Ni yapi masharti ya msingi ambayo dini ya Uislamu inayomshurutisha mtu?

Submitted by on Wed, 08/08/2018 - 14:40
Dear Brother / Sister,
Ili kuweza kufahamu umuhimu unaopewa haki za kibinaadamu katika Uislamu, ni lazima tuangalie hali ya dunia kabla ya Uislamu.
1. Dola zote za duniani zilikuwa zikitawaliwa na tawala za kifalme. Mfalme, mtawala au dola ilikuwa na mamlaka kamili juu ya watu aliowatawala. Aliweza kumnyonga yeyote kwa matakwa yake na hakuwajibika kwa yeyote.
2. Watu waligawanyika katika matabaka. Watu waliomzungua mfalme, ndugu zake na waheshimiwa walikuwa katika daraja la upendeleo. Kwa upande mwingine, kulikuwa na watu wengi waliotwezwa na ambao haki zao zilikiukwa, hao waliunda tabaka jingine. Kulikuwa na tofauti kubwa baina ya matabaka.
3. Utumwa ulitumika katika hali ya unyama mkubwa. Heshima ya mwanadamu ilikandamizwa.
4. Watu walikuwa wakitendewa kulingana na mbari zao na rangi, ubora wa ukoo ulizingatiwa kuwa ndio kigezo pekee. Watu hawakuthaminiwa kwa akili zao, elimu, uwezo, maadili na wema.
5. Hakukuwa na haki za msingi na uhuru. Haki za msingi kama vile uhuru wa dini na dhamiri, haki ya kumiliki mali, uhuru wa kupata makazi, uhuru wa fikra haukumhusu raia wa kawaida. Watu walikuwa wakidhulumiwa na kuteswa kutokana na imani zao na fikra.
6. Kanuni za msingi za sheria zilikandamizwa chini ya miguu. Haikuwezekana hata kufikiria dhana za sheria za msingi kama vile usawa mbele ya sheria, utawala wa sheria, haki ya kutoingiliwa (faragha) na uhalali wa adhabu. Hakukuwa na mahakama huru na isiyopendelea. Matakwa binafsi na amri ziliiweka kando sheria; watu waliotenda uhalifu uliofanana waliadhibiwa adhabu tofauti kwa kuzingatia matabaka yao.
Dunia ilipokuwa hatika hali hii, dini ya Uislamu ilikuja na kufanikisha mapinduzi makubwa katika historia ya mwanadamu.
Ikiangaliwa kwa macho yasiyo na upendeleo, itaonekana kuwa malengo makuu ya kibinadamu yanayoamuliwa sasa yalishaamuliwa katika Quran na katika Sunnah za Mtume Mtukufu kwa karne nyingi kabla ya matamko ya haki za kibinaadamu kutolewa katika ulimwengu wa Magharibi.
Kwa hakika, kanuni zinazohusu haki za kibinadamu zilizomo katika hotuba (Hotuba ya Kuaga) aliyohutubu Mtukufu Mtume (s.a.w) wakati wa Hajj ya Kuaga ni mfano wa wazi juu ya hilo.
Hotuba hiyo iliyosomwa katika hadhara ya Waislamu zaidi ya 100.000 mnamo mwaka 632 BK; yaani, miaka 1157 kabla ya Tamko la Haki za Mwanadamu na Raia kutolewa mwaka 1789, linalozingatiwa kuwa ni waraka wa kwanza wa kimaandishi unaohusu haki za kibinaadamu.
Kanuni hizo mpya zilizowekwa na Uislamu kuhusu haki za kibinaadamu zilikuwa ni zenye kuvutia mno juu ya kupigania haki za kibinaadamu huko Magharibi.
Mwanadamu ana thamani zaidi ya kipekee kuliko viumbe wengine. Thamani hiyo huongezeka anapomwamini Allah na kutii amri Zake. Hivyo, mwanadamu anakuwa mgeni mheshimiwa zaidi ulimwenguni. Mwanadamu anapata thamani ya utu anapozaliwa au hata kabla yake, kwa kuumbika kwake katika mji wa mimba, na anakuwa nayo katika maisha yake yote.
Thamani inayoanzia tokea kuwa mwanadamu inamwenea kila mmoja. Huruma hii imemzingira kila mmoja, mwanamume au mwanamke, mzee au kijana, mweusi au mweupe, mnyonge au mwenye nguvu, masikini au tajiri pasi na kujali dini, taifa, mbari na rangi zao.
Hivyo dini ya Uislamu inahifadhi damu ya kila mmoja isimwagwe, heshima isivunjwe, mali isiporwe, nyumba isiingiliwe bila ya ruhusa, ukoo usivunjwe na dhamiri kutokandamizwa. Inahakikisha heshima na hadhi ya kibinadamu.
Haki za msingi na uhuru ulioleta utu kutokana na Uislamu ni kama ifuatavyo:
1. Uislamu umemaliza ubaguzi wa kimbari na rangi. Watu wote wanatokana na Adam. Haiwezekani mtu kujichagulia mbari na rangi. Ni kudura ya Allah. Ni makosa makubwa na madhara makubwa kwa Uislamu na utu kuwabagua watu kwa rangi na mbari na kudharau baadhi ya mbari na rangi na kuwatazama wengine kuwa ni bora.
Allah anaeleza katika Quran kuwa amewaumba watu kutokana na mwanamume mmoja na mwanamke mmoja, na akawafanya mataifa na makabila wanapoongezeka ili waweze kujuana. (al-Hujurat, 13)
Kama ilivyoonekana, sababu ya watu kutofautiana kwa mbari na rangi ni kujuana na kusaidiana wala si kudai kuwa ni bora.
Tukio litakaloangazia ufahamu huu wa Uislamu ni kama ifuatavyo:
Swahaba Abu Dharr, siku moja alimkasirikia Bilal al-Habashi na akamtukana kwa kumwita, “mtoto wa mwanamke mweusi”. Abu Dharr alimdharau kwa sababu ya rangi ya mama yake. Mtume (s.a.w) alipoambiwa hayo, Mtume alikasirika na akamwambia Abu Dharr kama ifuatavyo:
— Ewe Abu Dharr! Umemshutumu Bilal kwa sababu ya rangi ya mama yake? Inamaanisha kuwa bado una fikra za Jahiliyya!"
Abu Dharr, ambaye alitamka maneno hayo kutokana na kushikwa na ghadhabu za ghafla bila ya kukusudia, alisikitikia sana alichofanya na akatubu. Alianza kulia, akalala chini na kuweka uso wake chini; kisha, akasema,
“Sitainua uso wangu kutoka ardhini isipokuwa mpaka Bilal aje kunikanyaga shavuni.” Akakariri kumwomba msamaha Bilal.
2. Uislamu umekomesha jambo la kujifaharisha kwa koo na mababu. Katika mkutano ambao Maswahaba walikuwepo, Sa'd bin Abi Waqqas aliwaomba baadhi ya Maswahaba mashuhuri wawaorodheshe wahenga wao. Wakati huo huo, aliwaorodhesha wahenga wake tokea mwanzo mpaka mwisho. Salman al-Farisi (Mwirani) pia alikuwepo hapo. Hakuwa na wahenga wa kujifaharisha nao kama wa-Qurayshi. Hakuwajua wahenga wake kwa kina, pia.
Sa'd bin Abi Waqqas alipomwomba awaorodheshe wahenga wake, hakupendezwa na ombi hilo na akasema, “Mimi ni Salman; mwana wa Uislamu. Siwajui wahenga wangu kama mlivyo nyinyi. Ninajua jambo moja tu. Allah amenitukuza kupitia Uislamu.”
Swahaba Umar pia aliudhiwa na jambo hilo lisilo la lazima la Sa’d lililoleta hisia za Jahiliyya. Alilipenda sana jibu hili lenye maana kubwa la Salman; akasema, “Mimi ni Umar; mwana wa Uislamu.” Hivyo, alitoa jibu sawa na la Salman.
Mtume (s.a.w) aliposikia habari za tukio hilo, alilipenda sana jibu la Salman. Akasema, “Salman ni katika mimi; anatoka katika familia yangu.”
Mtume aliwaozesha mabinti wa familia mashuhuri za wa-Quraysh kwa baadhi ya watumwa waliopewa uhuru miongoni mwa Maswahaba; hivyo, aliondosha fikra za Jahiliyya zilizoegemea ubora wa koo.
3. Uislamu umewapa watu haki ya kuangalia na kuwakagua watawala wao. Unalenga kumaliza vitendo vya kidikteta, uonevu, dhuluma na uhalifu.
Swahaba Abu Bakr alipoteuliwa kuwa Halifa, aliwahutubia watu kama ifuatavyo:
"Enyi watu! Nimeteuliwa kuwa ni kiongozi wenu ingawa mimi si mbora zaidi baina yenu. Kama nitatekeleza jukumu langu kulingana na Uislamu, nitiini. Kama nitaiacha njia sahihi, nionyeni."
Siku moja, wakati wa Ukhalifa wake, Swahaba Umar aliwauliza Waislamu msikitini, "Mtafanyaje kama nitaiacha njia sahihi? Wakasema, "Tutakusahihisha kwa mapanga yetu." Swahaba Umar akafurahi baada ya kusikia jibu hilo.
4. Uhuru wa fikra na dhamiri. Uhuru wa fikra na dhamiri ni haki muhimu zaidi baada ya haki ya kuishi. Kumnyima mtu haki hii kunamaanisha kumtoa katika utu wake na kumshusha mpaka katika kiwango cha wanyama. Kwa hiyo, Uislamu hauruhusu kukandamizwa fikra na dhamiri. Huku kukiwa na kanuni, “kusiwe na kulazimishana katika dini”, Uislamu haukuzingatii huko kufaa kuwafanya watu wakubali kanuni za imani kwa nguvu.
5. Uislamu umeshughulikia desturi ya utumwa kwa uangalifu sana na kulipa hilo ngazi ya kisheria.
Dini ya Uislamu ilipokuja, utumwa ulikuwa umeenea kote duniani pamoja na vitendo vyake viovu sana na vya kinyama. Uislamu kwa kawaida haukutarajiwa kuukomesha mfumo huo kikamilifu, ambao ulienea duniani kote. Kwa hivyo, haukukomesha utumwa kisiasa kali na kwa ghafla lakini ulirekebisha sana masharti na kuupa hali ya utu na ustaarabu zaidi. Licha ya hayo, Uislamu uliongeza na kurahisisha njia za uhuru na kuingiza kanuni ambazo zingekomesha utumwa kwa njia isiyo dhahiri.
6. Uhuru wa Mali. Kupenda vitu na tamaa ili kupata mali ni miongoni mwa hisia kadhaa ambazo Allah alimpa mwanadamu. Hili limeelezwa wazi katika Quran.
Uislamu umempa kila mtu haki ya mali na kuwaandalia namna ya kutimiza haja hii kihalali. Haki iliyowekwa na Uislamu kwa kila mmoja kuweza kumiliki mali kamwe haiwezi kuingiliwa bila ya idhini ya mwenyewe.
7. Usawa wa Kisheria. Uislamu unawatazama watu wote kwa usawa mbele ya sheria kama yalivyo meno ya kitana. Hauruhusu upendeleo unaozingatia hali ya kijamii na koo za watu.
Katika Uislamu, utawala wa sheria na sheria hiyo kuwa juu ni lazima. Mkuu wa dola na watu wa kawaida hutendewa sawa. Mhalifu kwa hakika huadhibiwa hata kama ni mkuu wa dola.
Kesi ya Fatih Sultan Mehmet na msanifu majengo wa Kigiriki, Swahaba Ali na Myahudi, Salahaddin al-Ayyubi na Mwarmenia katika hadhara ya makadhi ni mifano yenye kuvutia sana kuhusu jambo hili.
Katika siku ya ushindi wa Makkah, mwanamke mmoja kutoka familia mashuhuri ya kabila la Makhzum aliiba na kukamatwa nacho. Alipaswa kuadhibiwa. Hata hivyo, kwa kuwa alikuwa ni wa familia mashuhuri, hawakutaka familia hiyo kuaibika; kwa hivyo, walitaka mwanamke huyo asamehewe. Wangelifanyaje hilo? Wangemweleza nini Mtume kuhusu hilo? Hatimaye, waliamua kumtuma Usama, ambaye Mtume alimpenda sana, kwenda kwa Mtume. Usama alikwenda mbele ya Mtume na kumweleza suala hilo. Akamwomba Mtume amsamehe mwanamke mwenye hatia. Mtume alikasirika sana. Akatoka na kutoa hotuba ifuatayo ya kihistoria: “Enyi watu! Mnajua sababu za umma za kabla yenu kuangamizwa? Mtu wa hadhi ya juu alipotenda uhalifu, wao, walimwachilia. Mtu wa kawaida alipotenda kosa, kwa hasira walimtaka mtu huyo aadhibiwe. Ukandamizaji huu ulisababisha kuangamizwa kwao. Naapa kwa Allah, kama Fatima, binti wa Muhammad, angeiba, ningemwadhibu bila ya kusita.
Hapo, adhabu ilitimizwa.
Maneno yaliyo katika hotuba ya Swahaba Abu Bakr alipoteuliwa kuwa Khalifa hayana kifani.
"Walio dhaifu miongoni mwenu ndio wenye nguvu zaidi machoni mwangu mpaka wapate haki zao; wenye nguvu ni dhaifu sana machoni mwangu mpaka nichukue haki za wengine kutoka kwao."
8. Kutoingiliwa na Uhalali wa Adhabu. Katika Uislamu, hakuna adhabu bila ya sheria, na haiwezekani kumwadhibu mwingine badala ya mhalifu.
Kanuni ya kutoingiliwa na uhalali wa adhabu imeelezwa kama ifuatavyo katika sura al-Anam: "Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake. Na habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe." (Aya: 164)
9. Uhuru na Uadilifu wa Mahakama. Katika Uislamu, mahakama, ambazo ni taasisi za haki, zimeepushwa na kila namna ya msukuko kutoka nje, chuki binafsi na kinyongo, na matendo ya kidikteta; mahakimu hawaruhusiwi kupoteza uadilifu wao. Katika mahakama za Kiislamu, wakuu wa dola wameshitakiwa sambamba na raia wa kawaida; walikuwa wakiadhibiwa ikiwa walikutwa na hatia.
10. Kinga ya Makazi na Kutoingiliwa. Katika Uislamu, hakuna mwenye haki ya kumwingilia mtu na kuingia katika makazi yake bila ya idhini. Katika Uislamu kumekatazwa kupeleleza mambo ya faragha ya watu.
11. Uhuru wa Kusafiri. Uislamu unazingatia kuwa safari humsaidia mtu kujifunza mambo na kupona maradhi. Kwa hiyo, watu wanahamasishwa kusafiri.
12. Haki ya kuishi na kuhakikisha ulinzi wa uhai, mali na heshima. Hili limeelezwa vyema na Mjumbe wa Allah katika Hotuba ya Kuaga:
"Enyi Watu!, kama mnavyoutazama mwezi huu, siku hii, na mji huu, Makkah, kuwa ni mtukufu, basi utazameni uhai, mali na heshima ya kila Muislamu kuwa ni dhamana takatifu. Hayo yamehifadhiwa dhidi ya namna zote za ukiukwaji."
13. Hifadhi ya Kijamii. Dini ya Uislamu inamlinda mtu ili asipate tabu na asidhuriwe kwa uzee, ugonjwa, majanga, na ajali; unamhakikishia maisha mema ya baadaye wa masikini kwa njia za hifadhi ya kijamii ilizoziweka. Uislamu unawahimiza watu kufanya kazi kwanza ili waweze kujitunza wenyewe kifedha. Kwa kuongezea, umeweka hifadhi ya kipekee katika familia na baina ya majirani na shukrani ziende kwenye taratibu kadhaa ilizoziweka. Taratibu hizo zote za hifadhi zisipotosheleza, dola yenyewe inahakikisha hifadhi ya kila mmoja. Utaratibu wa zakah na taasisi zingine ndizo hifadhi za uhakika za kijamii.
14. Uhuru wa kazi, mishahara, haki na usawa. Kufanya kazi na kufanya juhudi kunatambuliwa na kuhimizwa katika Uislamu. Hakupendezi kuombaomba na kuwa ni mzigo kwa wengine. Kufanya kazi ili kupata riziki kwa njia halali kunazingatiwa kuwa ni ibada kama mtu huyo atakamilisha majukumu yake ya faradhi. Aya inayosema "Mtu huyo hatakuwa na kingine isipokuwa kile anachokipigania" inaonesha umuhimu ambao Uislamu umeweka kwenye bidii na kazi.
Kwa kuhakikisha uhuru wa kazi — kwa sharti kuwa imepatikana kihalali —, Uislamu unapanga mahusiano baina ya waajiriwa na mwajiri katika njia bora kabisa.
Kanuni ya "Mlipe mfanyakazi mshahara wake kabla jasho lake halijakauka" inahakikisha haki ya mfanyakazi katika njia kamilifu.
Kama ilivyo kanuni, mfanyakazi atajitaidi kufanya kikamilifu kazi aliyopewa na kwa namna bora zaidi na kustahiki mshahara anaoupata.
15. Ulinzi wa Watoto. Uislamu unawatunza watoto tangu kuzaliwa kwao, unawasaidia wazazi katika matumizi yao ya chakula na mavazi na unatenga mali kwa ajili yao kutoka hazina. Leo, dola zote tajiri huwapa ruzuku wazazi kwa ajili ya watoto. Mjumbe wa Allah alilisisitiza jeshi lake kutowaua wanawake na hususani watoto wakati wa vita.
16. Elimu ya Msingi ni Lazima na Bure. Hadithi inayosema, "Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila Muislamu, mwanamume na mwanamke" inaweka elimu ya lazima. Mtaala wa elimu ya msingi umeandaliwa kwa uangalifu katika Uislamu.
Pamoja na, elimu ya kidini, elimu ya kimaadili na ya kujua kusoma na kuandika, elimu ya ufundi imejumuishwa katika elimu ya msingi. Uislamu unaona kuwa ni lazima mtoto ajifundishe elimu ya ufundi pamoja na elimu ya dini.
Maswali juu ya Uislamu