumtambua mtume mwongo na mkweli ni ushahidi unaotosha wa kuja mtume mwingine baada ya Yesu.

Suala la kuja mtume baada ya Yesu (AS) pia linatosha kwa ajili ya Utume wa Mtume Muhammad (S.A.W) kwa sababu baada ya Yesu (AS), matokeo yenye manufaa ya kuunda jamii zilizomwamini Mungu, kumtegemea Mungu, kumpenda Mungu na kuacha kuabudu sanamu kulifanikiwa tu katika dini iliyoletwa na Mtume Muhammad (S.A.W).

13. Yesu (AS) anakuja Jerusalem. Anaanza kuhubiri kila siku. Hata hivyo, watu mashuhuri, wakuu wa nchi na viongozi wa kidini walitaka kumuua. Yesu (AS) anawapa ujumbe ufuatao:

“Ikiwa hamwamini ukweli huu, Mungu atakuleteeni juu yenu taifa litakaloamini na kuishi kwa mujibu wao …”

Katika mojawapo ya mafundisho yake, anaeleza mfano unaoelezwa hapa chini na ukweli wake kwa wakuu wa nchi;

Mfano wa Mmiliki ardhi (Mathayo 21:33-46; Marko 12:1-12; Luka 20:9-19)

Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara. Akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima?”

Wakamjibu Yesu kama ifuatavyo:

Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.”

Yesu akawauliza:

Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; naye yeyote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki.” (Mathayo 21:43)

Mkuu wa makuhani na Mafarisayo waliposikia mithali yake, walitambua kuwa alikuwa anazungumza habari zao.

Wakataka kumkamata, lakini waliogopa mkusanyiko, kwa sababu mkusanyiko ulimzingatia kuwa ni mtume.

 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake …”

 “Jiwe” lililotajwa katika sentensi hizo kwa hakika ni Mtume Muhammad (S.A.W) na watu watakaopewa mali ya Mungu ni ummah (jumuia) wa Kiislamu … Juhudi za wanazuoni wa Kikristo za kutafsiri “jiwe” kuwa ni Yesu (AS) ni bure.

a. Kwa hakika inafahamika kutokana na sentensi hizo kuwa mtu aliyeelezwa kwa taswira ya jiwe atakuwa tofauti na Yesu (AS) ambaye wengine wamedai kuwa ni mwana wa Mungu. (Allah atukinge dhidi ya hilo).

b. Kwa mujibu wa madai yao, Yesu (AS) aliuliwa na Wayahudi. Haifai kuuliza mantiki ya jiwe kuwaangukia juu yao kwa kuwa anayeangukiwa atapondekapondeka?

c. Yesu (AS) alisema katika Biblia ya Yohana, 12:47; Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu…” kwani hili ni kinyume cha utendaji wa “jiwe” kama ilivyoelezwa hapo juu kwa sababu kwa mujibu wa maneno ya Biblia, anayeangukia juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika, na atakayeangukiwa nalo atapondekapondeka.”

d. Zaburi, inaeleza kuwa inastaajabisha kuwa jiwe limekuwa jiwe la mingi kwa maneno, “…nalo ni ajabu machoni petu.” Kwa mujibu wa madai ya Wakristo, Daud (AS) alimheshimu sana Yesu (AS) mpaka –Alah atuepushie hilo- akawa anadhani kuwa Yesu ni Mungu. Basi kwa nini anaona ajabu kuwa Yesu ni jiwe la mingi? Kwa hivyo, mtu huyo lazima asiwe Yesu (AS) na utume wake lazima uwe wa kustaajabisha. Ukweli nyuma ya hilo ni kama ifuatavyo: Kwa kuwa wana wa Israil hawakutokana na Hadhrat Hajar na hawatokani na familia hiyo, wanaona kuwa Wana wa Ismail kuwa wako sawa nao na kwa hakika hakutokea mtume yeyote kutoka katika familia ya Ismail (AS) inawezekana ndio sababu ya kukanganyika kwao.

e. Mtume Muhammad (S.A.W) ambaye ukweli wake na kustahiki kwake kumethibitishwa na shuhuda nyingi, amesema yafuatayo katika hadithi kuwa jiwe hilo ni yeye mwenyewe:

“Tashbihi ya Mitume kabla yangu na mimi ni kama jengo lililojengwa vizuri sana lakini halina jiwe la msingi. Watu walioliangalia walivutiwa sana kwa uzuri wake; hata hivyo, walistaajabu kuhusu kutokuwepo jiwe la msingi. Hapa jengo hilo limekamilishwa nami na Utume unaishia kwangu.” (1)

14. Katika Biblia, kumeelezwa habari za Mtume atakayekuja na atakayekuwa mkuu wa ulimwengu kuwa ni “mwenye Sayf na fimbo.” (2) Neno la Kiarabu Sayf hapa linamaanisha upanga. Kwa hivyo, Mtume ana wajibu wa kupigana Jihad. Kwa hivyo, mtu huyu hawezi kuwa Yesu (AS) kwa sababu hakuteuliwa kufanya Jihad na Hakupigana vita. “Mwenye upanga” anaweza kuwa ni Mtume Muhammad (S.A.W) peke yake. Kwa kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) na ummah Wake aliteuliwa kupigana Jihad. Licha ya hivyo, Mtume Muhammad ana fimbo na alikuwa akitembea nayo.

15. Na tena, Mtume atakayekuja baadaye ametajwa kuwa ni “Sahib-ut Taj” (mwenye taji). (3) Hili pia ni jambo lake pekee Mtume Muhammad (S.A.W). Maana ya Taj ni kilemba alichokuwa akijizungushia kichwani. Hapo kale, watu waliokuwa wakivaa kilemba (vazi la kichwani) miongoni mwa mataifa walikuwa ni Waarabu. Kwa hivyo, ‘Sahib-ut Taj’ aliyetajwa katika Biblia kwa hakika inamaanisha ni Mtume Muhammad (S.A.W).

SWALI: Kwa nini kwamba ilhali mitume wengine wanabashiri kuja kwa Muhammad (S.A.W), Yesu (A.S) anafanya hivyo kikamilifu na katika namna ya habari njema?

JIBU: Kwa sababu Ahmad (S.A.W) alimtetea Yesu (S.A.W) dhidi ya madai na kashfa za kutisha za Wayahudi, na ameokoa dini yake dhidi ya kupotoshwa. Zaidi ya hivyo, mbele ya udhia wa Shari‘a za Wana wa Israil, ambao hawakumtambua Yesu, alikuja na Shari‘a iliyoadilishwa ambayo ilikuwa nyepesi, yenye kuenea kote, na iliyoziba mapungufu ya Shari‘a ya Yesu’. Kutokana na sababu hizo, Yesu mara nyingi alitoa habari njema kuwa "mtawala wa dunia" atakuja!

[1]Sahihu’l-Bukhari, IV, 162- 163
[2]Nabhani, Hujjatullah ala’l-Alamin, 99, 114.
[3] Nabhani, Hujjatullah ala’l-Alamin, 113,114; Ali al-Qari, Sharhu’sh-Shifa, 1:739.

Shuhuda za Utume wa Hadhrat Muhammad (S.A.W) katika Taurati Iliyogeuzwageuzwa.

Qur’an inasema kuwa Wayahudi walikiuzageuza kitabu kitukufu cha dini yao, Taurati, kwa kubadilisha sehemu za maneno yake na maana zake. Hiyo ndiyo sababu juu ya ishara zilizomhusu Mtume Muhammad (S.A.W) ndizo zilizokusudiwa kugeuzwageuzwa na kubadilishwa na Wayahudi. Watu wa kitabu kitukufu, waliobadilisha maana halisi za maneno, walileta ugumu wa kufahamu ishara za maelezo ya Mtume Muhammad (S.A.W).

Aya zinazoashiria jambo hilo kutoka katika Qur’an ni kama ifuatavyo:

Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno kuyatoa mahala pake, na husema: Tumesikia na tumeasi…” (an-Nisa, 4/46)

Wao huyabadilisha maneno kutoka pahala pake. Wanasema: Mkipewa haya basi yashikeni, na msipo pewa haya tahadharini …” (al-Maida, 5/41)

Sasa tuangalie maneno ya Taurati yanayomwashiria Mtume Muhammad (S.A.W):

1. Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, “Ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu; nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema Bwana wa majeshi.” (Agano la Kale Haggai 2:6-7)

Habari njema za kuja kwake na neno la "Himada" katika maandiko ya asili ya Taurati yanatokana na mzizi wa jina Muhammad kwa Kiarabu na herufi za maneno Ahmad kuwa ni “Ha, Mim na Dal” na hayo kwa kawaida yana maana moja. Kwa hivyo, neno linaloleta maana ya jina la Mtume Muhammad (S.A.W) limetajwa pamoja na tukio kubwa sana litakalotokea baadaye kwa mujibu wa maneno ya aya hiyo.

Kwa hivyo, lipi linaloweza kuwa kubwa zaidi ya ujio wa Mtume Muhammad (S.A.W), aliyeeneza habari ya kuwepo Mungu kwa mabilioni ya watu baada ya Agano la Kale? Kwa hiyo aya hii ya Taurati inaeleza habari za Mtume Muhammad (S.A.W) na ushindi wa Uislamu duniani kote, ambao ni jambo kubwa sana na tukufu.

2. Sehemu ya 42 ya Isaya ya Agano la Kale inaeleza ukweli kuhusu Mtume Muhammad (S.A.W) na kuja kwake… Hebu kwanza tusome sehemu inayohusiana nayo ya Agano la Kale na kisha tuchanganue maneno hayo, ambayo yapo katika Taurati:

Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mungu Bwana anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda; yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye roho wao waendao ndani yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa. Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu. Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Na sifa zake tokea mwisho wa dunia; Ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo, Na visiwa, nao wakaao humo. Jangwa na miji yake na ipaze sauti zao, Vijiji vinavyokaliwa na Kedari; Na waimbe wenyeji wa Sela, Wapige kelele toka vilele vya milima.

Kuna ulinganifu baina ya maneno yaliyomo katika Isaya ya Agano la Kale sehemu ya 42, na Mtume Muhammad (S.A.W). Maneno ya mambo hayo yaliyobashiriwa pia ni muhimu sana. Kwa hivyo, habari hiyo njema haikufunuliwa katika enzi za Musa (AS) au hata kabla yake. Hayo yatatokea kweli baadaye… Habari njema zilizoelezwa hapa ni Mtume Muhammad (S.A.W) na hebu tuone hayo kwa kuchanganua neno moja baada ya jingine:

a. “Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu.” (Agano la Kale 42:1)

Sentensi hii ya Agano la Kale inamwashiria kikamilifu Mtume Muhammad (S.A.W). Kwa kuwa Mungu alimsaidia, alimridhia na alimteua miongoni mwa wanadamu. Licha ya hivyo, Mungu alimtuma kwake Jibril (AS) (Malaika mkuu) na kuweka haki miongoni mwa mataifa pamoja naye. Kwa hivyo, sifa tano za mtu huyo zilizotolewa habari njema katika maneno hayo anazo. Sentensi hii ya Taurati inatoa habari njema kikamilifu za Mtume Muhammad (S.A.W) kwa maneno yake yote.

b. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli…” (Agano la Kale 42:2-3)

Maneno hayo, yaliyomo katika Taurati, yanaeleza kuhusu maadili ya juu ya Mtume Muhammad (S.A.W). Wakati Qur’an inaeleza sifa za Mtume Muhammad kwa maneno “Na wewe uko katika tabia bora kabisa” (1), Taurati imeeleza hilo kama ilivyooneshwa hapo juu. Kwa hivyo, mtu ambaye habari njema zinatolewa atakuwa ni mwenye maadili ya juu. Mtume Muhammad (S.A.W) ana maadili hayo ya juu sana na anakubalika kwa kila mtu.

c. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake…” (Agano la Kale 42:4)

Maneno hayo ya Taurati pia yanafahamisha habari za Mtume Muhammad (S.A.W). Kwa kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) alitawala ardhi alipokuwa hai na akahifadhi haki. Na kamwe hakukosa ujasiri wake. Hata pindi alipoteremshiwa aya, “Allah atakulinda dhidi ya watu (yaani fitina)” (2), aliwaondoa walinzi waliokuwa wakisubiri mbele ya hema lake na akawaambia; “Sasa Allah atanilinda, hamna haja ya kusubiria hapa.” (3) Watu na mataifa ambao walichoka mateso na dhuluma walimngojea mtu huyu. Kwa hivyo, maneno hayo yanafahamisha habari za ujasiri wa Mtume Muhammad (S.A.W), kuhifadhi kwake haki na watu wa pwani kumsubiri; kwa mantiki hii, imeashiria na hata kutoa maelezo kumhusu Mtume Muhammad (S.A.W).

d. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa…” (Agano la Kale 42:6)

Mtu ambaye habari njema zilitolewa kumhusu yeye katika Taurati ilisemekana kuwa amehifadhiwa na Mungu na kwa sababu hii, katika hali ngumu sana na hata katika nyakati ambapo kunusurika ilishindikana, alihifadhiwa na kufika salama kama ilivyoandikwa katika historia. Hata wakati wa kuhama, pindi uwezekano wa kukamatwa na washirikina ulipokaribia sana pangoni walipojihifadhi na pindi sahibu yake mwaminifu, Abu Bakr (RA), alikuwa akimlilia, alimweleza rafiki yake kuhusu kuwepo ulinzi imara wa  kiungu kwa kusema “Usihofu, Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi.” (4) katika kila awamu ya maisha ya Mtume (S.A.W), ulinzi huu wa kiungu ulionekana. Wale wanaoyajua maisha ya Mtume watalifahamu hilo vyema zaidi.

Licha ya hivyo, Mtume Muhammad (S.A.W) aliwafanya watu wawe wema baina yao. Uhasama wa damu ulikomeshwa na maadui wakawa marafiki waaminifu, shukrani zimwendee … na tena mataifa yalipata njia ya kweli, shukrani zimfikie na kwa kweli alikuwa chanzo cha nuru. Kwa hivyo, mtu ambaye habari zake njema zimetolewa ana sifa tatu katika Taurati: I. Mungu anamlinda, II. Atakuwa vyema na watu, III. Atakuwa kiongozi wa mataifa; hizo ni sifa zinazojulikana kwa kila mtu.

e. kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa…” (Agano la Kale 42:7)

Maneno hayo ya Taurati pia yanafahamisha habari za Mtume Muhammad (S.A.W). Kwa kuwa nyoyo butu na akili zenye maradhi ziliponywa, shukrani zimwendee yeye. Kwa msaada wake, nafsi zimekombolewa kutokakatika utumwa wa shari na wale wanaoishi katika giza la ushirikina wameifikia nuru ya tawhid (kumpwekesha Mungu).

f. Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu…” (Agano la Kale 42:8)

Maneno hayo ya Taurati ni muhimu. Kwa kuwa, kwa aya hii, Mungu anaeleza kuwa mtu kuhusu huyo ambaye habari zake njema zimeelezwa atauvunja ushirikina. Mapambano makubwa zaidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) yalikuwa dhidi ya washirikina na alipopata ushindi wa mji wa Makka, jambo la kwanza kabisa alilolifanya lilikuwa ni kuyavunja masanamu.

Licha ya hivyo, katika aya hii, Mungu anasema, “hataruhusu kusifiwa masanamu” Mtume Muhammad (S.A.W) aliifanya kazi hiyo pamoja na kutamka maneno “Alhamdulillah”, alieleza kuwa kila sifa njema ni kwa Mungu. Kwa hivyo, mtu ambaye habari zake njema zinaelezwa ni Mtume Muhammad (S.A.W) kwa sababu Mtume Muhammad (S.A.W) alitimiza kwa mafanikio kazi ya mtu kuhusu ambaye habari zake njema zimeelezwa.

g. Jangwa na miji yake na ipaze sauti zao, Vijiji vinavyokaliwa na Kedari; Na waimbe wenyeji wa Sela, Wapige kelele toka vilele vya milima. (Agano la Kale 42:11)

Maneno hayo ya Taurati pia yanafahamisha habari za Mtume Muhammad (S.A.W). Kwa kuwa, Mtume Muhammad (S.A.W) alikuwa mwanachama wa jumuia iliyotokana na wajukuu wa Kadar, ambaye alikuwa mwana wa Ismail (S.A.W), mwana wa Abraham (AS). Kwa hivyo, maneno hayo yanaashiria mababu wa Mtume Muhammad (S.A.W).

Kwa kifupi, Sehemu hizo za Agano la Kale zinalingana kikamilifu na Mtume Muhammad (S.A.W). Licha ya hivyo, katika muendelezo wa sehemu hii ya Agano la Kale, aya ya 17, kufedheheshwa kwa washirikina ni muhimu kwa sababu ufedheheshwaji huo ulifanywa na Mtume Muhammad (S.A.W). Ndiyo, pamoja na uchambuzi wa kina zaidi, mtu anaweza kukuta ishara nyingi zaidi katika Agano la Kale. Kwa hivyo, kama zilivyo sayansi nyingi kuanzia taaluma ya maisha ya kiinitete (embriolojia) mpaka unajimu, kutoka jiolojia mpaka elimukale (akiolojia) zinathibitisha kinachosemwa na Qur’an, ishara za Agano la Kale zinathibitisha utume wake Mtume Muhammad (S.A.W).

3. Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. (Agano la Kale, kitabu kitukufu cha Kumbu Kumbu la Torati, 18:18)

4. Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi. Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake. Naam, na manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena, walihubiri habari za siku hizi. (Agano Jipya, Matendo 3:22-23)

Sasa hebu tuchanganue sentensi hizi mbili zilizochukuliwa kutoka katika Biblia:

a. Hotuba ya Hadhrat Musa (AS) kama “ndugu zako” kwa Wana wa Israil, waliokuwa wanatokana na mbari ya Ishaq (AS), ambaye alikuwa mwana wa Hadhrat Ibrahim (AS), ni ishara wa wajukuu wa Hadhrat Ismail (AS) ambaye alikuwa ni kaka yake Hadhrat Ishaq (AS), yaani, kwa wana wa Ismail. Mtume aliyetokana na wana wa Ismail ni Mtume Muhammad (S.A.W) peke yake kwa sababu Mtume Muhammad (S.A.W) peke yake ndiye aliyetokana na mbari ya Ismail. Hadhrat Joshua (AS) na Yesu (AS) hawakutokana na wajukuu wa mbari ya Hadhrat Ismail bali walitokana na wana wa Israil.

b. Usemi “mtume kama mimi”, Hadhrat Musa (AS) alimkusudia Mtume Muhammad (S.A.W). Kwa kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) ndiye aliyeshabihiana na Hadhrat Musa mpaka sifa ishirini kama vile jihad, sheria na kanuni alizoweka, adhabu aliyoweka na utii wa jumuia kwake… lakini si Hadhrat Joshua au Yesu (AS).

c. Maneno katika aya, “Nitatia maneno yangu katika kinywa chake” ni ishara ya hali ya kutokujua kusoma na kuandika ya Mtume Muhammad (S.A.W) na ingawa hakujua kusoma na kuandika, alihifadhi neno la Mungu kiurahisi na aliwasomea watu. Habari hii ilidhihirika kweli sawa sawa na ilivyosemwa.

Na tunataka kuonesha maneno yaliyomo katika aya za 18 na 19 za Agano la Kale, kitabu kitukufu cha Kumbu Kumbu la Torati: katika sentensi hizo, kumesisitizwa kuwa “mtume huyo anazungumza neno la Bwana wake”. Sifa mojawapo muhimu ya Qur’an aliyoteremshiwa Mtume Muhammad (S.A.W) ni kuwa, surah 113 kati ya 114 zinaanza na “Basmala” yaani “B-ismi-llahi r-rahmani r-rahim” ("Kwa Jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu"). Licha ya hivyo, Mtume Muhammad (S.A.W) alianza kusoma aya za Quran na kila kitu kwa Basmala na aliunasihi ummah wake kufanya hivyo. Hivyo, mtu ambaye habari zake njema zilielezwa katika Agano la Kale na yeye kuelezwa kuwa ni mwenye kuanza mambo kwa jina la Mwenyezi Mungu ni Mtume Muhammad (S.A.W).

5. Bwana alitoka Sinai, Akawaondokea kutoka Seiri; Aliangaza katika kilima cha Parani, Akaja Meribath-Kadeshi na watukutu elfu kumi. Upande wake wa kuume Palikuwa na sheria ya moto-moto kwao.” (Agano la Kale, kitabu kitukufu cha Kumbu Kumbu la Torati, 33:2)

a. Katika maneno haya ya Taurati: “Alitoka Sinai” ni ishara inayomhusu Hadhrat Musa (AS) na ufunuo wa kiungu wa amri kwake; kwa upande mwingine, Akawaondokea kutoka Seiri ni ishara inayomhusu Yesu (AS) na ufunuo of Biblia kwake, na hatimaye Aliangaza katika kilima cha Parani ni a ishara kwa ajili ya Mtume Muhammad kuwa atatokea Makka. Kwa kuwa Paran hutamkwa Faran kwa lugha ya Kiarabu na Faran ni katika majina ya zamani ya Makka.

Licha ya hivyo, sentensi zinazosema kuwa Hadhrat Ismail anaishi katika jangwa la Paran kutoka katika Agano la Kale pia ni ushahidi wa hilo. Kwa kuwa Hadhrat Ismail (AS) alikuwa akiishi Makka. Kwa hivyo, Paran ni Makka kwa ishara ya Agano la Kale. Kwenye maneno ya Taurati, Mungu anaeleza kuwa Aliangaza katika kilima cha Parani. Ni nani anayeweza kuwa aliangaza hapo asiyekuwa Mtume Muhammad (S.A.W)?

b. Kinachomaanishwa kwa maneno mtukufu katika maneno yaliyomo katika maneno “alikuja pamoja na watukufu elfu kumi” ni Ahl al-Bayt wa Mtume Muhammad na swahaba zake. Katika kipindi kifupi sana, jumuia hii tukufu ilifikia mpaka idadi ya watu elfu kumi na hata mamia ya maelfu.

c. Maneno Upande wake wa kuume Palikuwa na sheria ya moto-moto kwao yanasimama kwa ajili ya jihad na pia ni ishara kuwa mitume wa baadaye wana jukumu la Jihad. Mtume Muhammad (S.A.W) na jumuia yake wanawajibika na jihad; kwa hivyo, mtu aliyeashiriwa katika maneno husika yanahakikisha kuwa mtu huyo ni Mtume Muhammad (S.A.W). Kwa hivyo, maneno hayo ya Taurati yanafahamisha habari za Mtume Muhammad (S.A.W) kwa alama za mara tatu.

6. Mungu akamwambia Ibrahimu, “Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa huku akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana.”

“Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.” (Mwanzo 21, 12-21)

Katika sehemu hii ya Taurati, kuna maelezo kuwa taifa litaundwa kutokana na mwana wa Hadhrat Hajar. Taifa hilo ni Mtume Muhammad (S.A.W) na ummah wa Kiislamu. Hakuna mitume wengine waliokuja kutokana na wajukuu wa Hadhrat Ismail isipokuwa Mtume Muhammad (S.A.W).

7. “Kwa hakika Mungu alimwambia Ibrahim kuwa Hajar - mama yake Isma‘il- atazaa watoto. Atatokea mtoto katika wanaye ambaye mkono wake utakuwa juu ya watu wote, na mkono wa watu wote utafunguliwa juu yake kwa utukufu.” (Agano la Kale, Mwanzo, 17)

Maneno hayo ya Taurati pia yanafahamisha habari za Mtume Muhammad (S.A.W). kama tulivyoeleza hapo awali, hakuna mitume wowote maarufu na mashuhuri waliotokana na wajukuu wa Ismail (AS), ambaye alikuwa mwana wa Hajar isipokuwa Mtume Muhammad (S.A.W).

8. “Musa alisema: “Ewe Mola Mlezi! Kwa hakika nimekuta katika Taurati jumuia bora itakayoibuka kwa manufaa ya wanadamu, itakayoamrisha mema na kukataza maovu, na itakayowamini Mungu. Naomba hiyo iwe Jumuia yangu!” Mungu akasema: “Hiyo ni jumuia ya Muhammad…” (Agano la Kale, Isaya, 42)

Jina Muhammad limetajwa kuwa ni Mushaffah, Munhamanna, na Himyata, katika namna ya majina ya Assyrian kwa Kihebrania, katika vitabu vya kimbinguni. Jina Muhammad katika hali yake ya asili lilikuwepo katika sehemu chache. Na hizo chache ziligeuzwageuzwa na Wayahudi. Licha ya hivyo, sentensi alizotamka Musa katika Taurati zinazoeleza jumuia aliyoiona ni za kuvutia sana.

Musa alipoeleza sifa za jumuia hiyo, alisema, “Hao ni watu bora zaidi, iliyotokea katika historia ya wanadamu, kuamrishana mema, kukatazana maovu, na kumwamini Allah.” Maneno hayo hayo yametumika katika aya ya 110 ya sura of Aal-i Imran katika Quran:

Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu.

Kama inavyoonekana, Upo upatanifu kamili baina ya maneno ya Musa katika Taurati na katika Quran. Upatanifu huu unathibitisha kuwa jumuia hiyo aliyoiona Musa ilikuwa ummah wa Muhammad.

9. “Katika siku za mwisho, ya kwamba mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima...mataifa yote watakwenda, kila moja kwa jina la mungu wake, na sisi tutakwenda kwa jina la Bwana... (Agano la Kale, Micah 4 verses 1, 2, 5)

Sentensi hiyo ya Taurati inaeleza waziwazi mlima mtukufu zaidi miongoni mwa milima, na takbira na ibada za mahujaji zinazotokea duniani kote; yaani, “ummah wa Muhammad” unaojulikana kama “ummah uliorehemewa.”

10. Agano la Kale, Daniel, sura ya 2: katika sura hiyo, Nebukadneza, aliyepindua dola ya Assyria, aliyeutengeneza mji wa Babeli kuwa ni kituo na aliyetawala kwa miaka arobaini na tatu, ndoto aliyoota na Daniel, aliyefasiri ndoto yake wametajwa. Muhtasari wa kisa hicho ni kama ifuatavyo:

Daniel, aliyekuwa katika jela ya katili Nebukadneza, alimweleza mfalme kuhusu ndoto yake kabla Nebukadneza hajamsimulia Daniel ndoto yake. Mfalme alithibitisha alichosema kwa mshangao na akasema, “Hiyo ilikuwa ndoto, na sasa nifasirie.” Daniel alisema:

“Sanamu ni utawala wa duniani. Wewe ni kichwa chake.  Baada yenu, utainuka ufalme mwingine; unawakilishwa na shaba kwa kuwa ni dhaifu kwenu. Kisha, falme mbili zaidi zitakuja na kutanuka. Ufalme mwingine wa chuma utawavunjavunja wengine. Kisha, nafasi yake itachukuliwa na falme nyingine nyingi, nyingine imara na nyingine dhaifu; chuma na udongo haviwezi kuchanganyika pamoja; halikadhalika falme hizo hazitakaa pamoja na kuungana. Kisha, Mungu atazivunja falme hizo na kumpeleka sultan ambaye utawala wake utaendelea mpaka Siku ya Kiama; mtu huyo mtukufu atawapeleka watu kwenye furaha kamili duniani na ahera. Hiyo ndiyo tafsiri ya kutanuka kwa jiwe lililoanguka kutoka mbinguni katika ndoto yako na kuvunja sanamu vipande vipande.“

Sentensi hizo za Taurati, ambapo humo kumeelezwa ndoto zilizofasiriwa na Daniel, zinatufahamisha kuhusu mtu mtukufu atakayeendelea kuishi mpaka Siku ya Kiama pamoja na dini atakayoleta. Hakuna shaka kuwa mtu huyo ni Mtume wetu (s.a.w). Mtume (s.a.w) alivunja masanamu vipande vipande na kupata ushindi duniani kwa usultani yakinifu na nyoyo kwa usultani wa kiroho.

[1] al-Qalam, 68/4.
[2] al-Maida, 5/67.
[3] Tirmidhi, Tafsîr, 5/6.
[4] Abu Nuaym, Dalail, Juz. 2, uk. 328


Shuhuda za Utume wa Hadhrat Muhammad (S.A.W) katika Zaburi Iliyogeuzwageuzwa.

Zaburi, ambayo ni kitabu cha pili katika vitabu vya kiungu, imetajwa katika aya tatu tofauti za Qur’an tukufu. Aya hizo ni hizi zifuatazo:

Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyo wapelekea wahyi Nuhu na Manabii walio kuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi. (An-Nisa, 4/163)

Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo mbinguni na katika ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine; na Daudi tulimpa Zaburi..” (Al-Isra, 17/55)

Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema.(Al-Anbiya, 21/105)

Aya mbili za mwanzo katika hizo zinaeleza kuwa Zaburi, ambayo ni mojawapo ya vitabu vinne vya kiungu, alipewa Daud (AS) na aya ya tatu inaeleza kuwa Zaburi ilitumwa baada ya Taurati…

Sasa, tutaangalia katika sehemu za Zaburi, ambapo kuna ishara zinazomhusu Mtume Muhammad (S.A.W).

1. Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele. Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako. Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli na upole na haki Na mkono wako wa kuume Utakufundisha mambo ya kutisha. Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako; Imo mioyoni mwa adui za mfalme. Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma …” (Zaburi, 45:2-7)

Sasa, tuangalie jinsi maneno hayo ya Zaburi yanamkusudia dhahiri Mtume Muhammad (S.A.W):

a. “Wewe ni mbora zaidi katika watu…”

Mazuri ya dhahiri ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyojumuika juu ya kiwiliwili chake kitukufu na ambayo pia yanaashiria mazuri yake ya ndani hayapo kwa yeyote. Zaidi ya hivyo, Imam Qurtubi anasimulia kuwa uzuri wa Mtume Muhammad (S.A.W) haukujitokeza kikamilifu. Kama uzuri wake wa juu juu ungeweza kuonekana kikamilifu, maswahaba wasingemudu kumwangalia. (1)

Jabir bin Samura (RA) anasimulia; “Nilimwona Mtume Muhammad (S.A.W), ambaye alikuwa ni jua la ulimwengu katika usiku wa mbalamwezi. Alikuwa amevaa joho jekundu. Nilianza kuuangalia uso wake uliokuwa uking’aa na mwezi ili kujaribu kujua kipi kilikuwa kizuri zaidi. Ninaapa kwa Allah kuwa utukufu wa uso wa Mtume Muhammad (S.A.W), ambaye alikuwa karibu yangu, ulikuwa mzuri kuliko mwezi.” (2)

Hadhrat Aisha (RA) anaeleza uzuri wa Mtume (S.A.W) kwa maneno  yafuatayo: Wanawake walioona uzuri wa Hadhrat Yusuf (AS) walijikata vidole baada ya kujisahau; kama wangemwona Mtume Muhammad (S.A.W), wangejikata mikono yao.”

b. “Kazeni mapanga yenu juu ya mapaja yenu …”

Mtume Muhammad (S.A.W) anasema yafuatayo katika Hadithi yake mojawapo: “Nimetumwa pamoja na upanga katika kipindi kinachokaribiana na Siku ya Kiama…” (3) Aya hii ya Zaburi pia inaonesha kuwa Mtume atakayekuja anaitwa “Sahib as-Saif”; yaani, atakuwa mwenye upanga na atawajibika kupigana jihad. Na ummah wake pia unaitwa Sahib as-Saif; yaani, watawajibika kupigana jihad. Habari hizo za Zaburi zinaweza kuonekana katika maisha Mtume (S.A.W) na katika jumuia yake katika uhalisia wake.

c. “Kwa niaba ya ukweli, fedheha, na uadilifu. Uruhusu mkono wako wa kulia udhihirishe amali za kiuchamungu.”

Sentensi za Zaburi pia zimetaja habari za haki ya Mtume Muhammad (S.A.W). Kwa hakika, Mtume Muhammad (S.A.W) ni mwenye busara zaidi kati ya wanadamu. Yafuatayo yamesimuliwa: Mwanamke wa kabila la Mahzumi aliiba. Makuraishi hawakutaka mwanamke huyo, kutoka kabila tukufu aadhibiwe. Mtume Muhammad (S.A.W) alimpenda sana Usama bin Zayd. Walijua kuwa Mtume asingeumiza hisia zake. Kwa sababu hiyo, walimwomba Mtume asimwadhibu mwanamke huyo kwa kumweka Usama kama mhenga. Mtume (S.A.W) alimwambia Usama kama ifuatavyo:

“Wana wa Israil waliangamizwa kwa sababu tu walikuwa na upendeleo. Walikuwa wakiwaadhibu masikini kwa adhabu kali sana lakini hawakuwaadhibu matajiri na wenye ushawishi. Ninaapa kwa Allah kuwa kama binti yangu mwenyewe Fatima atatenda uhalifu huo, nitamwadhibu vivyo hivyo.” (4)

Mtume Muhammad (S.A.W) hakufanya ubaguzi wowote wa kidini pindi alipofanya maamuzi ya kisheria. Kama Myahudi alikuwa katika upande wa haki, Alimpa Myahudi huyo haki yake kwa kuichukua kutoka kwa Muislamu. Vitabu vya Sirah vimejaa visa vinavyohusu uadilifu wa kipekee wa Mtume.

c. “Mishale yako ina ncha kali. Mataifa yatakuangukieni chini yenu, kwa mishale katika moyo wa maadui wa mfalme …”

Ukweli wa habari hizi za Zaburi pia unaonekana katika maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W). Kwa kuwa Uajemi, Byzantina, India, China na nchi nyingine nyingi zilishindwa na watu wake wengi walisilimu na kuingia katika ummah wa Mtume Muhammad (S.A.W). Na maneno hayo ya Zaburi yanaelezwa katika aya za Qur’an kama ifuatavyo:

Mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na msafiri, ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu. Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.” (Al-Hashr, 59/7)

e. “Umewapenda walio wema, na kuuchukia walio uovu.”

Sentensi hii inafahamisha kuhusu sifa mbili za Mtume Muhammad (S.A.W) kama sifa hizo zilivyoelezwa katika Qur’an kama ifuatavyo:

Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao waumini, lakini wengi wao wapotovu.(Aal-e-Imran, 3/110)

2. Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako, Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote. Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu Katika vizazi vyote. Kwa hiyo mataifa watakushukuru Milele na milele.” (Zaburi 45:16-17)

Sentensi hizi za Zaburi pia zinamhusu Mtume Muhammad (S.A.W) kwa sababu, ingawa miaka 1400 imepita tangu kifo cha Mtume Muhammad (S.A.W), waumini wamekuwa wakisoma salawat kwa kusema “Swalli 'ala Muhammadin wa 'ala ali Muhammad…” hususani baada ya swala tano za kila siku kwa enzi nyingi. Kwani yupo mwingine anayetajwa sana kama Mtume Muhammad (S.A.W) juu ya ardhi? Kwa hakika hapana. Kwa hivyo, inawezekana kwamba mtu aliyetajwa katika Zaburi si Mtume Muhammad (S.A.W)?

3. Na awe na enzi toka bahari hata bahari, Toka Mto hata miisho ya dunia. Wakaao jangwani na wainame mbele zake; Adui zake na warambe mavumbi. Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi; Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa. Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie. Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, Na nafsi za wahitaji ataziokoa. Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu, Na damu yao ina thamani machoni pake. Basi na aishi; Na wampe dhahabu ya Sheba; Na wamwombee daima; Na kumbariki mchana kutwa. Na uwepo wingi wa nafaka Katika ardhi juu ya milima; Matunda yake na yawaye-waye kama Lebanoni, Na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi. Jina lake na lidumu milele, Pindi ling'aapo jua jina lake liwe na wazao; Mataifa yote na wajibariki katika yeye, Na kumwita heri. Na ahimidiwe Bwana, Mungu, Jina lake tukufu na lihimidiwe milele; Dunia yote na ijae utukufu wake!” (Zaburi 72, 2-19 muhtasari)

Mwenye kusikia sentensi za Zaburi atahakikisha kuwa zinamsifia Mtume (s.a.w). Sifa zote zilizotajwa katika aya hizo za Zaburi zipo kwa Mtume (s.a.w).

Mpaka katika sehemu hii ya somo letu, tumesoma baadhi ya sehemu zilizogeuzwa za Injili, Taurati na Zaburi zilizomwashiria Mtume (s.a.w). Tumehakikisha kabisa kuwa mbili jumlisha mbili ni sawa sawa na nne kuwa vitabu vya kimbinguni vinamtaja Muhammad (s.a.w) na kutoa habari njema kuwa atafika. Ingawa vitabu hivyo vya kimbinguni vimegeuzwageuzwa sana na hususani aya zinazomhusu Mtume (s.a.w) zilijaribiwa kubadilishwa na kuondoshwa, Hadhrat Muhammad (s.a.w) anang’aa sana kama jua katika vitabu vya kimbinguni vilivyopo.

[1] Peygamberimizin Şemaili, Prof.Dr. Ali Yardım, Damla Yayınları.
[2] Darimi, Muqaddima, 10.
[3] Tirmidhi Vol. 3 p. 213; Ahmad bin Hanbal V/218.
[4] Bukhari, Anbiya 54, Hudud 12; Muslim, Hudud 8, 9.

Maswali juu ya Uislamu

Author:
Maswali juu ya Uislamu
Subject Categories:
Read 8.853 times
In order to make a comment, please login or register