Ni yapi malengo ya vita ambavyo Mtume Muhammad (S.A.W.) amepigana?

The Answer

Dear Brother / Sister,

Ni ukweli unaojulikana kuwa sababu nyingi za vita hivi zinaweza kutajwa. Kwa mujibu wa tathmini yetu, vita vya mtume Muhammad (S.A.W.) vilitokana na sababu zifuatazo na hekima:

1. Ili kumfanya adui ahisi kwamba wanazo nguvu za kutosha za kupigana.

Baadhi ya vita vya mtume (S.A.W.), hususani vya sariyya ambavyo vilitokea kabla ya Vita vya Badr, vimelenga kuwaonesha washirikina na Wayahudi wa Madinah waliokuwa na uhasama dhidi ya Uisilamu na wafwasi wake, na washirikina wa Makkah waliokuwa wakisubiri fursa ya kuwashumbulia Waisilamu kuwa Waisilamu ni imara na kuweka eneo la uhuru kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Uisilamu na kuwalinda Waislamu dhidi ya mashambulizi. 1

Vita hivi vya sariyya ni mapambano yaliyofanyika ili kuonesha kuwepo kwa Waisilamu na nguvu yao na matokeo ya kuvivuka vizuizi katika njia ya tabligh. Utawala wa nguvu za kikatili wa wakati huo katika eneo hilo, kwa kumwona mwenye nguvu ndiye mwenye haki na kuwanyima wanyonge haki ya kuishi ulisababisha Mtume Muhammad (S.A.W.) kutuma makundi ya maaskari ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo. Vita vya sariyya vya Saif al-Bahr na Rabigh pamoja na Abwa, Buwat, Hamraul Asad na Badr ndogo vimeendeshwa kwa lengo hilo. 2

2. Kuzuia vyanzo vya kifedha vya mashambulizi.

Baadhi ya vita vya mtume (S.A.W.) vilipiganwa kwa lengo la kudhibiti njia za biashara ya washirikina wa Makkah na kuwadhoofisha kiuchumi kwa kuwa walianza kuliandaa jeshi ili kupigana na Mtume Muhammad (S.A.W.) na Waisilamu kwa kutumia bidhaa za Waisilamu walizolazimika kuziacha walipohama kutoka Makkah na kushikiliwa na washirikina hapo baadaye. Maisha ya kipekee ya washirikina wa Makkah yalikuwa ni biashara. Walinzi wa misafara waliokuwa na silaha waliopelekwa Damaskas walilazimika kufuatiliwa karibu na Madina ili wasiwadhuru Waisilamu. Kwa sababu hii, Mtume Muhammad (S.A.W.) aliandaa vita hivyo vilivyotajwa vya ghazwa na sariyya ili kuifuatilia misafara ya washirikina. 3

Kwa hakika, Vita vya Badr vilipiganwa kwa lengo la kuepusha maandalizi ya vita ambavyo wangeanzisha Makuraishi kwa manufaa waliyoyapata kutokana na misafara ya kibiahara. Vita vya Uhud viliandaliwa kwa pato lililotokana na msafara wa biashara ya Damaskas ya Abu Sufyan ili kulipiza kisasi kwa Mtume Muhammad (S.A.W.). 4

Vita vya sariyya vya Saiful-Bahr, Rabigh, Harar, Nahla, Qarda na Is, vilivyokuwa dhidi ya washirikina wa Makkah, ambao daima walikuwa wakiwatishia Waisilamu, vilikuwa ni nguvu fanisi dhidi ya nguvu kubwa-kubwa katika kujiandaa kwa ajili ya vita kama vile kufuatilia misafara ya kibiashara na kukata vyanzo vya kifedha. 5

3. Kujilinda dhidi ya mashambulizi.

Wakati mapigano yote ya Mtume Muhammad (S.A.W.) yalikuwa na sifa ya kijilinda kwa upande wa sababu zake na malengo yake makuu, idadi ya mapigano ya kujilinda kwa upande wa mikakati ni ndogo. Baadhi ya vita vya Mtume Muhammad (S.A.W.) vilitokea kutokana na mashambulizi ya adui ili kuwaondoa Waisilamu na mshikamano wao wa kikanda. Katika mazingira hayo, Mtume Muhammad (S.A.W.) alitumia haki yake ya kisheria ya kujilinda. Kwa kuwa Quran imeruhusu kupigana ili kujilinda panapo shambulizi 6 na imesisitizwa kuwa mapigano yanapaswa yapiganwe kwa kutegemea sababu halali za kisheria. 7

Kipindi cha mapambano kati ya vita vya Badr na Khandaq ni majaribio ya kujilinda dhidi ya washirikina wa Makka na Wayahudi wa Madina. 8 Umuhimu wa hatua za lazima za kujiinda hususani kwa Wayahdui/Wayahudi, ambao waliishi nao pamoja, unaweza kuonekana katika kipindi cha baadaye. Kwa hakika, kutokana na uhaini uliofanywa na kabila la Quraydha, Waisilamu wamepitia vipindi vya hatari wakati wa mapigano walipolazimika kuilinda Madina dhidi ya vikosi vyenye nguvu vya Ahzab, vilivyoundwa na washirikina wa Makkah na Wayahudi wa Khaybar. 9 Katika kipindi cha Madina, Mtume Muhammad (S.A.W.) alilazimishwa kupambana na sifa za kiadui za Wayahudi dhidi ya Waisilamu na alilazimika kuwa tayari dhidi ya mashambulizi yanayoweza kutokea. 10 Kwa sababu hii, mapigano ya Badr, Uhud na Khandaq yalikuwa ni mapigano makubwa ya kujilinda kwa upande wa kisheria na mkakati ambao umelenga kujilinda dhidi ya mashambulizi.

4. Ukusanyaji wa taarifa kuhusu adui.

Baadhi ya ghazwa na sariyya ya Mtume Muhammad (S.A.W.) zilitokea ili kukusanya taarifa dhidi ya maadui waliokuwa wakivizia fursa ya kushambulia wakati wowote ule. Waisilamu walilazimika kuwa makini muda wote dhidi ya maadui wa namna zote, hususani washirikina. Kwa sababu hizi, baada ya kuhakikisha usalama wa Madina, Mtume Muhammad (S.A.W.) alilenga kuwa na hadhari zaidi dhidi ya washirikina wa Makkah kwa kuweka mikataba na makabila jirani. Vita vya mwanzo vya sariyya viliendeshwa kwa lengo la kukusanya taarifa kuhusu adui, kupeleleza kiintelijensia na kudhibiti mazingira yao ya kisiasa na kiuchumi. 11

Doria na makachero walipelekwa kabla ya vita ili kupata taarifa. Kuwa na taarifa kuhusu hali halisi ya adui kupitia mapambano ya doria, inteligensia na njia nyengine kulikuwa na umuhimu mkubwa mno wa usalama wa Waisilamu. Kwa ajili hiyo, Waisilamu ambao walisumbuka kwa kuwa na nguvu yenye mipaka dhidi ya adui mpaka pale ushindi wa Makka ulipolazimishwa kupokea taarifa kuhusu nguvu ya ya adui ya mapigano iliyojumuisha mbinu zao za kupigana, pahala na kwenye mazingira yapi wangefanya hivyo. 12 vita vya sariyya vya Nahla, Dhu’l Qassa ya mwanzo, Wadi’l Qura’, Jinab ya pili, Hunayn, Abdullah ibn Rawaha na vita vya sariyya vya Khaybar vilitokea ili kuwa na taarifa kuhusu adui ambae angevurumisha mashambulizi ya kushtukiza.

5. Uvunjaji wa mikataba na kuwaadhibu wahaini

Uvunjaji wa mikataba unajenga uhalifu kwa mahusiano ya kimataifa. Kuvunja vipengele vya mikataba kwa upande wowote ule ilikuwa ndio sababu ya baadhi ya mapigano katika kipindi cha Mtume Muhammad (S.A.W.). Uvunjaji wa katiba ya Madina (hati ya Madina) pamoja na uvunjaji wa mkataba wa Hudaybiyyah, mikataba ambayo imefungwa na Mtume Muhammad (S.A.W.) baada ya Kuhama kumepelekea sababu kuu ya baadhi ya mapigano.

Mtume wa Allah (S.A.W.) mara zote alitimiza mikataba mbali mbali kikamilifu. Mfano bora kabisa wa hili ni huu hapa: Kwa mjibu wa ibara ya mkataba wa Hudaybiyyah, “Mtu anaposilimu akiwa Makka na akataka apate hifadhi Madina, madai yake hayo hayatokubaliwa na atarejeshwa kwao Makka.” Baada ya hatua ya utilianaji saini, Abu Jandal, aliyekuwa mwana wa ujumbe wa Makka, alimjia Mtume Muhammad (S.A.W) akiburura minyororo yake na kudai hifadhi kutoka kwake. Wakati Suhayl ibn Amr, aliyetia saini mkataba kwa niaba ya watu wa Makkah, alikataa dai lake kulitetea wazo kwamba makubaliano yalishapitishwa, Abu Jandal alilia sana, “Enyi Waisilamu! Mtanirejesha tena kwa hawa Makuraishi wanaotaka kunifanya niikane dini?” Huku haya yanatokea Mtume (S.A.W.) akasema, “Ewe Abu Jandal, kuwa na subira! Tarajia malipo yako kutoka kwa Allah. Allah atakauonesha wewe na mfano wako mlango. Tumeshaweka mkataba na Makuraish. Hii ni ahadi ya pande mbili kwa ajili ya Allah na hatuwezi kuivunja. 13

Tukio hili la kusikitisha ni mfano muhimu mno wa uaminifu wa Mtume (S.A.W.) kwa ibara za mkataba.

Kipindi cha mapigano ambayo yalianza baada ya Kuhama kilimalizika kwa mkataba wa Hudaybiyyah; hata hivyo, mkataba huu ulivunjwa na Makuraish. Kwa sababu hii, Mtume Muhammad (S.A.W.) alisonga mbele kuelekea Makka ili kuwafunza nidhamu. 14 Kama ilivyo kwa mapigano yaliyoendeshwa na washirikina, mapigano ya Mtume Muhammad (S.A.W.) yaliyoendeshwa dhidi ya makabila ya Kiyahudi yaliyopo Madina yaliendeshwa kwa masuala ya kisheria kama vile kuvunja kanuni za mkataba na kuungana na maadui dhidi ya masharti ya mkataba.

6. Kuadhibu Mavamizi na Uporaji

Uporaji wa wanyama waliotegemea malisho ya kiangazi waliomilikiwa na Mtume (S.A.W.) na Waisilamu na wengine kufa shahidi kwa wakati huo huo kulizusha kisingizio cha baadhi ya mapigano ya sariyya. Ni wajibu kupambana na watu waliozoea kuwashambulia Waisilamu kwa sababu tu ya imani zao pamoja na makabila yaliyoandaa mashambulizi haya. Ulinzi alioumarisha mtu ili kulinda mali yake na maisha yake katika shambulizi la uvamizi na uporaji linazingatiwa kuwa ni kujilinda. Upotevu wa mali na uhai wakati wa kujilinda hauhitaji adhabu yoyote kwa upande wa sheria za Kiisilamu. Mapigano ya vita vya sariyya ya Harar, Dhu’l Qassa ya pili, Tarif, wana wa Fazara, Ukl, Uranis na Mayfaa pamoja na mapigano ya ghazwa ya wana wa Quraydha, Safawan / Badr ya kwanza, Sawiq na Dumatu’l Jandal yametokea kutokana na uporaji wa mali za Waisilamu na Mtume (S.A.W.) na mashahidi wa baadhi ya Waisilamu wakati wa jaribio la uporaji huu na matukio mbalimbali yakiwemo mashambulizo hayo hayo.

7. Kumzuia Adui asiungwe mkono

Mtume Muhammad (S.A.W.) alikuwa na sifa ya amani na alikuwa muwazi kwenye makubaliano katika kila hatua ya maisha yake. Alifunga mikataba pamoja na makabila yenye dini tofauti-tofauti yaliyoishi Madina katika mazingira alipofurushwa kutoka ardhi ya kwao na kulazimishwa kuhama lakini hakuachwa katika amani hata huko Madina. Katika muundo huu, baadhi ya makubaliano yalifungwa pamoja na baadhi ya makabila kabla ya adui aliyekuwepo katika njia ya  biashara ya Makuraish ili kuwazuia wasiungane na adui na kuunda jukwaa la amani. 17 Mapigano ya ghazwa ya Abwa na Dhu’l-Ushayra yalitokea ili kuyayakinisha makubaliano ya amani. Mapambano ya Mtume wa Allah (S.A.W.) yanapaswa yazingatiwe kuwa ni juhudi za kumaliza migogoro kwa amani wakati wa zama za Madina, ambapo bado hakukuwa na vita vilivyopamba moto.

8. Uingiliaji kati wa Kijeshi uliofanywa pindi zilipopokelewa habari za shambulizi.

Sehemu muhimu ya vita vya ghazwa na sariyya vya Mtume Muhammad (S.A.W.) vilitokea kutokana na kupokea habari za shambulizi wakati mwingine kutoka kwa kabila moja na wakati mwingine mjumuiko wa makabila yaliyojipanga dhidi ya Mtume na Waisilamu kwa sababu tu ya imani yao. Sio kwamba mrejesho baada ya kupokea habari za njama ya kushambuliwa ungemaanisha kusalimu amri mbele ya adui. Mtume Muhammad (S.A.W.) alihama ili kuepuka pigo la kwanza ya shambulizi ambalo kwa hakika lilipangwa na adui. Wakati shambulizi la adui ndio sababu ya kisheria kwa ajili ya vita, mrejesho wake unazingatiwa kuwa ni sababu ya kisheria dhidi ya maandalizi ya mashambulizi hayo yaliyopokelewa na inteligensia. 18 Vita vifuatavyo vya ghazwa na misafara ya kijeshi ya Tabuk vilitokea kutokana na kupokea taarifa za njama za adui kutaka kushambulia; Dhul-Qassa ya kwanza, Qarqaratu’l- Kudr, Bahran, Dumatu’l Jandal, Muraysi, Wadi’l-Qura, Turaba, Najid / Hawazins, Mayfaa, Jinab, Dhatu’s-Thalathil, wana wa Bakr, Abdullah ibn Rawaha, Khaybar, Ghaba, mapigano ya sariyya ya Qutba ibn Amir pamoja na Ghatafan, Qatan, Dhatu’r-Riqa, Hunayn, Taif, Khaybar na mapigano ya vita vya ghazwa ya Fadak. Vita vingi vya ghazwa na sariyya itapozingatiwa, itaonekanwa kwamba vimetokea kutokana na kupokea habari ya shambulio.

9. Kuwasaidia Waisilamu wanaoteswa.

Viko vita vilivyokuwa na lengo la kukomesha shinikizo kwenye uhuru wa dini na imani lililowekwa na makabila fulani na dola kadhaa zilizowadhulumu na kuwatesa Waisilamu. Makabila na dola kadhaa zilizojawa na hisia za chuki dhidi ya Waisilamu walionesha chuki zao kila walipopata fursa. Chuki hii ilikuwa ikioneshwa kwa mtindo wa dhuluma na kuwatesa Waisilamu walioishi dola jengine wakiwa ni wachache.

Mwisilamu mmoja mmoja na jumuia kadhaa zilizodhulumiwa na walionyimwa uhuru wa kutekeleza imani na ibada ya dini yao wanabebeshwa jukumu kama hawatojaribu kukomesha dhuluma hii. 19

Na kwa nini basi isilazimike kupigana kwa ajili ya Allah na kwa wale, waliokuwa wanyonge, wanaotendewa vibaya (na kudhulumiwa)? – wanaume, wanawake, na watoto, ambao kilio chao ni: “Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anayetoka kwako.” 20

Aya ya hapo juu inaweza kutumiwa kuwa ni msingi kwa ajili ya kupigana kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaodhulumiwa. Ukweli kuwa Mtume (s.a.w.) alilisaidia kabila la Khuzaa baada ya ombi lao la kutaka msaada katika kipindi cha Amani ya Hudaybiyya 21 unaweza kutafsiriwa kuwa ni kutimiza amri ya aya hii. 22 Mapigano ya sariyya ya Bi’r al-Mauna na mapigano ya ghazwa ya Dumatul-Jandal yalikuwa ni uingiliaji wa kijeshi wa Mtume (s.a.w.) uliotokea ili kuwasaidia Waisilamu walioweko matesoni.

10. Kutokomeza vikwazo vinavyozuia tabligh (kufikisha ujumbe wa Uisilamu)

Kwa kuwa tabligh ni jukumu la msingi la Mtume (s.a.w.), lengo kuu ni kumtambulisha Allah duniani kote kwa njia ya amani. Jukumu la tabligh halikupuuzwa hata katika mazingira ya wakati ambapo adui aliwalazimisha Waisilamu kupigana. 23 Kama ulivyo umuhimu wa jukumu hili, Mtume (s.a.w.) alituma wajumbe wa tabligh kwa makabila na dola kadhaa kandokando ya Madinah. Wakati sababu iliyo nyuma ya mapigano ya ghazwa na sariyya yaliyodaiwa kutokea kutokana na tabligh yakichunguzwa, itaonekanwa kuwa yametokea kwa sababu ya wajumbe hao walilazimika kujihami walipokuwa wakishambuliwa. Kwa maneno mengine, vita vilitokea kwa sababu wanaolinganiwa hawakuukubali Uisilamu bali kwa kuwa waliwashambulia Waisilamu. Kwa hivyo, Mtume (s.a.w.) alipigana ili kutokomeza vikwazo vilivyozuia tabligh na sio kuwafanya watu kuukubali Uisilamu kwa mabavu.

Miongoni mwa mapigano ya sariyya ambayo Mjumbe wa Allah (s.a.w.) ameyapeleka kwa kusudi la kulingania Uisilamu ni Dhat al-Atlah chini ya uongozi wa Ka’b b. Umayr 24, Dhat ath-Thalathil yaliyoongozwa na Amr b. As 25, Dumatul-Jandal yaliyoongozwa na Abdurrahman b. Awf, Jazima yaliyoongozwa na Khalid b. Walid 26. Mapigano ya sariyya yaliyoongozwa na Ibn Abi’l Awja kwenda kwa Wana wa Sulaym kuwalingania Uisilamu lakini walisema, “Hatutaki wito wenu.” Kisha, waliwashambulia Waisilamu kwa kufyatua mishale yao na Waisilamu wote kufa mashahidi isipokuwa Ibn Abi’l Awja. 27

Wakati mwengine Mtume (s.a.w.) alituma wajumbe kwa baadhi ya makabila na madola wakati alipoombwa na wakati mwingine alipeleka wajumbe kwa kusudi la kufikisha ujumbe wa Uisilamu bila ya kuombwa kufanya hivyo. Baadhi ya wajumbe hawa ambao hawakuwa na lengo lolote isipokuwa ni kufikisha ujumbe wa Uisilamu walishambuliwa kwa kushtukiziwa na kufanyiwa uhaini; walikufa mashahidi. Mapigano ya sariyya yafuatayo yalishambuliwa na Waisilamu walioshiriki humo walikufa mashahidi: mapigano ya sariya ya Raji’, Bi’r al-Mauna, Wana wa Sulaym, Dhat al-Atlah, Dhat ath-Thalathil, Wana wa Jazima, Uman, Bahrayn na Dumatul-Jandal.

Yapo makabila yaliyodai wajumbe wa tabligh wakieleza kuwa wameshakuwa Waisilamu na kuahidi kuwa watawalinda wajumbe hao; hata hivyo, waliwashambulia kwa kuwashtukiza na wajumbe hao kufa mashahidi; mashambulizi haya yalisababisha kuzuka baadhi ya mapigano ya sariyya na ghazwa. Wajumbe ambao hawakuwa na jukumu jingine isipokuwa ni kuwajulisha watu kuhusu dini iliyoleta wokovu kwa utu walishambuliwa kihaini na kushtukiziwa. Mtume (s.a.w.) alipambana dhidi ya watu hao walioushambulia Uisilamu ili kuulinda Uisilamu. Mapigano ya ghazwa ya Dhat ar-Riqa na mapigano ya sariyya ya Jamum, Mayfaa, Wana wa Amir, Sayf al-Bahr ya Pili na Khaybar yalizushwa ili kuzuia mashambulizi dhidi ya wajumbe wa amani.  

11. Kuwaadhibu wale waliowatendea vibaya na kuwaua mabalozi

Mjumbe wa Allah alituma mabalozi kwa watawala wa nchi kadhaa katika ukanda husika baada ya Mkataba wa Hudaybiyya kwa kusudi la kuwalingania Uisilamu. Miongoni mwa watawala hao walijibu wito huo kwa vizuri; hata hivyo, wengine waliujibu kwa namna hasi/vibaya na kuwatusi mabalozi na Mtume (s.a.w.). 28
Baadhi ya mabalozi hawa waliotumwa kwa viongozi na watawala wa makabila na nchi mbalimbali ili kutimiza wajibu wa tabligh walitukanwa, kuuliwa au kushambuliwa. Hata hivyo, mabalozi na wajumbe walikuwa na dhamana ya uhai katika sheria ya kimataifa. 29 Kuwatusi, kuwashambulia na kuwauwa mabalozi waliokuwa na dhamana ya uhai ulikuwa ni uhalifu mkubwa mno. Mapigano ya sariyya ya Himsa, Wana wa Qurayt na Qurata na vikosi vya Muta yaliendeshwa kwa sababu hii.

12. Kujibu tangazo la vita lililotolewa na adui

Azimio la vita lililofanywa na adui ni moja ya sababu za Mtume (s.a.w.) kupigana. Kutokulijibu kabila au dola linaloendesha vita dhidi yako kutachochea uadui na kuwafanya wakushambulie kwa nguvu zaidi na kishupavu; kwa hivyo, ni lazima kujibu tangazo la vita lililotolewa na adui. Katika hali hiyo, kulijibu tangazo la vita kunazingatiwa ni kujilinda kwa sababu adui huyo anaonesha kuwa anakusudia khasa pindi anapotangaza vita. Wakati Mtume (s.a.w.) alipokalibiwa na azma hiyo na hatari ya kushambuliwa, alijibu tangazo hilo la vita. Mfano pekee wa vita vya namna hii ni mapigano ya Ghazwa ya Badr ndogo.

Wakati Mtume aliposhindwa na washirikina wa Makkah kwa namna fulani wakati wa Mapigano ya Uhud, alikubali pendekezo la Abu Sufyan, aliyempa changamoto iliyoegemea kwenye ufahari wa ushindi, kupigana tena karibu na viunga vya Badr mwaka uliofuata. 30 Kama ulivyo umuhimu wa kujibu azimio na kitisho cha vita kwa Makuraish, Mtume aliandaa jeshi na kwenda kwenye vikosi 31; hata hivyo, alipokwenda huko, hakukuwa na mtu. Abu Sufyan, aliyeketi nje ya Makkah na jeshi la watu elfu mbili, aliamua kurudi kabla ya kufika Badr kutokana na udhuru wa njaa. 32 Imefahamika wazi kuwa kikosi hiki kilitekeleza jukumu kutokana na tangazo la vita la Abu Sufyan.

Hitimisho

Inafahamika kutokana na somo hili, ambapo sababu za Mtume (s.a.w.) zimechunguzwa, kwamba mapigano yake na vita viliegemea kwenye sababu tofauti-tofauti. Kwa mujibu wa hayo, vita vyote vimeegemea kwenye sababu za kisheria; kwa hivyo, inaweza kuhitimishwa kuwa hakuna mapigano, vita au uingiliaji kati wa Mtume (s.a.w.) ambao si wa haki. Ikiwa sababu zote zitazingatiwa, itaonekana wazi kuwa Mtume (s.a.w.) hakushambulia kabila lolote au dola lolote kinyume na haki.

Ikiwa kanuni za Uisilamu, zinazotegemea Quran na Sunna, zimezingatiwa, itaonekanwa kuwa mahusiano kati ya mtu mmoja mmoja na dola mbalimbali yanategemea kanuni ya amani. Vita ni wajibu usiotakikana kuwa ni kitu cha mpito; vinaweza kutokea kuwa ni mapambano kwa ajili ya kuwa hai.

Kuvielezea kwa njia inayohusiana na leo hii, itaonekana kuwa sababu za vita vya Mtume (s.a.w.) ni za kisheria kama zimechunguzwa chini ya vigezo vinavyotumiwa kubainisha uhalali wa vita hapo kale na sasa.

Tanbihi

1. Khattab, Mahmud Shit, Komutan Peygamber Hz. Peygamber’in Askerî Dehası, kimefasiriwa na Ağırakça, Ahmed, İst., 1988, uk. 56.
2. Kwa maelezo zaidi kuhusu mapigano ya ghazwa na sariyya, tazama Nargül, Veysel, Kur’an ve Hz. Peygamber’in Uygulamaları Işığında Cihad, (Tasnifu Isiyochapishwa ya shahada ya Udaktari), Erzurum, 2005, uk. 111-217.
3. Ibn Hisham, Abu Muhammad Abdulmalik b. Hisham, as-Siratu’n-Nabawiyya, kilichochapishwa pamoja na uhakiki wa Mustafa Saka na marafiki, by., nd., II, 241-242, 245; Muslim, Sayd 17.
4. Ibn Sa’d, Muhammad, at-Tabaqatu’l-Kubra, Beirut, 1985, II, 37; Samhudi, Nuruddin Ali b. Ahmad, wafau’l-Wafa, Beirut, nd., I, 281. Pia tazama Ibnu’l-Athir, Abu’l-Hasan Ali b. Muhammad, al-Kamil fi’t-Tarikh, Beirut, 1965, II, 113, 116; Bukhari, Manaqib, 251, Maghazi, 2.
5. Tazama Hamidullah, Muhammad, İslam Peygamberi, kilichofasiriwa na Salih Tuğ, Ankara, 2003, II, 1036-1037.
6. al-Hajj, 22/38; al-Baqara, 2/190; ash-Shura, 42/41.
7. al-Baqara, 2/194.
8. Khattab, Komutan Peygamber, uk. 13.
9. Waqidi, Muhammad b. Umar, Kitabu’l-Maghazi, Chuo Kikuu cha Oxford, 1966, II, 459-460; Ibn Qayyim, Abu Abdillah Muhammad b. Abi Bakr, Zadu’l-Maad fi Hady-i Khayri’l-Ibad, Cairo, nd., III, 129-130.
10. al-Baqara, 2/91; Aal-i Imran, 3/183; Qasas, 28/48-50.
11. Ibn Hisham, I-II, 601, ff.; Hamidullah, İslam Peygamberi, I, 139.
12. Tazama Balazuri, Abu’l-Abbas Ahmad b. Yahya b. Jabir, Ansabu’l-Ashraf, Beirut, 1996, I, 383-384; Kattani, Abdulhay, at-Taratibu’l-Idariyya, Beirut, nd., I, 363.
13. Ibn Hisham, III-IV, 318; Bayhaqi, Ahmad b. Ali b. Husayn, as-Sunanu’l-Kubra, Hyderabad, 1344, Sunan, IX, 219-220.
14. Ibn Qayyim, Zadu’l-Maad, III, 290, 394.
15. Tazama Ibn Hisham, I-II, 501-504.
16. Ibn Sa’d, II, 28-29, 57-59, 74-78; Ibnu’l-Athir, II, 137-139; Suhayli, Abdurrahman b. Abdillah b. Ahmad, ar-Rawdu’l-Unf fi Tafsiri’s-Sirati’n-Nabawiyya li Ibn Hisham, Kairo, nd., II, 296; Samhudi, I, 277-278, 298.
17. al-Anfal, 8/58; at-Tawba, 9/12-13; Güner, Osman, Resûlullah’ın Ehl-i Kitap’la Münasebetleri, Ankara, 1997, p. 299.
18. al-Anfal, 8/58; at-Tawba, 9/12-13; Aal-i Imran, 3/146-147, 200.
19. al-Hajj, 22/39-40.
20. an-Nisa, 4/75.
21. Abu Yusuf, Yaqub b. Ibrahim, Kitabu’l-Haraj, Cairo, 1396, p. 230; Balazuri, Futuhu’l-Buldan, kimechapishwa pamoja na uhakiki wa Abdullah Anis at-Tabbaa’, Beirut, 1987, uk. 41.
22. Yaman, Ahmet, İslam Devletler Hukukunda Savaş, İstanbul, 1998, uk. 86-87.
23. Darimi, Siyar, 8.
24. Ibn Sa’d, II, 127-128.
25. Ibnu’l-Athir, II, 232.
26. Ibn Hisham, IV, 280-281.
27. Ibn Sa’d, II, 123.
28. Ibn Kathir, Ibn Kathir, Imaduddin Abu’l-Fida Ismail, al-Bidaya wa’n-Nihaya, Beirut, 1966, IV, 268 ff.
29. Shaybani, Muhammad b. Hasan, Sharhu Siyari’l-Kabir, (pamoja na ufafanuzi wa Sarakhsi), Beirut, 1997, II, 72; Turnagil, Ahmet Reşid, İslamiyet ve Milletler Hukuku, İstanbul, 1972, uk. 92-96.
30. Ibn Hisham, III, 100; Balazuri, Ansab, I, 417.
31. Tabari, Abu Jafar Muhammad b. Jarir, Tarikhu’t-Tabari Tarikhu’l-Umam wa’l-Muluk, Beirut, nd., III, 42; Ibn Hazm, Abu Muhammad Ali b. Ahmad, Jawamiu’s-Sira, kilichofasiriwa na M. Salih Arı, İstanbul, 2004, uk. 180-181.
32. Ibn Hisham, III, 220; Ibn Sa’d, II, 59-60.

Dk. Veysel Nargül

Maswali juu ya Uislamu

Author:
Maswali juu ya Uislamu
Subject Categories:
Read 1.106 times
In order to make a comment, please login or register
MASWALI YENYE KUFANANA