Ni lipi lengo na fikra kuu ya Quran? Quran ni kitabu cha namna gani?

The Answer

Dear Brother / Sister,

"QUR’AN ni Maandiko yaliyoteremshwa yenye muhtasari wa vitabu vitukufu vya Mitume wote, ambao nyakati zao zilikuwa tofauti kabisa, maandiko ya watawa wote, ambao njia zao zilikuwa ni tofauti kabisa, na kazi za wanazuoni wote watakatitfu zilikuwa ni tofauti kabisa, ambao njia zao zilikuwa ni tofauti kabisa. Sura zake sita ni nzuri sana na zimetakaswa mbali na giza la mashaka na hali ya kushuku; nukta yake ya kusaidia kwa hakika ni ufunuo wa kimbinguni na Neno la milele;  kusudio na lengo lake linajidhihirisha kuwa ni furaha ya milele; sura yake ya ndani ni dhahiri kuwa ni uongofu halisi; sura yake ya juu kimsingi ni nuru ya imani; sura yake ya chini ni ushahidi na uthibitisho usiopingika; sura yake ya juu inadhihirika wazi kuwa ni kuusalimisha moyo na utambuzi; sura yake ya kushoto inaonekana wazi kuwa ni kutiisha mantiki na akili; matunda yake hayabishaniwi kuwa ni Rehema ya Mwingi wa Rehema na ulimwengu wa Peponi; na daraja lake na kufaa kwake kiuhakika kumepokewa na malaika na wanadamu na majini." (Badiuzzaman Said Nursi, Sözler (Maneno))

Quran ni kitabu cha aina gani?

Umuhimu wa kuigeukia Quran na kuifanya iwe juu katika maisha yetu leo, ardhi inapovamiwa na fitina na vurugu, uko dhahiri. Kama watu wamejiingiza katika upuuzi na kutumia muda wao juu ya hilo, kama watarejea na kutii kazi za watu badala ya kitabu kitukufu cha Allah, kama wale wanaodai kuuwakilisha Uislamu wanawaita watu kwenye chama chao, dhehebu na kikundi badala ya Quran, kama Waislamu wanazingatia vitabu vilivyojaa ushirikina, na si Quran kuwa ni kitabu chao cha mwongozo, kama ummah umeiacha Quran kama ambavyo Mjumbe wa Allah analaumu katika aya ya 30 ya sura al-Furqan:

"Kisha Mjumbe atasema: ‘Ewe Mola wangu Mlezi! Kiukweli watu wangu wameifanya hii Qur'an kuwa ni kitu cha kipuuzi.'"

ikiwa Waislamu wako katika hali kama hiyo ya watu wa kitabu kitukufu na wanafikwa na mgogoro wa utambulisho unaoweza kuelezwa kuwa hauna nafasi ya kusimama juu yake na kutokusimama imara katika Sheria, Injili, na Quran kama inavyoelezwa katika aya ya 68 ya sura al-Maidah: 

"Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hamna lenu jambo mpaka muishike Taurati na Injili na yote mlio teremshiwa kutokana na Mola wenu Mlezi. Na hakika ulio teremshiwa wewe kutokana na Mola wako Mlezi yatawazidishia wengi katika wao uasi na ukafiri. Basi usiwasikitikie watu makafiri. '"

basi, umuhimu wa kuigeukia Quran, kuifahamu na kuisaidia unakuwa lazima. Ni muhimu kuijua vyema Quran, kuisoma na kuifahamu ili kuifanya itawale maisha yetu.

Kitabu cha Kipekee, Kisicho na Kifani na cha Aina Yake Kinachopita Viwango vya Kibinadamu:

Jambo la kwanza ambalo msomaji ambaye mara tu ndio amaeanza kusoma Quran anahitaji kukizingatia ni hiki: si kitabu kilichoandikwa na wanadamu na kimegawanyika katika sura kadhaa chini ya vichwa vya habari au kitabu chenye sehemu za utangulizi, mwili na hitimisho. Quran si kitabu cha fasihi au itikadi tulivyovizoea; si kitabu cha historia, unajimu, elimu-jamii au hata tiba; pia si kitabu cha dini ya Wayunani na Warumi wa zamani. Kinavuta nadhari kwenye masuala mengi yaliyo katika mawanda ya matawi ya sayansi yaliyotajwa hapo juu, lakini ni kitabu tofauti na cha kipekee kabisa kwa upande wa malengo, mtindo, lugha, mpangilio na mtindo wa kushughulikia mambo. Ni kitabu cha ajabu kisichoweza kupimwa na tawi lolote la sayansi; kama Mawdudi anavyoliweka wazi hilo, "ni kitabu pekee cha aina yake duniani". 

Quran haikuteremshwa ili kuwajulisha wasomaji wake kuhusu masuala kadhaa au kuwahamasisha kufanya utafiti wa kisayansi.  Hata hivyo, lengo lake la kipekee ni kuwafanya watu na majini, ambao wamewajibishwa kwa sababu wana akili na utashi, wapatet utambuzi wa utumishi kama inavyoelezwa katika aya ifuatayo:

"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. " (adh-Dhariyat, 51/56)

na kupata furaha kamili kote duniani na ahera. Quran si kitabu kisicho na lengo:

Wala si mzaha.” (at-Tariq, 86/14)

Ni mkusanyiko kamili wa vigezo na kaida zenye kubainisha ukweli mbali na uwongo, jema mbali na ovu na zuri mbali na baya.

Ni sifa ya kipekee kabisa ya Quran, ambayo lengo lake la kipekee ni uongofu na furaha ya wanadamu, kutumia mtindo unaoafikiana na lengo hilo, wakati mwigine kuiambia akili, wakati mwingine hisia, wakati mwingine dhamiri na wakati mwingine moyo wa msomaji wake, kuvuta nadhari kwenye mataifa yaliyopita, mbingu na ardhi, ufalme wa mimea na wanyama, ukweli mwingi wa kisaikolojia, kisosholojia, kifalsafa na kimaadili na kuwaomba wasomaji wake wafikirie juu ya masuala hayo.

Kwa hiyo, Quran inaonekana kana yenye utata na iliyovurugika kwa upande wa mambo inayoyashughulikia ingawa imepangika katika muundo wa sura na aya. Ni umuhimu wa mtindo wa kipekee wa Quran kuliendea jambo linaloonekana kutokuhusika huku ikishughulikia suala husika, kuzuia mambo mara kwa mara, kutaja ufumbuzi wa matatizo ya kiutendaji ya jamii hasa wakati wa hatua ya miaka –ishirini-na-mitatu ya kuteremshwa na matatizo ya wanadamu yaliyoenea kote kwa ujumla, kuwahimiza watu wafanye amali njema na kutii kanuni za kimaadili, kuwapa habari njema za Pepo, kuwaonya wasifanye amali mbaya na kuwaonya dhidi ya Jahanamu.

Quran inaposomwa tena na tena, inaonekana bora zaidi kiasi cha kuwepo mshikamano na msimamo miongoni mwa mada zake, maneno na dhana, ambapo hakuna sentensi inayotumika bila ya umuhimu na kwamba kitabu chote kimejikita juu ya lengo moja: kumfanya mwanadamu apate uongofu na furaha kamili. Kama Muhammad Asad anavyoliweka wazi hilo, "Kamwe hakuna kitabu chochote - ikiwemo Biblia – kimeenezwa kwa wengi, na kwa muda mrefu sana, jibu lenye kufahamika la swali hili, "Mwenendo wangu uwe vipi ili nipate maisha mema duniani na furaha katika maisha yajayo?"

Kitabu cha Kweli, Kamilifu, Kisicho na mikingamo, Kisichobadilishwa, Kimetumwa na Allah:

Hakuna shaka kuwa Quran ni kitabu cha kweli alichoteremshiwa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) kutoka kwa Allah, Mola Mlezi wa Ulimwengu." Quran hii haiwezi kusanifiwa au kuandikwa na yeyote isipokuwa Allah. Inathibitisha sehemu za kweli za ufunuo uliofikia mpaka leo hii na inaeleza ufunuo ambao bila ya shaka unatoka kwa Mola Mlezi wa ulimwengu kikamilifu: 

“Na haiwezekani Qur'ani hii kuwa imetungwa na haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Lakini hii inasadikisha yaliyo tangulia, na ni mfafanuo wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kutokana na Mola Mlezi wa viumbe vyote. " (Yunus, 10/37)

Quran inaeleza ukweli huu kuwa ni jibu la madai kama yafuatayo:

Haya si chochote ila ni uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine… Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha. " (al-Furqan, 25/4, 5),

"... Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini. Wala si kauli ya kuhani...." (al-Haaqqa, 69/41, 42)

na inawapa changamoto wale wote wenye kutoa kashfa za kipuuzi:

"Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli. Na mkitofanya - na wala hamtofanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe walio andaliwa hao wanao kanusha." (al-Baqara, 2/23, 24)

"Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao, isipo kuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli. " (Yunus, 10/38)

Mtu anayeiangalia Quran kwa umakini kwa hakika atagundua katika mtizamo wa kwanza kuwa haiwezi kuwa imeandikwa na mwanadamu. Haiwezekani kuona udhaifu wowote binafsi wa mtunzi unaoweza kuonekana katika kitabu au dondoo zozote zinazohusiana na masharti ya njia ya mawasilianao ambamo mtunzi anaishi. Mathalani, kama Abdullah Draz anavyoonesha kuwa Quran inaendelea kuwa juu ya sifa za kibinadamu kama vile jiografia na mbari; haitoi majina kamili ya watu na sehemu inazozitaja; inatoa mafunzo kwa ajili ya elimu ya ujumla ya watu kwa kuwataja. Jambo hili peke yake linatosha kuthibitisha kuwa Quran ni neno la Allah.

Licha ya hivyo, inawezekana kukuta baadhi ya makosa na dosari kutokana na uchunguzi wa kina hata katika kitabu kizuri kilichoandikwa na mwanadamu. Hakuna mtu yeyote anayeichunguza Quran kutokana na sababu mbalimbali kwa mamia ya miaka walioweza kukuta kosa hata dogo au ukinzani. Haiwezekani kukuta hali ya upogo au kosa katika Quran:

“Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo." (al-Kahf, 18/1)

Kitabu kitukufu cha Allah kinawapa watu changamoto kuhusu jambo hilo:

"Hebu hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi." (an-Nisa, 4/82)

Yeyote mwenye kuisoma Quran kwa kuzingatia na kujaribu kuifahamu ataiona kuwa si neno la mwanadamu lililotamkwa kwa utukizi na bila ya lengo lolote:

"Wala si mzaha." (at-Tariq, 86/14).

"Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake." (al-Baqara, 2/2)

“Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu kwa haki. Na wale walio khitilafiana katika Kitabu wamo katika upinzani ulio mbali na haki (lengo)." (al-Baqara, 2/176).

"Ni mfafanuo wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kutokana na Mola Mlezi wa viumbe vyote." (Yunus, 10/37; as-Sajda, 32/2; Yasin, 36/5; az-Zumar, 39/1)

Ni kitabu ambacho hata herufi yake moja haiwezi kubadilishwa na Allah, mwenye uwezo juu ya kila kitu, ameamua kukilinda. {6/115; 15/9}.

Ni Mwongozo Unaowapeleka Wanadamu kwenye Njia Sahihi na Nuru Inayowatoa Gizani Kuwapeleka katika Mwangaza:

Quran ni mwongozo wa wokovu kwa watu wote katika kila zama na mahali kwa ujumla. Ni mwongozo unaoonesha njia za majibu kwa waumini walio katika mgogoro na matatizo. Dhana ya uongofu (hidayah kwa Kiarabu) linalomaanisha njia ya kutokea kwa wale wasiojua mwelekeo wa kwenda jangwani linalingana na nafasi ya Quran kwa wanadamu wote.

Quran, inayoeleza kuwa mwanadamu yuko katika hasara kwa kuapa kwa kutumia istilahi zama {al-Asr, 1-2}, ni "mbinu ya wokovu" na "chelezao " kwa mwanadamu, ambaye ametatizika kutokana na migogoro ya kiroho, mmomonyoko wa kimaadili na matatizo ya kijamii katika siku zilizopita na hata leo.  

"Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa." (Ibrahim, 14/1)

Njia pekee ya ufumbuzi kwa ajili ya jumuia iliyopoteza fadhila zake na sifa nzuri na ambayo hali yao ya sasa na ijayo imekuwa na giza la kupata ustawi na furaha inaoneshwa katika kitabu kitukufu cha Allah kama ifuatavyo:

"… Bila shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinacho bainisha. Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye njia iliyo nyooka. " (al-Maida, 5/15, 16)

Itikadi za kibinadamu, zinazoletwa na madai kuwa watatatua matatizo hayo ya wanadamu, hupunguza matatizo hayo kwa majibu ya muda mfupi na yasiyokamilika; kwa upande mwingine, Quran analeta njia kamili za wokovu na za milele zinazofaa kwa kila zama na mahali. Quran inamfananisha mtu anayejaribu kutatua matatizo kwa majibu yaliyotolewa na wanadamu kuwa ni kama mtu asiyejiweza anayechukua hatua chache pindi radi inayong’aza macho inayoyapiga katikati ya giza na kisha anayesimama {2/20}. Quran inaongoza kwenye lililo sahihi zaidi. {17/9}. Kwani, ni ukweli mtupu {13/1; 17/105}.

Rehema, Ukarimu, Ponyo na Mwongozo kwa Wanadamu:

"Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini. Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya." (Yunus, 10/57-58)

Quran ni ponyo na faraja, na matokeo ni rehema, kwa namna zote za vurugu na matatizo ya kiroho. Nyoyo zilizopata weusi kwa sababu ya uchafu wa kiroho na madhambi na kuwa ngumu kwa kuugua maradhi {2/10; 6/43; 8/49} zinaweza kutakaswa, kulainishwa na kuponywa kwa Quran peke yake:

"Husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu." (az-Zumar, 39/23)

 “Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua." (ar-Rad, 13/28)

Hivyo, Quran inakuwa ponyo na rehema kwa ajili ya wale ambao nyoyo na akili zao zinavurugwa kutokana na hadaa za Kishetani. Nyoyo za watu wanaoondokewa na matatizo ya namna hiyo na maradhi zinaelimika na busara ya kuganga yajayo hufanya kazi.

"... hii (Qur'ani) ni hoja zinazo toka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu na rehema kwa watu wanao amini." (al-A'raf, 7/203; al-Jashiya, 45/20)

Quran ni aina ya kitabu kitukufu ambacho {6/155}, kama Swahaba Umar (ra) anavyoliweka wazi hilo, "Allah hufungua macho yaliyofumba, masikio yasiyosikia na nyoyo zilizofungwa kwa kutumia Qur’an."

Ushauri na Onyo Ambalo Huwafanya Watu Wawe na Ufahamu na Kuwajibika:

Jina mojawapo la Quran ni "dhikr", yaani, mawaidha; na jina jingine ni "tadhkira" yaani mwonyaji na mkumbushaji. Quran ni mkusanyiko wa mawaidha na maonyo yanayomfundisha na kumkumbusha mwanadamu juu ya majukumu yake na yanayomwongoza kwenye heri na ukweli:

“Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili." (Ibrahim, 14/52)

Quran inamfahamisha mwanadamu kuhusu majukumu yake kwa upande wake yeye mwenyewe, Mola wake Mlezi, watu wengine na maumbile. Inawafundisha wale wasiotambua majukumu yao na inawakumbusha wale wanaoyasahau majukumu yao. Inawaonya vikali wale wasiotimiza majukumu yao kwa makusudi. 

Kama, mshairi, As Mehmet Akif, anavyoliweka wazi hilo, Quran haikuteremshwa ili wasomewe wale wanaokufa au ili kuagua. Iliteremshwa ili kuwapa mawaidha watu walio hai, kuwakumbusha wale wasiozingatia ukweli na kuwaonya dhidi ya majanga duniani na ahera yanayoweza kuwakumba. Hivyo, hakuna udhuru ulioachwa kwa wale wasiozingatia maonyo na mawaidha. {36/5-6, 69-70; 6/155-157}.

"Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa wenye kughafilika." (Yasin, 36/5, 6)

"Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha." (Yasin, 36/69)

“Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri..." (Yasin, 36/70)

“Na hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa. Basi kifuateni, na mchenimngu, ili mrehemewe." (al-Anam, 6/155)

"Msije mkasema: Hakika mataifa mawili kabla yetu yameteremshiwa Kitabu; na sisi tulikuwa hatuna khabari ya waliyo kuwa wakiyasoma. Au mkasema: Lau kuwa tumeteremshiwa sisi Kitabu tungeli kuwa waongofu zaidi kuliko wao. Basi imekufikieni bayana kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu, na rehema. Basi nani aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye kanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa wanao jitenga na Ishara zetu adhabu kali kabisa kwa sababu ya kujitenga kwao.' (al-Anam, 6/156, 157)

Rejea Pekee kwa Ajili ya Waumini, Nyenzo Pekee na Kigezo Kinachopambanua Ukweli Mbali na Uongo:

Rejea kuu kwa kila Muislamu anayeuchagua Uislamu kuwa ni dini yake na anajisalimisha kwa Allah ni Quran. Atajifundisha kanuni za maisha zitakazomletea furaha duniani na ahera kutokana na Quran. Atajifundisha anachohitajika kuamini na anachohitajika kukataa, kipi ni chema na halali na kipi ni kiovu na haramu, anachotakiwa kufanya na anachotakiwa kukiepuka kutokana na Quran. Atautakasa moyo wake, kuimarisha kujisalimisha kwake kwa Allah na kuhuisha imani yake na msisimko wake pamoja nayo. {9/124; 16/102}

“Na inapo teremshwa Sura wapo miongoni mwao wasemao: Ni nani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia Imani? Ama wale walio amini inawazidishia Imani, nao wanafurahi. " (at-Tawba, 9/124)

"Sema: Ameiteremsha hii Roho takatifu kutokana na Mola wako Mlezi kwa haki, ili awathibitishe wale walio amini, na kuwa ni uwongofu, na ni bishara kwa Waislamu." (an-Nahl, 16/102)

Atajifundisha mazuri ya Peponi na kitisho cha mateso ya Jahanamu kutoka katika kitabu kitukufu cha Allah; Hivyo, atafanya jitihada ya kuendesha maisha bora na atatenda zaidi kwa umakini ili kuepuka madhambi na amali mbaya. Kwa kifupi, muumini atapata kila kitu kuhusu jinsi ya kufanya ili apate radhi za Allah kwa ujumla katika Quran:

Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu. (an-Nahl, 16/89)

Hata hivyo, mtu asihitimishe kutokana na aya hii kuwa Quran ni ensaiklopidia au kitabu cha sayansi. Si kitabu kinachotaja nadharia za muda mfupi za kisayansi; ni mwogozo wa maisha. Ni kitabu cha mwongozo kilichotumwa na Allah, aliyetuumba sisi na anayeyajua zaidi maumbile yetu kuliko sisi; kinatuonesha jinsi ya kutumia viwiliwili vyetu vya kupita katika dunia hii ya mpito:

Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini." (Yusuf, 12/111)

Quran ni neno sahihi la mwisho la Allah. Wanadamu, waliohutubiwa kwa njia ya ufunuo tangu Hadhrat Adam (as), mtu wa kwanza, ambaye Quran, ambayo ni hazina bora inayothibitisha yaliyo ya kweli katika mafundisho yaliyotangulia ya upwekeshaji  yaliyosahaulika, yaliyopotea au kubadilishwa na inayosahihisha makosa yaliyomo ndani mwao. Wanadamu wanaweza kujua kipi ni ukweli wa kiungu na kipi si sahihi na ushirikina, shukrani ziiendee Quran, ambayo ni "Furqan" (Kipambanuzi baina ya heri na shari).

Quran kwa hakika ni kipimo kwa ajili ya Waislamu. Akili ya Muislamu, mtizamo wa kidunia na mwenendo unapaswa uundwe na Quran. Anapaswa kuangalia kila kinachomjia kwa jina la elimu na utamaduni wa Kiislamu kwa utumia Quran, moja baada ya kingine; na anapaswa apambanue baina ya lililosahihi na lisilosahihi, la kweli na la kishirikina, lilo bora na lililobuniwa.

Isisahaulike kwamba fursa adhimu ya Uisilamu ni kwamba wafuasi wake wanayo Furqan, (mpambanuzi) kitabu ambacho hakijakumbwa na mabadiliko yoyote, kilichopo chini ya hifadhi ya Allah na kitakachobakia kuwa ni kigezo kisicho na doa kinachopambanua baina ya ukweli na uongo. Ni kitabu kisicho na kasoro hata chembe.

Waumini hufanya rejea kwenye Quran ili kujifundisha siri za dunia na ahera; pia hurejea kwenye Quran na sunnah bora ya Mjumbe wa Allah, ambaye ni Quran hai, kuhusu masuala wasiyoafikiana.

Kwa kifupi, Quran ni kitabu kitukufu cha rejea ambacho thamani yake kamwe haitapungua mpaka Siku ya Kiama kwa ajili ya waumini. Kitabu hiki cha hazina ndicho rejea pekee ambayo waumini watafanya rejea ili kutatua namna zote za matatizo ya kiroho yakiwemo masuala ambayo wao hawaafikiani.

Kitabu cha Vitendo na si Nadharia:

Quran si kitabu kinachoshughulikia baadhi ya mambo ya kihistoria, kijamii, kifalsafa na kimaadili kwa njia ya kinadharia. Hata hivyo, kinalenga katika kuweka jumuia iliyoundwa kwa maadili ya kidunia na kanuni za kiroho inazoziweka. Inalenga kwenye kuondoa kila kinachohusiana na ukosefu wa fadhila na shari na kuwafanya wanadamu wote wajisalimishe kwa Allah, yaani, Uislamu, kama ilivyobadili mojawapo kati ya jamii za kijinga zaidi duniani na kuwa jamii bora zaidi {2/193}; ni kitabu cha kimapinduzi. Quran iliteremshwa ili itekelezwe kivitendo na watu waitii.

"Fuateni mliyo teremshiwa kutoka kwa Mola Mlezi wenu, wala msifuate rafiki au walinzi wengine badala yake. Ni machache mnayo yakumbuka." (al-Araf, 7/3)

Kila anayeiamini Quran, kimsingi, Mtume (s.a.w), anaitii na kushikamana na kanuni ilizoziweka:

"Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa. " (az-Zukhruf, 43/43, 44)

Quran "ni kitabu kitukufu cha Allah ambacho hamtapotea kamwe kama mtashikamana nacho." {Ibn Majah} ni kamba imara ya Allah itakayokupelekeni kwenye mwangaza, ukomavu, na heshima kama mtaishikilia; Hakuna kulazimishana katika dini. Ukweli utajitokeza dhahiri mbali na uongo; mwenye kukataa Uovu na akamwamini Allah atakuwa amekamata kishikizo cha kutumainia, kisichovunjika.”

“Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua." (al-Baqara, 2/256); {al-Baqara, 2/256, 257; Aal-i Imran, 3/103}

“Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka." (Aal-i Imran, 3/103)

Jamii inayoshikamana na kamba ya Allah na kutii kanuni za ufunuo inakuwa na furaha duniani na ahera. Wale wanaoupa mgongo ukweli wa kiungu na kukiacha kitabu kitukufu cha Allah kwa kutokukitii watakosa furaha katika sehemu zote mbili za ulimwengu.

Kanuni za kimaadili, nasaha na mapendekezo yaliyo katika Quran yanakuwa muhimu yanapotekelezwa kivitendo. Mathalani, nasaha zifuatazo za kiungu hazitakuwa na manufaa yoyote kama hazitafanyika kivitendo:

“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya."

"
Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki..."

"
Wala msiyakaribie mali ya yatima..."

“na
timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa. (katika Siku ya Hesabu)."

"
Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa..."

"
Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa. (katika Siku ya Hesabu)."

"
Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima."

"
Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako Mlezi. " (al-Isra, 17/32-38)

Kitabu cha Wazi Wazi, Chenye Kufahamika, Kilichorahisishwa:

Kama inavyoonekana katika aya za 32-38 za sura ya al-Isra tulizozinukuu kama ni mfano hapo juu, aya za Quran zina kanuni zenye kutendeka zinazoweza kufahamika hata kwa jumuia yenye ujinga mwingi. Quran haina utatanishi, wala kutokufahamika, wala kitabu cha kale kinachoweza kufahamika kwa wataalamu, wanasayansi na maulamaa tu au chenye alama za siri zinazoweza kutafsiriwa nao peke yao. Hukaririwa mara kwa mara kwa ujumla mwanzoni mwa sura za Quran ambapo Quran na aya zake viko wazi na vyenye kufahamika.

Katika Quran, kila kitu kimeelezwa "kupitia mifano mbalimbali" {18/54; 20/113} na kwa kina {6/55, 56, 126; 41/2-3}. Quran imerahisishwa ili ifahamike kupitia sitiari na mifano:

"Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka?" (al-Qamar, 54/17, 22, 32, 40)

"Kwakuwa wale wa mwanzo waliohutubiwa na Quran hawakujua kusoma na kuandika, Shari'ah tukufu za Uislamu zilikuwa rahisi. Shari'ah iliteremshwa katika mfumo ambao ungefahamika na kutekelezwa kwa urahisi na wale wanaohutubiwa bila ya kuhitajika elimu yoyote au ubobezi. Kudai kinyume chake ni kinyume na msingi wa Shari'ah. Watu wa mwazo kuhutubiwa hawakujua kusoma na kuandika; kwa hivyo, shari'ah iliyoteremshwa ilikuwa nyepesi. Vinginevyo, wangesema, "Iko juu ya kiwango chetu; haifanani na maneno yetu; hayo ni maneno tusiyoyajua au kuyafahamu, n.k..." {41/44}.

Licha ya hivyo, Allah anaeleza, "Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo." {2/286}; "Wala (Allah) hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini" {22/78}. Kwa sababu za kiutekelezaji, Shari'ah ilibidi iteremshwe katika lugha na mtindo ambao ungeweza kufahamika kwa kila mtu." Shatibi

Quran imeelezewa kama ifuatavyo katika hadithi:

“Baadhi ya watu ni watu wa Allah. Mjumbe wa Allah alipoulizwa, 'Ni kina nani hao?', Alisema, 'Hao ni watu wa Quran; hao ni watu wa Allah na marafiki zao." (Tirmidhi)

"Rehema na wingi humiminikia mahali na malaika na utulivu huzingira mahali ambapo muumini anasoma Quran kwa unyoofu na kwa kutaka radhi za Allah." (Tirmidhi)

Harith al-Awar anasimulia: "Pindi tulipokuwa tunapita njia ya msikitini, niliwakuta watu wameacha kumtaja Allah na kuingia katika mazungumzo yasiyofaa. Kwa hivyo, nilimwendea Hadhrat Ali (ra) na kumwambia niliyoyaona.

Akaniuliza, 'Unasema kweli, ni hivyo?'

Nilipomhakikishia kuwa hivyo ndivyo ilivyokuwa, alisema: 'Nilimsikia Mjumbe wa Allah akisema,

"Tazama! Mfarakano utatokea! Hapohapo nikamuuliza: ‘Ni ipi njia ya kujinusru nao? Ewe Mjumbe wa Allah! Alijibu: Ni kutii kitabu kitukufu cha Allah.

Kina habari zote kuhusu yaliyowatokea jumuia za kabla yenu, habari za mifarakano na misukosuko itakayotokea baada yenu na ishara za Siku ya Kiama.

Pia ina hukumu kuhusu mambo yatakayotokea miongoni mwenu (kuhusu mambo kama vile imani-ukafiri, utii-uasi, kilichoruhusiwa-kilichokatazwa, n.k.). N
i kipambanuzi baina ya ukweli na uwongo.

Iko makini katika kila inachokitaja, Hakuna neno ndani mwake ambalo ni la kupita bure tu au la nje ya mada. Mwenye kuangukia katika upuuzi kwa kutokukizingatia na kutokutenda kulingana nacho, Allah atamwangamiza. Kama yeyote atatafuta uongofu mahali pengine Allah atamwacha apotee.

Ni kamba madhubuti ya Allah. Ni ukumbusho wa hekima, na ni njia iliyonyooka kabisa. Inahifadhi nafsi zinazoitii zisiharibiwe na upotovu na ndimi zenye kuisoma dhidi ya kutatizika. Wanazuoni wa Qur’an daima hutamani zaidi yaliyomo ndani mwake. Kukisoma mara kwa mara hakumchoshi msomaji wake; wala msomaji hapotezi ladha kwa kurudiarudia kukisoma. Mastaajabu yake makubwa yanayowashangaza wanadamu hayaishi kamwe.

Ni aina ya kitabu ambacho, pindi walipokisikia, majini iliwabidi wakiri kuwa, '
Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya ajabu. Kwa hakika Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini.' (Surah al-Majini, 72/1-2) Mwenye kukitamka, atakuwa anasema ukweli. Mwenye kutenda kulingana nacho atalipwa. Mwenye kuhukumu kulingana nacho, atakuwa mwadilifu. Mwenye kuwalingania watu kukiendea, atawaongoza kwenye njia iliyonyooka. Oh Awar! Jifundishe vyema maneno haya mzuri." (Tirmidhi)

Kwa muhtasari, Quran, “kitabu cha muujiza", kitakachokomesha siku za giza tunazoishi ndani mwake na matatizo na machungu tunayoumia na kitakachowaongoza wanadamu wote kwenye "furaha ya wote", kiko katika utumiaji wetu kama hazina isiyo na kifani. Tunachohitajika kufanya ni kusoma hii "mbinu ya wokovu" kwa macho maangalifu ili tupate majibu ya maswali ya leo na kuwa na nguvu na msisimko uliokuwepo katika siku za mwanzoni mwa Uislamu.

Nyenzo:

A. Yıldız-Ş. Özdemir, Kur'an Nedir, Nasıl Okunmalıdır, Pınar Yayınları.

Maswali juu ya Uislamu

Author:
Maswali juu ya Uislamu
Subject Categories:
Read 3.292 times
In order to make a comment, please login or register
MASWALI YENYE KUFANANA