Inaweza kuthibitishwa kuwa Uisilamu ni dini ya upendo, amani na uvumilivu? Unaweza kutoa mifano ya hayo?

Submitted by on Sat, 18/08/2018 - 10:33
Dear Brother / Sister,
Neno Uisilamu linamaanisha amani kwa Kiarabu. Uisilamu ni dini iliyoteremshwa ili kumwakilisha mtu pamoja na maisha yaliyojaa utulivu na amani ambayo yana huruma isiyo na mwisho ya Allah iko waziwazi. Allah anawaita watu kuja katika maadili ya Uisilamu kuwa ndio kigezo ambacho huruma, uvumilivu na amani vinaweza kufanyiwa kazi. Yafuatay yanaelezwa katika aya 208 ya sura al-Baqara:
“Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za She’tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.”
Kama inavyoonekana katika aya, Allah anaeleza kuwa usalama wa watu unaweza kuhakikishwa tu kupitia kuukubali Uisilamu na kutekeleza kwa vitendo maadili ya Quran.
Allah anailaani fitina
Allah anawaamuru watu kujiepusha kufanya amali mbovu na kuwakataza na ukafiri, madhambi, uasi, dhuluma, ukandamizaji, mauaji na umwagaji damu. Wale wasiotii amri hii ya Allah wanatambuliwa kuwa ni wale wanaofuata nyayo za Shetani kama aya inavyoeleza; wanajitwalia waziwazi mwelekeo ambao Allah ameuharamisha. Zipo aya nyingi zinazohusiana na suala hilo katika Quran. Mbili kati ya hizo ni hizi zifuatazo:
“Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya fisadi katika nchi: hao ndio watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya.” (ar-Rad, 13/25)
“Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.” (al-Qasas, 28/77)
Kama inavyoonekanwa, Allah anakataza aina zote za matendo yanayohusiana na fitina, ikiwemo kutishia na matumizi ya nguvu na kuwalaani wale wote wanaotenda matendo ya namna hiyo. Mwisilamu ni mtu anaeipamba na kuiboresha dunia.
Uisilamu unaulinda uhuru wa kutafakari na uvumulivu
Uisilamu, ambayo ni dini inayoeleza na kuhakikisha waziwazi uhuru wa kutafakari na maisha, imetoa maamrisho yanayozuia na kukataza kuwekana roho juu, migogoro kati ya watu, kusemana na hata kuwadhania watu vibaya.
Sio tu kutishia na matumizi ya nguvu, Uisilamu unakataza kuweka hata shinikizo dogo kwenye fikra za watu.
“Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu.” (al-Baqara, 2/256)
“Wewe si mwenye kuwatawalia.” (al-Ghashiya, 88/22)
Ni kinyume na maumbile na uhalisia wa Uislamu kuwateza nguvu watu ili waamini katika dini au kufanya ibada. Kwa kuwa, Uisilamu umeweka utashi huru na ridhaa makini kuwa ndio sharti la imani. Bila ya shaka, Waisilamu wanaweza kuonya na kuhamasishana hivyo wanaweza kutekeleza kwa vitendo sifa za kimaadili zilizofafanuliwa ndani ya Quran. Hata hivyo, hawawezi kutezana nguvu kuhusiana na hilo. Sio sawa kupendekeza vipaumbele fulani vya kidunia ili kumfanya mtu fulani afanye ibada.
Fikiria kuhusu kigezo cha jumuia kilicho kinyume cha mtindo wa hilo. Mathalani, jaalia kuwa watu wanatezwa nguvu kuabudu. Jumuia ya namna hiyo iko kinyume kabisa na Uisilamu. Kwa kuwa, imani na ibada vinakuwa na thamani vinapotekelezwa kwa ajili ya Allah. Ikiwa mfumo wa utawala utawalazimisha watu kuamini na kuabudu, watu watakuwa ni washika dini kwa sababu ya kuuogopa mfumo-tawala. Kilichokuwa na thamani kwa upande wa dini ni kutekeleza dini kwa vitendo kwa ajili ya Allah katika mazingira huru kabisa.
Allah ameharamisha kuua watu wasio na hatia
Kwa mujibu wa Quran, kumuua mtu asiye na hatia ni moja ya madhambi makubwa mno:
“…aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.” (al-Maida, 5/32)
“Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini – na atakaye fanya hayo atapata madhara,” (al-Furqan, 25/68)
Kama inavyoonekanwa katika aya hapo juu, wale wanaoua watu wasiokuwa na hatia wanaonywa na adhabu kali. Allah anaeleza kuwa kumuua mtu mmoja ni uhalifu mkubwa mno kama kuua watu wote. Haiwezekani kwa mtu anayetii mipaka iliyowekwa na Allah kumdhuru hata mmoja achilia mbali kuua maelfu ya watu wasio na hatia. Wale wanaodhani kwamba wanaweza kuikwepa haki na kunusurika nayo hawatoweza kukwepa kisasi mbele ya Allah. Kwa hivyo, waumini wanaojua kwamba watalipiziwa mbele ya Allah baada ya kifo wanatenda mambo kwa uangalifu mno ili kutii mipaka iliyowekwa na Allah.
Allah anawaamuru waumini kuwa na huruma
Maadili ya Mwisilamu yanafafanuliwa kama ifuatavyo katika aya:
“Tena awe miongoni mwa walio amini na wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumiana. Hao ndio watu wa kheri wa kuliani.” (al-Balad, 90/17-18)
Moja ya sifa muhimu mno za maadili yaliyoteremshwa na Allah kwa waja Wake ili wapate wokovu Siku ya Kiama, rehema Zake na Pepo ni “kuamrishana subira”.
Uisilamu, unaoelezwa katika Quran, una muundo wa kisasa, wenye kuelimisha na wa kimaendeleo. Mwisilamu wa kweli anayo haiba ya amani, uvumilivu, kidemokrasia, kitamaduni, utambuzi/usomi, uaminifu, jicho la sanaa na sayansi na ustaarabu.
Mwisilamu aliyelelewa na maadili ya juu yaliyotajwa na Quran anatangamana na kila mtu kwa upendo unaotumainiwa na Uisilamu. Anaonesha heshimwa kwa fikra za aina zote, anathamini uzuri wa kisanaa na sanaa, na anaonesha kuwafikiana, sifa za kujumuika pamoja na uwastani. Jumuia zilizoundwa na watu kwa mfumo huo zitakuwa na maendeleo zaidi ya ustaarabu na maadili ya juu kuliko zile za dola za kisasa zinazofuatana na furaha, amani, haki, usalama, wingi wa neema na usitawi.
Allah anaamrisha uvumilivu na subira
Nadharia ya “kusamehe na kuvumilia” iliyotajwa na ibara “shikamana na kusamehe” katika aya 199 ya sura al-Araf katika Quran inaunda moja ya kanuni za kimsingi za dini ya Uisilamu.
Ikirejelewa historia ya Uisilamu, itaonekana waziwazi kuwa ni namna gani sifa hizi muhimu za maadili ya Quran zinatekelezwa kwa vitendo. Waisilamu wanaondosha matendo maovu katika kila pahala wanapopafikia na kuweka uwastani wa uhuru na uvumilivu. Wanawawezesha watu wanaotofautiana kidini, kilugha na kitamaduni kuishi pamoja chini ya paa moja la amani na utulivu; pia wanawafanya wale wanaowatii kunufaika na elimu kubwa, utajiri, na ubwana. Kwa hakika, moja ya sababu muhimu za kwa nini Ufalme wa Uthmaniya, ulienea kwenye eneo kubwa la kijiografia, uliokuwepo kwa karne kadhaa ni kuufanyia kazi uwastani wa uvumilivu na kufahamu kuwa umetambulishwa na Uisilamu. Mara zote Waisilamu wamekuwa ndio wenye huruma zaidi na waadilifu katika vipindi vyao. Matapo mengine ya kikabila yaliyoishi katika umbo hili la mchanganyiko wa kimataifa wametekeleza dini zao kwa uhuru na walikuwa na nyenzo zote za kutekeleza dini zao na tamaduni.
Pindi uvumilivu, waliokuwa nao Waisilamu katika namna yake halisi, utatekelezwa kwa namna ambayo Uisilamu unaamuru, utaleta amani na utulivu kwa dunia nzima. Kwa hakika, yafuatayo yameelezwa katika Quran.
“Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu. (Fussilat, 41/34)
Aya ya hapo juu inavutia mazingatio kwa sifa hii.
Yote yanaonesha kuwa sifa za kimaadili ambazo Uisilamu umewashauri watu ni za wema utakaoleta amani, utulivu na haki kwa dunia. Ushenzi, unaoitwa “ugaidi wa Kiisilamu”, ulioweko kwenye agenda ya dunia, ni kazi iliyofanywa na washabiki wajinga ambao wako mbali kabisa-kabisa na maadili ya Quran na wahalifu ambao hawana mahusiano kabisa na dini ya Uisilamu. Utatuzi wa kielimu wa kutumika dhidi ya watu hawa na makundi yanayofanya ushenzi chini ya kusingizio cha Uisilamu ni kuwafundisha watu kuhusu maadili halisi ya kweli ya Uisilamu.
Kwa maneno mengine, dini ya Uisilamu na maadili ya Quran hayaungi mkono ugaidi na magaidi; kinyume chake, yataiokoa ardhi kutokana na matatizo ya ugaidi.
Dini ya Amani na Mtume wa Upendo
Mitume ni watu walioteuliwa kuifanya dunia kuwa ni ardhi ya ustawi na amani. Wameletwa ili kufikisha dini ya Uisilamu, ikimaanisha, “amani na usitawi” kwa utu. Mtume ameeleza yafuatayo katika hadithi:
“Sisi mitume ni ndugu wa baba mmoja, dini yetu ni moja.” (Bukhari, Anbiya, 48)
Allah anaeleza yafuatayo katika Quran:
“Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu.” (Aal-i Imran, 3/19)
Anatuhabarisha kuwa mitume wote waliteremshwa ili wawajuvye watu kuhusu dini hii na kwamba mitume wameonesha mifano ya mwanzo kwa watu.
Usilamu unamaanisha kuwa ni amani na usitawi. Mwisilamu maana yake ni mtu mwenye kupata amani na usitawi na mwenye lengo la amani na usitawi. Moja ya majina ya Allah ni “Salam” (Amani). Kwa mujibu wa hayo, yeye ndiye chanzo cha amani na usitawi. Mwisilamu anaejisalimisha Kwake ni mtu anaepata amani na utulivu katika ulimwengu wake wa ndani kwa kushikamana na chanzo cha amani na usitawi na kisha ni mwenye kutaka kufikisha amani hii kwa ulimwengu wa nje. Kwa hakika, Mwisilamu mwema anajaribu kujiweka mbali na aina zote za mkanganyiko, migogoro na hisia zenye kuidhuru amani ya ndani hata kama anaishi katika mazingira yasiyopendeza kabisa. Kwa hivyo, Mwisilamu anaeikusudia “Daru’s Salam’ (ardhi ya amani na usitawi), Pepo, amechaguliwa kuifanya dunia kuwa ni ardhi ya amani. Labda ni kwa sababu hii, mtu wa kwanza aliyeingizwa Peponi kabla ya kuja duniani; kwanza, aliumbwa aishi Peponi na aliandaliwa kwa utamaduni wa Peponi; kisha, akaletwa duniani. Vile kutumwa duniani, binadamu ana mapenzi na Pepo; anajaribu kujenga duniani kwanza na anaota angalau kuipata huko ahera.
Vivyo hivyo, jina jengine la Mwisilamu ni mumin (muumini), linalomaanisha kuwa na usalama na uaminifu. Mumin pia ni jina la Allah. Kwa hivyo, muumini maana yake ni mtu anayemwamini Allah, ambaye ndiye chanzo cha usalama na uaminifu, anayeshikamana Naye, ambaye ni mwenye kufungamana na amani ya dunia yake ya ndani na anayechukua uwastani huu wa usalama aliyoujenga katika dunia yake ya ndani kuupeleka katika dunia ya nje. Kwa hivyo, uwepo wa waumini ni jambo zuri kwa kila mtu. Kwa hakika, yafuatayo yanaelezwa ndani ya Quran huku kukitajwa jumuia ya Uisilamu:
“Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu…” (Aal-i Imran, 3/110)
Jina jengine la Allah ambaye ni mmiliki wa dini ya Uisilamu ni Wadud (Hud 11/90). Wadud ni nomino inayomaanisha yule anayependa mno au yule anayependwa sana. Ndio, Allah ndio chanzo cha mapenzi. Ameumba mapenzi na akayaweka ndani mwetu pale Alipoyapuliza ndani mwetu kutokana na roho Yake. Kama Ibn Arabi anavyoeleza,
“tumetokana na asili ya mapenzi; tumeumbwa nje ya mapenzi; tukayaelekea mapenzi na kuyapa moyo wetu.” (Ibnu'l-Arabi 1998, 38)
Kwa hakika, yafuatayo yanaelezwa katika aya:
“Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kurehemu na Mwenye upendo.” (Hud, 11/90)
Allah, aliye mzuri katika namna zote na anapenda mazuri, ameyaingiza mapenzi katika maumbile ya binadamu, akatuma mitume, waliojawa na upendo, ili upendo uonekana dhahiri katika maneno na mtazamo; pia ametuma vitabu vilivyo na kanuni zinazowawezesha watu kupenda na kupendwa. Hatimaye, alimtuma Bwana Muhammad (s.a.w.) na kuwageuza watu walioshambuliana kikatili kuwa watu wanaopendana na kuwapendelea wengine zaidi ya wao wenyewe. Aya mbili zifuatazo zinahusiana na suala hilo:
“Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.” (Aal-i Imran, 3/103)
“Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.” (al-Hashr, 59/9)
Kwa mujibu wa Uisilamu, ushindi mkubwa ni amani. Kwa hakika, kinachomaanishwa na ushindi wa wazi katika aya ya mwanzo ya sura ya al-Fath “Hakika tumekufungulia Ushindi wa dhaahiri” ni Mkataba wa Amani wa Hudaybiyah (Tabari, 26:67-68; Ibn Kathir, 4:183) kwa mujibu wa wanazuoni wengi. Kulingana na kipengele muhimu mno cha mkataba huu, uliotiwa saini na makundi mawili yaliyokuwa ukingoni kuingia vitani, Waisilamu na washirikina wa Makkah wasingepigana kwa muda wa miaka kumi. Kwa mkataba huu, uliotiwa saini baada ya mapigano ya Badr, Uhud na Khandaq mnamo mwaka wa 6 wa Kuhama, Mtume (s.a.w.) aliondosha kikwazo cha vita vilivyouepusha Uisilamu, dini ya uaminifu na amani, kutoenea; kwa namna fulani, kikwazo kati ya watu na mapendefu yao na kuutafuta ukweli kiliondoshwa.
Bwana Muhammad (s.a.w.), Nembo ya Upendo na Uaminifu
Bwana Mtume (s.a.w.) alifanya kazi kwa ajili ya wema wa jumuiya, ambayo uwepo wake ni manufaa kwa utu, na alifariki baada ya kuiunda jumuia hiyo. Kwa hakika, alipokuwa hai, Wayahudi wa Khaybar haikuwasaidia kusema, “Pepo imejengwa duniani na Waisilamu” kutokana na yeye kusimamisha haki na usawa. Mtume (s.a.w.) ameonesha na kuweka mfano bora zaidi kupitia mfumo wa maisha yake.
“Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.” (al-Ahzab, 33/21)
Kwa hakika, alithaminiwa na kila mtu wakati wa uhai wake wa miaka-arubaini kabla ya utume mjini Makkah na aliitwa ‘Muhammadu’l-Amin’ (Muhammad Mwaminifu). Uaminifu huu na hadhi hii vilimsababishia/ulimsababisha Bibi Khadijah (r.a.) kumteua kuwa ni kaimu wake katika biashara ya kimataifa; alichaguliwa kuwa ni mwamuzi katika tukio la kuliweka Jiwe Jeusi kwenye Kaaba na alikuwa ni mjumbe wa kuheshimika katika jamii iliyoitwa Hilf al-Fudhul (Umoja wa Waadilifu), ulioanzishwa mjini Makkah ili kupambana dhidi ya dhuluma mjini humo. Uaminifu wake katika ubia wa biashara kabla ya kupewa utume umevutia umakini wa kila mtu. Maisha yake kabla ya utume ni kipindi cha miaka arubaini, ambao ni muda zaidi ya nusu ya maisha yake ya miaka sitini-na-tatu. Katika kipindi hicho, kabla hajapokea ufunuo kutoka kwa Allah, aliishi akiwa safi na mwaminifu ilhali watu wengine wamenyimwa uaminifu. Kwa hivyo, ukamilifu wake wa kimaadili kabla ya utume ni muhimu mno kwa watu wa leo ambao wangetumia sifa hasi/mbaya kuwa ndio kisingizio cha kutomwamini yeye. Yafuatayo yanaelezwa katika aya za Quran zikifafanua kuwa alikuwa ni mtu aliyejulikanwa kwa maadili yake ya juu katika jumuia aliyoishi: “Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa?” (al-Mu'minun, 23/69)
“Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli kusomeeni, wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nalikwisha kaa nanyi umri mzima kabla yake! Basi, je! Hamzingatii?” (Yunus, 10/16)
Nimeishi miongoni mwenu kwa miaka arubaini kabla ya kuwa mtume. Mnajua usahihi wangu, uaminifu, kuaminika na kutojua kusoma wala kuandika. Sijawahipo kumwasi Allah nilipokuwa kijana. Iweje mniombe nifanye kitu kama hicho sasa? (Qurtubi, 8:321) Moja ya aya za Quran zinataja sifa zake nzuri kama ifuatavyo:
“Na kwa hakika wewe una malipo yasiyo katika.” (al-Qalam, 68/3)
Aya hii ya sura al-Qalam, iliyoteremshwa kuwa ni sura ya tatu baada ya sura za al-Fatiha na al-Alaq, waziwazi zinathibitisha uaminifu alionao kwa sababu aya za Quran zilizozungukia maisha yake yote bado zilikuwa hazijateremshwa kwa wakati huo. Alikuwa na maadili adhimu na ya juu. Baadaye, Bibi Aisha, mkewe, aliifanyia muhtasari haiba yake ya kimaadili, iliyokuwa ilishapevuka zaidi na kamilifu kwa Quran kama ifuatavyo:
“Maadili yake ni maadili ya Quran.” (I. Hanbal, Musnad, 6:188)
Wakati wa sherehe ya arusi ya Mtume na Bibi Khadijah, Abu Talib, ami yake alimtambulisha mtoto wa nduguye, aliyekuwa na umri wa miaka ishirini-na-tano, kama ifuatavyo: “Kwa kweli, Muhammad ni kijana asiyekuwa na mfano na hawezi kuzingatiwa kuwa ni sawa na kijana yeyote wa Kikuraish. Hivyo, amekuwa ni kijana wa kipekee kwa heshima yake, utukufu wake, wema na weledi.” (I. Hisham, 1/201)
Bibi Khadijah (r.a.) alimwambia Mtume (s.a.w.), mumewe, yafutatayo wakati alipotaharuki mno pale alipopokea ufunuo wa mwanzo:
“Tulia; usiwe na wasiwasi. Naapa kwa Allah kuwa Allah hatokufedhehesha au kukuaibisha. Kwa kuwa, unawatunza ndugu zako. Daima unasema ukweli. Katu hukuwa mbadhirifu. Wewe ni mkunjufu na unawasaidia wanyonge. Unapenda kuwakirimu wageni. Unawasaidia watu walio katika matatizo na waliodhulumiwa.” (ibid, 1:253)
Wema alionao pia umetajwa na maadui zake. Kisra wa Roma alimuuliza Abu Sufyan, ambaye bado hakuwa muumini wakati huo, aliyekuwepo kwa Kisra kama ni balozi, akiuliza kuhusu sifa za Mtume (s.a.w.) na mazungumzo yafutayo yalitokea kati yao:
- Je umewahi kumsikia akisema uongo?
- Hapana, hatujawahi kusikia uongo wowote kutoka kwake.
- Mtu asiyedanganya watu hawezi kuongopa kuhusu Allah.
Jafar b. Abi Talib, aliyehamia Ethiopia, ameeleza yafuatayo mbele ya Najjash:
“Ewe Najjash! Allah ametuletea mtume miongoni mwetu; tumeshamjua kwa miaka arubaini kuwa ni mwaminifu, mtukufu na ni mtu wa kuaminika…” (Ibn Kathir, Tafsir, 2:411)
Mtume (s.a.w.) alikwenda Taif ili kuwafikishia watu wanaoishi huko ujumbe wa Uisilamu na kuwaomba wamuunge mkono alipofurushwa kwa shinikizo kubwa la washirikina na makafiri katika miaka yake kumi ya utume. Alikaa huko kwa miaka kumi na kutembelea nyumba moja baada ya nyengine akiwahubiria kuhusu Uisilamu. Hata hivyo, walimfanya kituko na kumfukuza. Walimrushia mawe na rafiki yake, Zayd mpaka miguu yao ikaroa damu walipokuwa wakiondoka. Alikimbilia kwenye bustani na huko akaomba dua ifuatayo:
“Ewe Allah! Nakulalamikia udhaifu wangu, ukosefu wa nyenzo na mateso niliyofanyiwa na watu. Ewe Mwingi wa Rehema kuliko wote. Ewe Mola Mlezi wa wanyonge na Mola wangu Mlezi pia. Umeniaminisha kwa nani? Kwa watu nisiowazoea ambao wamenipokea kiuadui? Au kwa adui ambaye umemtunuku madaraka juu ya mambo yangu? Kwa kuwa hujanikasirikia, basi sijali. Hisani yako ni tulizo kubwa mno kwangu. Narejea kwako kwenye nuru ya Uso Wako ambao giza la aina zote linatoweka na jambo lolote la dunia hii na baadaye limepangiliwa vyema, isijekuwa hasira Zako au kutokuridhika Kwako kuniangukie mimi. Ninatamani radhi zako mpaka uridhike. Nguvu zote ni zako.” (Köksal, 5/66-71)
Wakati huo huo, malaika alifika na kumwambia Mtume angewaangamiza kama angetaka. Bwana Mtume (s.a.w.) akajibu yafuatayo:
“Hapana. Sitaki waangamizwe. Kinyume chake, natarajia vizazi vyao vitamwabudu Allah na hawatomshirikisha Yeye na kitu chochote.” (Köksal, 5/76)
Jino lake lilipovunjwa katika vita vya Uhud, watu waliomzunguka wakamwomba awalaani washirikina. Akasema,
“Sikuletwa kuja kuwalaani watu. Ewe Mola Mlezi! Waongoe watu wa kabila langu kwa sababu hawaelewi.” (Bukhari, Anbiya, 37)
Kwa kifupi, alikuwa na upendo kwa watu wote; alijitolea maisha yake yote ili kuwaokoa watu; alikuwa mtume wa upendo na huruma. Kwa mujibu wake yeye, kumwongoa mtu mmoja, yaani, kumfanya asilimu, ni bora zaidi kuliko dunia na vilivyomo ndani yake.
Makkah ilikombolewa katika mwaka wa nane wa Hijria. Watu wa Makkah, waliomfukuza Mtume (s.a.w.) na waumini kutoka nje ya mji wao, waliowadhulumu na kuwatesa na walioushambulia mji wa Madinah mara kadhaa baada ya kuhamia huko, walilazimika kujisalimisha kwenye jeshi lililoingia Makkah chini ya amri ya Bwana Mtume (s.a.w.). Ilhali watu wa Makkah wanasubiria kwa wasiwasi na woga, Bwana Mtume (s.a.w.), aliyeonesha upendo, huruma na uvumilivu wa kiwango cha juu, aliwahutubia ifuatavyo:
“Leo hii hamtolaumiwa: Allah atakusameheni, kwani yeye ni Mwingi wa Rehema kwa wale wenye huruma. Ondokeni. Mko huru!” (Köksal, 15/288-289)
Ni muhimu mno kwetu kujua majina na sifa za Mjumbe wa Allah ambazo zimetajwa katika aya za Quran na hadithi ili tumjue vilivyo.
Ni mtume wa huruma (Rasulu'r-Rahma, Nabiyyu'l-Marhama). Hakuletwa kwa kundi fulani maalumu bali ni rehema kwa viumbe wote.
Yeye ni mbashiri wa habari njema na mwonyaji (al-Mubashshir, al-Bashir; al-Mundhir, an-Nadhir).
Yeye ni ukweli ulio dhahiri (al-Haqqu'l-Mubin).
Yeye ni kishikizo cha kuaminika (al-Urwatu'l-Wuthqa).
Yeye ni njia iliyonyooka (as-Siratu'l-Mustaqim).
Yeye ni nyota yenye kupenya mwangaza (an-Najmu'th-Thaqib).
Yeye ni taa inayoangaza nuru (an-Nur, as-Siraju'l-Munir).
Yeye ndiye anayelingania kwa Allah (Dai ilallah).
Yeye ndiye mwombezi ambaye uombezi wake ndio unaokubalika (ash-Shafi', al-Mushaffa').
Yeye ndiye mboreshaji (al-Muslih).
Yeye ndiye kipenzi na rafiki wa Allah (Habibullah, Khalilurrahman).
Yeye ndiye mwenye ushahidi mzuri na hoja (Sahibu'l-Hujja wa'l-Burhan).
Yeye ni mtu wa pekee aliyeteuliwa na Allah (al-Mustafa, al-Mujtaba, al-Mukhtar).
Amesifika; yeye ndiye anayestahiki kusifiwa (Muhammad, Ahmad, Mahmud, Hamid).
Yeye ni Muhammad mwaminifu (Muhammadu'l-Amin).
Yeye ndiye mtume wa mwisho (Khatamu'n-Nabiyyin) (Qadi Iyad, 189-195).
Inawezekana kumjua mtu huyu aliyejawa na upendo, aliyeteuliwa kuwa ni nembo ya uaminifu na wa kuchukuliwa kuwa ndio kigezo si kwa kingine isipokuwa kwa kumjua, kuwa kama yeye na kumpenda. Hichi ndicho kinachokusudiwa kwa kumwelewa yeye. Kwa hakika, alisisitiza ukweli huu kwa kusema,
“Mtu anayeifuata sunnah yangu ni katika mimi; na mwenye kuipuuza sio katika mimi.” (Ma'mar ibn Rashid, 11/291)
Kwa ujumla, kumfahamu na kumpenda Mtume (s.a.w.) kunawezekana tu kupitia kumjua yeye vizuri katika namna zote, kumfuata yeye, kumtaja sana, kuheshimu manufaa ya kilimwengu aliyoyatambulisha, kupenda alichokipenda na kujiweka mbali na asichokipenda, na kuwa na maadili ya Quran, ambayo ndio maadili yake.
Sura za Upendo kutoka katika Maisha ya Mtume
Sasa, tunataka kuonesha baadhi ya sura za upendo kutoka kwenye maisha ya Mjumbe wa Allah:
1. Kumpenda Allah: Mjumbe wa Allah (s.a.w.) alikuwa makini kwamba muda wote alikuwa chini ya uchunguzi wa Allah. Alijaribu kutimiza wajibu wake wa kumhudumia yeye. Lengo lake kuhusiana na hili lilikuwa ni “Kuwa mja anaeshukuru” (Bukhari, "Munafiqun," 79) Mtume (s.a.w.) alikuwa ni mtu aliyemjua Allah kwa namna bora zaidi. Mara zote alikuwa akiwasiliana Naye. Lengo lake la pekee lilikuwa ni kupata radhi Zake. Kifo kilimaanisha kumfikia Yeye. Kwa hakika, mapenzi ya Allah na kupenda kwa ajili ya Allah ndio maudhui makuu katika maneno yake mengi. Isitoshe, ukweli kwamba amejawa na upendo uliounganishwa na uhusiano wake na kuwasiliana na Allah.
2. Kupenda Watoto:Mtume (s.a.w.) aliwabeba watoto mapajani mwake, aliwabusu na kuwabimbabimba. (Bukhari, "Adab", 22) Pale mtu mmoja aliposema kuwa anao watoto kumi lakini hajawahi kumbusu hata mmoja wao, Mtume akasema, “Mtu asiyeonesha huruma hatohurumiwa. Nitafanyaje kama Allah ameondosha huruma moyoni mwako?” (ibid). Aliwajali watoto na vijana; aliwaheshimu na kuwathamini. Vijana walikuwa na nafasi muhimu na ya kipekee kati ya wale waliomwamini yeye. Aliwazawadia vijana fanisi kwa kuwateua kuwa makomandoo wa majeshi kulikowahusisha Maswahaba watukufu. Kwenye vikosi vya Tabuk, alimpa Zayd b. Thabit bendera ya Wana wa Najjar, ambaye alikuwa na miaka ishiri tu; Alimteua Bwana Ali, aliyekuwa na umri wa miaka ishirini-na-moja, kuwa ni mbeba bendera katika Vita vya Badr; alimteua Usama b. Zayd, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na nane kuwa ni komando wa jeshi lililokuwa na wanajeshi elfu arobaini lililotumwa dhidi ya Wana wa Qudaa; alimteua Muadh b. Jabal, aliyekuwa na umri wa miaka ishirini-na-moja, kuwa ni kadhi wa Yemen. (Doğuştan Günümüze…, 1:391-392)
3. Kuipenda Familia yake na Jamaa: Alikuwa ni kiongozi wa familia aliyeipenda familia yake. Hakuepuka kuisaidia. Alikuwa akikata-kata nyama, akikata-kata mbogamboga za mung’unye, na kupika. Aliitunza zaidi familia yake kuzingatia wajibu wao kwa Allah kuliko kitu kingine chochote. Kwa kuwa, alipokea amri ifuatayo kutoka kwa Allah:
“Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchamngu.” (Ta-Ha, 20/132)
Alianza kuwalingania watu wake kwanza kwa sababu Allah alimwamuru ifuatavyo:
“Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.” (ash-Shuara, 26/214)
Daima aliendeleza mahusiano yake na jamaa zake na kuwaomba wafanye hivyo, pia. Mara zote alisisitiza kuwapenda wazazi wawili, aliwahamasisha watu kuwapenda mama zao walezi na kaka zao walezi na marafiki wa baba zao; aliwajali na kuonesha mfano mzuri kabisa.
4. Kuwapenda Marafiki: Mtume (s.a.w.) aliwanyanyua hadhi watu walioishi katika giza la Jahiliyyah hadi kwenye cheo cha watu bora katika historia ya binadamu kwa kuvumilia aina zote za matatizo na ugumu. Aliwasamehe watu waliomtesa kipindi cha nyuma na kuwatukuza.
“Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.” (at-Tawba, 9/128)
“Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini.” (al-Hijr, 15/88)
“Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini...” (ash-Shuara, 26/215)
5. Kuupenda ummah: Alijitolea maisha yake kwa ummah wake; atasema, “Ummah wangu! Umman wangu! Ewe Allah! Nautaka ummah wangu!” ahera wakati mitume wengine watashughulishwa na matatizo yao wenyewe. (Abu Awana, Musnad, 1:158)
6. Kupenda Utu: Yeye ni mtume aliyeletwa kuwa ni rehema kwa viumbe wote (al-Anbiya 21/107). Alimlingania kila mtu kuja katika Uisilamu haijalishi walikuwa wabaya kiasi gani. Alikuwa ni mtume ambaye hakuacha kujitoa muhanga kwa namna yoyote ili kuwaokoa watu. Alizuru majumba, masoko, miji, na alienda safari za mbali katika maeneo mengi chini ya mazingira magumu kabisa. Aliwatendea vyema majirani zake bila ya kujali imani zao. Alipinga kuua watu bila ya haki, kuwatesa na kuwafanya watumwa. Alikataza kuua watu kwa kuwatesa hata katika vita; aliwaamuru wanajeshi wake kutokuwagusa wale ambao hawakushiriki katika vita na wale waliosema tumeukubali Uisilamu. Idadi ya watu waliokufa vitani wakati wa zama zake ilikuwa ni kiasi cha watu mia nne tu.
Upendo na huruma ya Mtume (s.a.w.) ilikuwa na asili ya kiungu:
“Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea.” (Aal-i Imran, 3/159)
7. Upendo wake kwa viumbe wengine na mazingira: Tunaona kwamba aliwapa umuhimu viumbe wengine wasiokuwa binadamu, kwa wanyama na mimea na kwamba alifanya kadri awezavyo kuweka mazingira safi.
“Wahurumieni waliopo ardhini ili waliowepo mbinguni wakuhurumieni nyinyi” (Tirmidhi, Birr, 16)
Kwa kuitamka hadithi ya hapo juu, Mtume ameashiria kuhurumiwa ni kuonesha huruma kwa viumbe vyote ardhini. Alieleza kuwa mwanamke aliyempa mbwa maji alisamehewa na yule aliyemuua paka kwa kumtesa alizivuta hasira za Allah. Alipomwona mtu akimkama mbuzi, alisema:
“Unapokama yawache baadhi ya maziwa kwa mtoto wa mbuzi.” (Majmua'z-Zawaid, 8:196)
Alipoulizwa, “je kuna thawabu mtu anazipata kwa kuwafanyia hisani wanyama?, akasema, “Ndio, kuna thawabu kwa kila hisani iliyofanywa kwa kiumbe chochote.” (Bukhari, Shurb, 9) Aliwaamuru watu kutia makali kisu wanapochinja mnyama na sio kuwanyanyasa wanyama wanapowachinja. (Muslim, "Sayd". 57)
Wakati mmoja, alipanda miti ya mitende mia tano (I. Hanbal, 5:354) na kueleza yafuatayo kuhusiana na hilo:
“Kama Mwisilamu atapanda mti kisha wanadamu, wanyama wa nyumbani, wanyamapori au ndege wakala matunda yake, kile walichokila kitazingatiwa kuwa ni sadaka kwa yule aliyeupanda mti ule.” (Muslim, Musaqat, 10)
“Kama unao mche wa mti, basi uatike hata kiama kinapokaribia sana kufika, uatike.” (Bukhari, al-Adabu'l-Mufrad, 168)
Alipomwona mtu anaupiga mti ili kondoo wake wale majani yake, aliingilia kati na kusema
“Taratibu! Kama unataka majani yaanguke, utikise mti; wala usiupige.” (Usdu'l-Ghaba, 3:276)
Allah ameitangaza Makkah kuwa ni eneo lililohifadhiwa (haram) na Mtume (s.a.w.) ameitangaza Madina na Taif kuwa ni maeneo yaliyohifadhiwa. (Bayraktar, 5:223-227)
“Ardhi yote imefanywa ni msikiti kwa ajili yangu; udongo wake ni safi na kufanya vitu kuwa safi.”
Zipo hadithi nyingi zinazoeleza upendo wa Mtume (s.a.w.) kwa Makkah, Madinah, Mlima wa Uhud na sehemu nyenginezo. Pia alipendezwa na viumbe wa mbinguni na kuthamini kupaa kwao na kuratibu nyakati kuwa ndio fursa ya kuomba.
Kumpenda Mtume
Mapenzi ni hisia ambazo zimejikita katika moyo na kudhihirika kwa maneno na ishara. Kumpenda mtu fulani maana yake ni kumpa vitu kwa ajili ya kipenzi. Mapenzi ni tendo la kutoa. Kumpenda Mtume (s.a.w.) ni kuuratibu moyo wa mtu kwa ajili yake, kujitolea muhanga na mtu kutoa mali na maisha kwa ajili yake ikibidi kufanya hivyo. Hili litatokea kwa kumjua tu yeye, kumfuata, kupenda alichokipenda na aliowapenda, kuonesha heshima kwa Quran na sunnah zake, ambazo amezikabidhi kwetu, kuzitunza na kutomtangulia kwenye suala lolote.
Hakuna mapenzi bila ya elimu. Kwa hivyo, hatuwezi kumpenda sawasawa isipokuwa tumjue yeye kikweli. Sio sahihi kuweka mpaka wa kumpenda yeye kwa kuwa na jina lake, kulitaja jina lake kwa heshima, vitu vyake binafsi alivyonavyo (masalio/kumbukumbu). Inamaanisha kuwa makini na ukweli kwamba kumpenda yeye kunamaanisha kulitaja jina lake mara kwa mara kwa heshima, kwamba tunamtaja pale tunapotamka kalima at-tawhid, salawat, tunaposoma na kusikiliza adhan, tunapotamka maombi ya Allahumma salli wa barik “Maamkizi ya Allah, rehema na baraka ziwe juu yako, ewe Mtume!”
Ni lazima kupenda ili kupendwa. Ili kustahiki upendo, kupenda na kupendwa kunawezekana tu kupitia kuwa na mahusiano na Allah ambaye ndio chanzo cha mapenzi.
“Hakika walio amini na wakatenda mema Arrahmani Mwingi wa Rehema atawajaalia mapenzi…” (Maryam, 19/96)
Chanzo cha mapenzi ni Allah, ambaye pia anaitwa al-Wadud (Mwenye Upendo wa Dhati).
“Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu. Sema: Mt’iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakigeuka basi Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.” (Aal-i Imran, 3/31-32)
Marejeo:
Asım Köksal, İslâm Tarihi; Bukhari, al-Adabu'l-Mufrad; Doğuştan Günümüze İslâm Tarihi; Abu Awana, Musnad; Ibn Hisham, as-Siratu'n-Nabawiyya; Ibnu'l-Arabi, İlâhî Aşk, (Kilichofasiriwa na Mahmut Kanık), İstanbul, 1998; Qadi Iyad, Kitabu'sh-Shifa; Ma'mar b. Rashid, al-Jami'; Mehmet Bayraktar, "Asr-ı Saadette Çevre Bilinci", Bütün Yönleriyle Asr-ı Saadet'te İslâm; Muhammed Hamidullah, Hz. Peygamberin Savaşları; Munawi, Faydu'l-Qadir; Tabari, Tafsir; Ibn Kathir, Tafsir; Razi, Tafsir; Qurtubi, Tafsir.
Maswali juu ya Uislamu