Ni nini swala? Kwanini swala, ambayo inajumuisha matendo machache tu ni muhimu sana katika Uislamu?
Dear Brother / Sister,
Mwenyezi Mungu Mtukufu hahitajii chochote; Hahitaji ibada zetu vile vile. Ni sisi ndio tunaohitaji ibada. Ibada ni aina ya tiba kwa majeraha yetu ya kiroho. Ni chakula chetu cha roho na tiba kwa maradhi yetu ya moyo. Hivyo basi, sababu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutuagiza tufanye ibada ni kwa faida yetu. Wakati daktari anaposisitiza ushauri juu ya matumizi ya dawa kwa mgonjwa, hufanya hivyo kwa faida ya mgonjwa na si kwa faida yake. Ni upuuzi kumuambia daktari, “Kwanini unasisitiza matumizi ya dawa hii? Kwanini unaitaka hii?”; ni hivyo hivyo, itakuwa upuuzi na ukosefu wa fikra madhubuti kufikiri, “Kwanini Mwenyezi Mungu anatuamrisha tuabudu? Kwanini anataka ibada?”
Sababu ya kwanini Allah ameumba ulimwengu ni kuonesha ishara za majina yake na sifa zake na kuleta mambo mazuri yanayoakisi ishara na kazi zilizofanywa kwa usanii wa hali ya juu ili ipelekee kushuhudia utukufu wa uwepo Wake na watambue kwa urahisi viumbe vyenye utambuzi kama wanadamu.
Mwanadamu siku zote ameshughulishwa na mambo ya dunia; hivyo, haangalii maajabu ya Kiungu na akapata somo kutoka kwao kuhusiana na umoja wa Muumba, elimu yake isiyo mipaka, nguvu na hekima zake. Mtu anaweza akatafuta njia kwenda kwa msanii kutokana na Sanaa, na kwa mtoaji wa neema kupitia neema kwa kuachana tu na mambo ya dunia. Lakini njia pekee ya kuachana na mambo hayo ni kupitia swala.
Mwangaza, hewa, maji, chakula, ambavyo ni vyakula kwa ajili ya maisha ya kidunia na uwepo wa uhai wa kiwiliwili ni mambo muhimu; sawa na ibada hasa ya swala, ambayo ni mwangaza kwa akili, ni hewa kwa moyo na chakula cha roho, ni muhimu mno kwa mtu mwenye akili.
Swala, ambayo maana yake ni kutubu na kuomba msamaha, kutokana na makosa yetu kwa Allah, Ambaye ana ufalme wa milele kabla na baada kwa ulimwengu wote, ambae ametuumba tukiwa si chochote si lolote, ambae anatupa neema kwa maelfu, anayetuahidi maisha ya milele Peponi kwa wale watakao muheshimu, ambae tunamuhitaji kwa kila pumzi yetu na ambae ndie mfadhili wetu, swala ndio maelezo ya mwanadamu ya heshima kwa Mola wake. Si akili, moyo au dhamira inaweza kuruhusu dharau kwa Mwenyezi Mungu kwa kutokutekeleza swala.
Swala ni kama muhtasari wa ibada ambao unajumuisha nguzo zingine zote za Uislamu. Kwa mfano, mtu anayeswali vile vile hufanya aina ya Hija kwa kuelekea Qiblah; hufanya aina fulani ya funga kwa kutokula wala kunywa wakati wa swala; hufanya aina fulani ya Zaka kwa kuutoa muda wake ambao ndio mtaji wake wa maisha, kwa kutaja majina ya Allah. Kwa kuongezea, anapokuwa anaswali hufanya ibada ya viumbe vyengine ulimwenguni kwa kusimama kama miti na mimea, kwa kurukuu kama viumbe vyenye miguu minne na kusujuda kama wadudu wanaotambaa.
Sawa na hilo, baadhi ya malaika wanamuabudu Allah kwa kusimama muda wote, wengine wanaabudu kwa kurukuu na wengine kwa kusujudu muda wote. Mtu anaetekeleza swala tano hukamilisha ibada za malaika kwa kufanya kila kitendo kwa muda fulani; kwa mantiki kwamba, naye huwa kama malaika!
Swala ni ishara ya ibada ambayo ndio msingi mkuu wa dini ya Kiislamu. Maelezo yafuatayo yanapatikana kwenye hadithi: “Tofauti kubwa kati ya Muislamu na asiyekuwa Muislamu ni swala.” (Muslim, Iman, 134; Abu Dawud, Sunnah, 15; Tirmidhi, Iman, 9)
Kila mtu anayeingia anga la kiroho la Uislamu kwa misingi ya mkataba wa wa Imani anahitaji kupumua kwenye hewa hii ya ibada. Ni jukumu la kiraia kwa kila mtu ambae amekubali uraia wa kiroho wa Kiislamu la kutekeleza ibada ya swala. Roho, akili na dhamira vyote vina haki ya kufaidika na anga la kiroho la ibada. Ni ukatili wa hali ya juu kuvinyima vitu hivyo haki ya kuamiliana na Mola wao kwasababu tu eti nafsi haitaki.
Adhana inayosomwa mara tano kwa siku ni wito wa kusimama mbele ya Allah na ni kama amri ya kuwaita wanajeshi kukusanyika katika kambi za kijeshi za dunia kwa Mfalme wa milele. Mtu ambae hatotokea mara zote tano kwenye kambi za kijeshi huhesabika kama mtoro na huduma zake za kijeshi hufutwa; anapaswa aanze tena huduma hizo upya.
Hebu fikiria hali ya mtu ambae hakutokeza licha ya wito wa Allah mara tano kwa siku na hukimbia!
Swala ni mkusanyiko halisi. Wenye maana ya kupeleka shukurani kwa rafiki wa kweli anaetupa neema zisizohesabika.
Swala ni kisimamo cha kimya kimya kutambua ukubwa wa Muumba.
Swala ni kiunganisho kinachong’aa ambacho kinaunganisha ardhi na mbingu. Ni muhimu kwa milango ya fahamu kwa ambao wanahitaji mwangaza wa Amani ya kiroho hawana namna isipokuwa wakumbatie kiunganishi hichi.
Kutekeleza swala kwa jamaa ni muhimu sana. Swala ya jamaa huzingatiwa kama moja ya sherehe kubwa za kiibada katika Uislamu. Ukweli kwamba swala ya jamaa hupewa umuhimu mkubwa inaonesha kwamba dini hii tukufu ni dini ya umoja na hivyo basi tunatarajia umoja wa kudumu baina ya Waislamu.
Swala ya jamaa hupunguza utabaka unaotokana na familia na matabaka ya kijamii. Haijalishi aina ya familia, rangi, utaifa, Waislamu wote husimama kwenye hadhi sawa wakitekeleza ibada ya swala na wote huelekea Qibla kimoja, wakimuabudu Allah mmoja wote kwa pamoja kama mwili mmoja.
Swala ya jamaa ni njia nzuri ya kuunganisha jamii. Ni fursa nzuri kwa waumini kila mmoja kujua hali ya mwenzake.
Ikiwa mawe ya jengo fulani ni madhubuti, jengo pia litakuwa madhubuti. Ni hivyo hivyo, ikiwa kila mtu, ambae ni jiwe kwenye jengo la jamii, akiwa sawa na madhubuti kiroho na kimwili kupitia ibada ya swala, basi na jengo la jamii litakuwa sawa na madhubuti. Sharti la msingi kwenye kutengemaa huku baada ya Imani ni swala.
Zipo aya nyingi na hadithi zinazoelezea umuhimu wa swala. Chache katika hizo zimeelezewa hapa chini kutoa fikra:
“Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira na Sala. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.” (al-Baqara, 2/153)
Kwenye aya hii, imeoneshwa kwamba ni muhimu kujifunza kuwa na subira na kufaidika na utukufu wa swala ili kufaulu mitihani duniani. Kwa kweli, swala na subira ni mfano wa magurudumu ya mashine kila moja humsaidia mwenzake. Kutekeleza ibada ya swala mara tano kwa siku hupelekea uvumilivu. Hata hivyo, mtu ambae hutekeleza swala tano hujifunza kuwa mvumilivu kwa sababu maisha yake huyaweka kwenye nidhamu maalumu. Hii ni kuwa, swala humsaidia mtu kuwa mvumilivu na uvumilivu humsaidia kutekeleza ibada ya swala.
"…Na kwa hakika jambo hilo (la swala) ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu" (al-Baqara, 2/45)
Katika aya ya hapo juu, inasisitizwa kwamba kutekeleza ibada ya swala ina mnasaba wa moja kwa moja na kumjua Allah. Na ni jambo gumu kweli kwa wale waliyokosa elimu hii kuonesha subira kubwa inayohusu kutekeleza ibada ya swala.
Ulimwengu huu mkongwe umeshuhudia watu wengi waliopata kusema, “Niliswali kwa mwaka mmoja; nikagundua kuwa si jambo la kumalizika; kwa hiyo nikaachana nayo.”
“Zilindeni Sala, na hasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kunyenyekea.” (al-Baqara, 2/238)
“Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu” (al-Ankabut, 29/45)
“Hakika wamefanikiwa Waumini, Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao.” (al-Muuminun, 23/1-2)
Katika mkutano wa “Alastu bi rabbikum” [Mkutano ambao Allah aliwaita viumbe na akawauliza swali Je, Mimi si Mola wenu? Viumbe wakajibu “Wewe ni Mola wetu na hakuna ubishi kwenye hilo], ambao uko nje ya mipaka ya akili ya mwanadamu na ambao ni mkutano wa siri kwenye ulimwengu usiyoonekana, kila mmoja alisema “Ndio” kwa kupitia mifumo yao ya kiroho na ulimi wa hekima kupitia swali la Allah, “(Je, Mimi sio Mola wenu?) Swala ni ishara ambayo inathibitisha ahadi iliyotolewa katika ulimwengu usiyoonekana ndani ya ulimwengu wetu huu. Swala ni ngao kwa waumini.
Maswali juu ya Uislamu
