Je, Uislamu dini ya vita?

The Answer

Dear Brother / Sister,

Vita havipendezi lakini utu haukuweza kuondoa vita katika historia nzima. Katika Quran, mapambano ya watoto wawili wa Adam yametajwa. Mmoja hakuwa na hatia na mwingine ni mgomvi. Yule mgomvi akamuua yule ambaye hakuwa na hatia. (Angalia sura al-Maida, 27-31). Jina la yule ambaye hakuwa na hatia ni Habil; na jina la mgomvi ni Qabil.

Qabil alipomuua ndugu yake, damu ya binadamu ilimwagwa kwa mara ya kwanza duniani. Hata hivyo, damu hii ilizidi kadiri wakati ulivyosogea na ikaenea duniani kote. Habil na Qabil ni wawakilishi wa watu wasio na hatia na wagomvi. Madam watu kama Qabil wapo duniani, watu kama Habil watakuwa na haki ya kujilinda.

Hivyo, Uislamu unaruhusu vita kwa kuzingatia masharti kadhaa ili kuzuia udhalimu wa wakandamizaji na kuhakikisha kuwa amani inaenea kote. Mathalani, tuangalie aya ifuatayo:

“Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.” (al-Hajj, 39)

Aya hii inamwambia Mtume na Maswahaba wake ambao ndio walio katika daraja la kwanza katika Uislamu. Walifanyiwa dhuluma na mateso yaliyosababisha kifo kwa baadhi yao katika mji wa Makkah. Baadhi yao walikwenda Abyssinia kwa kufuata ushauri wa Mtume. Baadaye wengine walihamia Madinah. Takriban kila mara walisikia habari kama zifuatazo: “Watu wa Makka wanashambulia; Watu wa Makka wameshambuliwa.” Waislamu waliruhusiwa kupigana walipokuwa katika hali hizo.

Yafuatayo yameelezwa katika aya nyingine zinazohusu vita:

“Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao uadui.” (al-Baqara, 190)

Masuala yafuatayo yametajwa katika aya hiyo:

1- “Piganeni na wale wanaokupigeni.” Yaani, msipigane na wale wasiokupigeni. Kwa hakika, Mtume aliwaamuru makamanda wake wasiwaue watoto, wanawake, wazee na waliojitenga kwa kukaa katika mahekalu.

2- Vita lazima viwe “fi sabilillah”, yaani “katika njia ya Allah.’ Huenda wengine wakapigana ili kuvamia nchi mpya na kupata rasilimali za malighafi, n.k. Hata hivyo, Muislamu anaweza kupigana kwa ajili ya njia ya Allah tu. Yaani, anapambana ili kuzuia ukatili, uovu na vurugu duniani.

3- Hairuhusiwi kuvuka mipaka wakati wa vita au baadaye. Uislamu unawaamuru Waislamu kuua kwa namna nzuri wanapolazimika kufanya hivyo. Mathalani, Uislamu unakataza kuua kwa kutesa na kukata masikio, pua, n.k.

Yafuatayo yameelezwa katika aya nyingine:

“Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako’’ (an-Nisa,75)

Katika aya hii, Waislamu wanashauriwa kupigana kama wanakandamizwa katika mji au kama wanazuiwa kutekeleza imani yao. Mwishoni mwa vita, Waislamu wanakuwa huru dhidi ya uonevu na wanapata uhuru wa dini na dhamiri; watu wa nchi hiyo wanakuwa huru kusilimu ama laa.

Tunaweza kusema yafuatayo katika kuhitimisha:

Kilicho muhimu katika Uislamu ni amani si vita. Hata hivyo, watu wanapokandamizwa au dola inaposhambulia dola nyingine, vita vitakuwepo. Uislamu unaruhusu vita katika hali hizo. Uislamu haukuanzisha vita katika wakati ambao havikuwepo duniani. Wanaouzingatia Uislamu kuwa ni dini ya vita waangalie historia yao wenyewe, wataona kuwa kulikuwa na vita takribani katika kila kipindi cha historia yao. Kwa hiyo, kuwepo kwa hukumu za vita katika Uislamu si upungufu kwa Uislamu bali ni ukamilifu. Katika hukumu zilizotajwa katika aya na hadithi, uhalisia kama vita ambavyo haviepukiki ulibadilishwa na kuwa ustaarabu na utu kutoka ubedui na unyama.

Maswali juu ya Uislamu

Author:
Maswali juu ya Uislamu
Subject Categories:
Read 225 times
In order to make a comment, please login or register
MASWALI YENYE KUFANANA
THE MOST ASKED QUESTIONS