Qur’an imesalimika vipi dhidi ya kugeuzwageuzwa?
Dear Brother / Sister,
Qur’an, maandiko matakatifu ya Allah na hutuba Zake za kiungu kwa wanadamu, iliteremshwa aya baada ya aya na sura baada ya sura katika miaka 23. Mtume alikuwa akizisoma aya na sura alizoteremshiwa kwa kuwasomea maswahaba zake, na wao wakawa wanazihifadhi na baadhi yao walikuwa wakiziandika. Licha ya hivyo, Mtume alikuwa na waandishi wa ufunuo. Wao hususani walikuwa na kazi ya kuandika aya na sura zilizoteremshwa.
Mtume alijulishwa kupitia kwa Malaika mkuu Jibril kuhusu mahali pa kuwekwa aya na sura zilizoteremshwa, pamoja na mpangilio wake katika Qur’an, na kisha Mtume akawa anawaeleza waandishi kuhusu ufunuo na kuweza kufanyika yaliyokuwa muhimu kufanyika. Qur’an yote iliandikwa katika muda alioishi Mtume na ilipangwa kipi kiwekwe mahali gani. Zaidi ya hivyo, Jibril alikuwa akija katika kila mwezi wa Ramadhani na alikuwa akimsomea Mtume aya na sura zote zilizoshushwa tangu mwanzo. Katika mwezi wa Ramadhani wa kabla ya Mtume hajafariki, Jibril alikuja tena, na kwa wakati huu waliisoma Qur’an mara mbili. Awali, Jibril alisoma, na Mtume alisikiliza; na baada ya hapo, Mtume alisoma na Jibril alisikiliza. Hivyo, Qur’an ilichukua umbo lake a mwisho.
Hata hivyo, katika wakati wa uhai wa Mtume Qur’an ilikuwa bado haijakusanywa katika kitabu kimoja. Ilikuwa imesambaa miongoni mwa maswahaba kama kurasa na ilihifadhiwa na maswahaba wengi. Hata hivyo, ilifahamika dhahiri na kwa hakika namna ya mpangilio wake wote.
Hatimaye, kutokana na kulazimika, katika wakati wa Halifa Abu Bakr, iliundwa kamati kutokana na waandishi wa ufunuo na mahafidhi hodari chini ya uongozi wa Zayd bin Thabit. Kamati hiyo iliteuliwa kwa ajili ya kuikusanya Qur’an katika kitabu kimoja. Kila swahaba alikuja na kukabidhi kurasa alizokuwa nazo za Qur’an. Kutokana na mgawanyo wa kazivya mahafidhi na waandishi wa ufunuo, kurasa, sura na aya zilipangwa kama alivyoeleza Mtume. Hivyo, Qur’an ilipangiliwa katika kitabu kimoja kilichoitwa Mushaf.
Matokeo yake, Qur’an imesalimika mbali na hali ya kusahaulika, kupotea, kugeuzwa au kubadiliswa, kwa kuwa iliandikwa sawa sawa na ilivyoteremsha kwa Mtume.
Kutokana na ulazima, katika wakati wa Halifa Uthman ibn Affan zilichapishwa nakala nyingi kutokana na kitabu hiki na kupelekwa katika sehemu mbalimbali. Nakala za Qur’an zilizopo sasa zinatokana na Qur’an hii.
Kutokana na ubora wa uimara wake, tofauti na Maandiko mengine Matakatifu, Qur’an iliwekwa katika hali ile ile ya ufunuo bila ya kugeuzwa kokote kwa hali yoyote wala kubadilishwa, na imetufikia kwa kuhifadhi uhalisi wake kwa miaka 1400. Ni dhahiri kuwa mtindo wa balagha na ufasaha wa Qur’an, hali yake ya kimuhtasari, wepesi wa kuihifadhi, kutokushabihiana na mhadhara wa kibinadamu, watu kushindwa kuiiga na kufikia kiwango chake cha umbuji, na uangalifu wa hali ya juu kabisa uliotumika katika kuihifadhi umechangia sana katika kutunza uhalisia wake. Hata hivyo, sababu halisi ni kwamba Allah aliiweka Qur’an katika hifadhi Yake na kwamba Ameahidi kuidumisha kama muujiza mpaka Siku ya Kiama kwa umbo na maana. Kwa hakika yafuatayo yanaelezwa katika Qur’an:
“Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.” (Qur’an, Al-Hijr, 15:9)
Leo, nakala zote za Qur’an zilizoko duniani ni za namna moja. Hakuna tofauti au ubadilishwaji. Licha ya hivyo, imehifadhiwa na mamilioni ya mahafidhi na inasomwa na mamilioni ya watu kwa wakati wote. Ubora huu haupo katika kitabu kingine chochote isipokuwa Qur’an, wala maandiko mengine yoyote ya kiungu. Ni muhimu kabisa kuwa Qur’an, ambayo ni maandiko ya mwisho ya Allah, ambayo kufaa kwake kunaendelea mpaka kiama, iwe na hadhi hii ya kipekee.
(Mehmed Dikmen, Islam Ilmihali, Cihan Yayinlari, Istanbul, 1991, uk. 94-97.)
Maswali juu ya Uislamu
